杏MAP导航

Tafuta

Baba Mtakatifu Leo XIV ameendeleza hija ya matumaini ya watu wa Mungu kwa kunogeshwa na kauli mbiu mbiu “Kutumaini ni kuunganishwa” mintarafu mafundisho ya Mtakatifu Ireneo wa Lyon. Baba Mtakatifu Leo XIV ameendeleza hija ya matumaini ya watu wa Mungu kwa kunogeshwa na kauli mbiu mbiu “Kutumaini ni kuunganishwa” mintarafu mafundisho ya Mtakatifu Ireneo wa Lyon.  (@Vatican Media)

Papa Leo XIV Katekesi Mwaka wa Jubilei 2025: Injili ya Matumaini

Baba Mtakatifu Leo XIIV: Kauli mbiu “Kutumaini ni kuunganishwa” mintarafu mafundisho ya Mtakatifu Ireneo wa Lyon, Askofu na Mwalimu wa Kanisa aliyetengazwa na Hayati Baba Mtakatifu Francisko tarehe 21 Januari 2022 kuwa Mwalimu wa Kanisa katika Umoja: “Doctor unitatis.” Mtakatifu Ireneo ni maarufu sana katika mchakato wa majadiliano ya kiekumene, awe ni chachu kwa wafuasi wa Kristo Yesu kujikita katika mchakato wa umoja kamili miongoni mwa Wakristo!

LEONE XIV Udienza giubilare di sabato 14 giugno 2025 Catechesi e saluti

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Mababa wa Kanisa wanasema, Matumaini ni fadhila ya Kimungu inayowawezesha waamini kutamani heri ya Ufalme wa mbinguni na uzima wa milele kwa kutumainia ahadi za Kristo Yesu na kutegemea, siyo nguvu zao wenyewe, bali msaada wa neema ya Roho Mtakatifu kwa sababu Mwenyezi Mungu daima ni mwaminifu katika utekelezaji wa ahadi zake. Kwa njia ya Fumbo la Utatu Mtakatifu, waamini wanaweza kuhesabiwa haki kwa neema yake ili wapate kufanywa warithi wa uzima wa milele, kama tumaini lao. Fadhila ya matumaini inajibu tamaa ya heri ilivyowekwa na Mungu katika moyo wa kila mtu. Yachota matumaini yanayovuvia matendo ya watu. Huyatakasa ili kuyapanga kwa ajili ya Ufalme wa mbinguni nyakati za upweke. Hufungua moyo katika kungoja heri ya milele. Akielekezwa na matumaini anakingwa na ubinafsi na anaongozwa kwenye furaha itokanayo na mapendo. Matumaini ya Kikristo yanakita mizizi yake katika Heri za Mlimani ambazo kimsingi ni muhtasari wa mafundisho makuu ya Kristo Yesu kwa wanafunzi wake. Matumaini ni “nanga ya roho”, hakika na thabiti; ni silaha inayowalinda waamini katika mapambano ya wokovu. Matumaini ni fadhila ya Kikristo inayojikita katika unyenyekevu na nguvu ya kuweza kusonga mbele katika safari ya maisha, licha ya vikwazo na magumu yaliyopo. Matumaini kwa Mwenyezi Mungu kamwe hayawezi kumdanganya mwamini kwani Mwenyezi Mungu daima ni mwaminifu katika kutekeleza ahadi zake. Mungu ni chemchemi ya furaha na amani mioyoni mwa waja wake. Rej. KKK 1817-1821. Katekesi kuhusu: “Roho Mtakatifu na Bibi Arusi. Roho Mtakatifu anawaongoza watu wa Mungu kuelekea kwa Yesu, tumaini letu” ni sehemu ya Maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 2025 ya Ukristo yanayonogeshwa na kauli mbiu “Peregrinantes in spem” yaani “Mahujaji wa matumaini.”

Papa Leo XIV akisalimiana na mahujaji
Papa Leo XIV akisalimiana na mahujaji   (@Vatican Media)

Ni katika muktadha wa maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 2025 ya Ukristo, Kristo Tumaini letu, Baba Mtakatifu Leo XIV ameendeleza hija ya matumaini ya watu wa Mungu kwa kunogeshwa na kauli mbiu mbiu “Kutumaini ni kuunganishwa” mintarafu mafundisho ya Mtakatifu Ireneo wa Lyon, Askofu na Mwalimu wa Kanisa aliyetengazwa na Hayati Baba Mtakatifu Francisko tarehe 21 Januari 2022 kuwa Mwalimu wa Kanisa katika Umoja: “Doctor unitatis.” Mtakatifu Ireneo ni maarufu sana katika mchakato wa majadiliano ya kiekumene, awe ni chachu kwa wafuasi wa Kristo Yesu kujikita katika mchakato wa umoja kamili miongoni mwa Wakristo. Ireneo kwa lugha ya Kigiriki ni Ε?ρηνα?ο?, Eirēnáios, “Mtu wa Amani”; kwa Lugha ya Kilatini ni Irenaeus; aliyezaliwa huko Smirne, nchini Uturuki kunako mwaka 130 BK. Ni Askofu aliyejibidiisha kunogesha umoja wa Wakristo dhidi ya uzushi wa “Wagnos.” Alikazia Mapokeo na Imani ya Kitume. Katika maandishi yake alijitahidi sana kutetea imani ya Kanisa Katoliki inayokita mizizi yake katika Mapokeo ya Mitume wa Yesu dhidi ya uzushi wa mafundisho ya “Wagnos” yaliyotegemea zaidi ujuzi ambao yeyote alidai kuwa nao akianzisha kikundi chake. Ni kiongozi wa kwanza pia kushuhudia Injili Nne kuwa Neno la Mungu. Mtakatifu Ireneo Mwalimu wa Kanisa katika Umoja: “Doctor unitatis” alikuwa ni daraja la maisha ya kiroho na majadiliano ya kitaalimungu kati ya Makanisa ya Mashariki na Magharibi. Jina lake kama linavyoonesha, alikuwa ni mtu wa amani aliyetoka kwa Bwana, ili kuwapatanisha na hatimaye, Wakristo wote waweze kuwa wamoja. Mtakatifu Ireneo ni shuhuda na hujaji wa matumaini.

Injili ya Matumaini
Injili ya Matumaini   (@Vatican Media)

Ni katika muktadha wa maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 2025 ya Ukristo, Kristo Tumaini letu, mkazo unawekwa kwenye Injili ya matumaini mbele ya walimwengu na ya wapinga Kristo: “Ninyi basi, hilo mlilolisikia tangu mwanzo na likae ndani yenu. Ikiwa hilo mlilolisikia tangu mwanzo linakaa ndani yenu, ninyi nanyi mtakaa ndani ya Mwana, na ndani ya Baba. Na hii ndiyo ahadi aliyotuahidia, yaani, uzima wa milele.” 1Yn 2:24-25. Baba Mtakatifu Leo XIV Jumamosi, tarehe 14 Juni 2025 ameendeleza Katekesi kuhusu Maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 2025 mintarafu fadhila ya matumaini kadiri ya mafundisho na ushuhuda wa Mtakatifu Ireneo, Askofu na Mwalimu wa Kanisa. Haya ni matumaini yaliyorithishwa na Mitume wa Yesu tangu mwanzo, wakampokea Neno wa Mungu katika uhalisia wa maisha yao, kiasi kwamba, matumaini haya yanaunganishwa na Mwenyezi Mungu, kama ambavyo waamini wanasali kila siku “duniani kama mbinguni” na kwamba, hii ni chemchemi ya matumaini ya waamini. Mtakatifu Ireneo atawasaidia waamini jinsi ya kumwilisha matumaini haya katika hija ya maisha yao, ni kiongozi aliyejitahidi kuhakikisha kwamba, anainjilisha Bara la Ulaya. Kwa hakika Bara la Ulaya limeinjilishwa na watu kutoka nje ya Barala Ulaya, kama ilivyo kwa wakati huu, kwani kuna umati mkubwa wa wakimbizi na wahamiaji wanaotangaza na kushuhudia imani yao kwa Kristo Yesu na Kanisa lake wakiwa ughaibuni.

Mahujaji wa matumaini
Mahujaji wa matumaini   (@Vatican Media)

Mtakatifu Ireneo aliweza kuunganisha Ulaya Magharibi na Mashariki, alama ya matumaini, kwani kimsingi watu kutoka sehemu mbalimbali za dunia wanatajirishana. Mtakatifu Ireneo ana amana na utajiri mkubwa anaoweza kuwashirikisha waamini katika ulimwengu mamboleo. Ni kiongozi aliyeshuhudia kinzani za mafundisho ya imani ndani ya Jumuiya ya Wakristo; kinzani na madhulumu, lakini yote haya hayakumkatisha tamaa, akajikita zaidi na zaidi kumtangaza na kumshuhudia Kristo Yesu, akajikita zaidi katika kujenga na kudumisha umoja wa waamini, akimtangaza Kristo Yesu kuwa ni Mlango wa matumaini; Mlango unaowaunganisha waja wake, changamoto kwa waamini ni kuendelea kuunganika pamoja naye ili kuweza kung’amua ukweli na itikadi, kwani hata leo hii maneno yanaweza kuua. Fumbo la Mwili wa Kristo Yesu linapaswa kupokelewa na kutafakariwa katika maisha ya watu na kwa kila kiumbe. Huu ni mwaliko wa kusikiliza na kujibu kilio cha Mwili, watu watambue kwamba, wanaitwa kwa majina, ili kusikiliza na kujibu kilio cha mateso na mahangaiko ya jirani zao, kwa kumwilisha Injili ya upendo katika safari ya maisha yao. Amri hii imeandikwa katika mwili wao kuliko hata sheria nyingine yoyote.

Mahujaji wa matumaini, imani na mapendo
Mahujaji wa matumaini, imani na mapendo   (@Vatican Media)

Mtakatifu Ireneo Mwalimu wa Kanisa katika Umoja: “Doctor unitatis” awasaidie waamini na watu wote wenye mapenzi mema kutumia vyema akili yao, ili kuunganisha mambo msingi. Kristo Yesu ni chemchemi ya maisha ya uzima wa milele kati ya waja wake, ni chanzo cha umoja na ushirika. Waamini watambue kwamba, wao ni mahujaji wa matumaini, kwani hii ni changamoto kwa watu wote na kwa kila kiumbe, kujielekeza katika ujenzi wa ushirika, wengine watawafuata. Kama ilivyokuwa kwa Mtakatifu Ireneo wa Lyon wakati wa Karne ya Pili, kila mwamini ajitahidi kuwa ni mjenzi wa madaraja, ili kuvunjilia mbali kuta za utengano zilizojengwa katika miji. Baba Mtakatifu Leo XIV anawaalika waamini na watu wote wenye mapenzi mema kufungua malango ya maisha, waunganishe ulimwengu na hapo Injili ya matumaini itaweza kustawi.

Injili ya Matumaini
14 Juni 2025, 14:52