杏MAP导航

Tafuta

Jumanne tarehe 24 Juni 2025, Sherehe ya Kuzaliwa kwa Yohane Mbatizaji, Mama Kanisa ameadhimisha Jubilei ya Majandokasisi Jumanne tarehe 24 Juni 2025, Sherehe ya Kuzaliwa kwa Yohane Mbatizaji, Mama Kanisa ameadhimisha Jubilei ya Majandokasisi  (@Vatican Media)

Papa Leo XIV: Katekesi Makini Kwa Maadhimisho ya Jubilei ya Majandokasisi

Papa Leo XIV amewakumbusha kwamba, kwa nguvu walizojaliwa na Mungu wao wanawasha moto wa matumaini katika maisha na utume wa Kanisa. Ni mahujaji na mashuhuda wa matumaini, wanaitwa na kutumwa kupenda kama ilivyo kwa Moyo wa Yesu kwa kujikita katika maboresho ya maisha ya kiroho; wakijitahidi kumsikiliza Roho Mtakatifu, huku wakiendelea kukabiliana na changamoto mamboleo kama zile za matumizi ya teknolojia ya akili unde na mitandao!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Hayati Askofu mkuu Anthony Petro Mayala wa Jimbo kuu la Mwanza, Tanzania aliwahi kusema, seminari ni kitalu cha kuotesha miche ambayo inaweza kupandwa sehemu nyingine na hatimaye kuzaa matunda mema. Seminari ni Chuo cha kuwaandaa Mapadre na kwamba, familia zinapaswa kuwa ni kitalu cha miito mitakatifu. Wazazi na walezi wawekeze katika malezi na makuzi ya watoto wao ili Kanisa na jamii katika ujumla wake iweze kupata Mapadre wema, watakatifu, wanyoofu wa moyo na wachamungu. Kwa vile Mapadre ni waadhimishaji na wagawaji wa Mafumbo ya Kanisa, wanapaswa kujitakatifuza katika maisha yao, kwa kuambatana na Mwenyezi Mungu kwa njia ya Sala, Tafakari ya Neno la Mungu na Maisha ya Kisakramenti yanayomwilishwa katika huduma makini kwa watu wa Mungu.

Jubilei ya Majandokasisi 24 Juni 2025
Jubilei ya Majandokasisi 24 Juni 2025   (@Vatican Media)

Maadhimisho ya Jubilei ya Mwaka 2025 kwa ajili ya wakleri ni mwaliko kwa Mapadre kuishi mintarafu Daraja Takatifu ya Upadre, kwa njia ya ushuhuda wa maisha na utume wa Kipadre, wakitambua kwamba, kwa njia ya Daraja Takatifu ya Upadre wanashirikishwa maisha na utume wa Kristo Yesu, ili kufundisha, kuongoza na kuwatakatifuza watu wa Mungu. Mapadre wanapaswa kusimama kidete ili kuweza kuishi fadhila za maisha na utume wa Kipadre, kwa kujitahidi kuishi kama Kristo mwingine “Alter Christus” ili kwamba, waamini waweze kumtambua Kristo Yesu ndani mwao. Mapadre wanapaswa kuwa ni vyombo na mashuhuda wa matumaini yanayosimikwa katika huduma kwa watu wa Mungu, changamoto na mwaliko wa toba na wongofu wa ndani, ili kuwa kweli ni watangazaji wa matumaini na hivyo kuendelea kuliishi Fumbo la Pasaka, yaani: Mateso, kifo na ufufuko wa Kristo Yesu.

Papa Leo XIV akitoa Katekesi kwa Majandokasisi
Papa Leo XIV akitoa Katekesi kwa Majandokasisi   (@Vatican Media)

Mapadre wasimike maisha na utume wao katika Neno la Mungu na Sakramenti za Kanisa na kwamba, Roho Mtakatifu ni mhimili mkuu wa mchakato wa uinjilishaji wa kina unaogusa mahitaji ya mtu mzima: kiroho na kimwili. Mapadre katika ulimwengu mamboleo wanaendelea kukabiliana na changamoto pevu, kumbe, ni dhamana na wajibu wa waamini kumwomba Bwana wa mavuno ili apeleke watenda kazi wema, watakatifu, wenye ari, moyo na bidii ya kazi, ili kweli waweze kuwa ni mashuhuda na vyombo vya faraja na furaha kwa watu wa Mungu. Ni katika muktadha wa Maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 2025 ya Ukristo, tangu tarehe 23 hadi tarehe 27 Juni 2025 kunaadhimishwa matukio makuu matatu, yanayowashirikisha: Majandokasisi, Mapadre na Maaskofu kutoka sehemu mbalimbali za dunia.

Majandokasisi: Sala, Neno la Mungu, Liturujia na Sakramenti za Kanisa
Majandokasisi: Sala, Neno la Mungu, Liturujia na Sakramenti za Kanisa   (@Vatican Media)

Jumanne tarehe 24 Juni 2025, Sherehe ya Kuzaliwa kwa Yohane Mbatizaji, Mama Kanisa ameadhimisha Jubilei ya Majandokasisi, kwa kufanya hija na kupitia kwenye Mlango Mtakatifu wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican na baadaye kufuata Katekesi ya kina iliyotolewa na Baba Mtakatifu Leo XIV na kwa mara ya kwanza katika maisha na utume wake, amekutana na Majandokasisi kutoka sehemu mbalimbali za dunia. Baba Mtakatifu Leo XIV katika katekesi yake amewakumbusha kwamba, kwa nguvu walizojaliwa na Mwenyezi Mungu wao wanawasha moto wa matumaini katika maisha na utume wa Kanisa. Ni mahujaji na mashuhuda wa matumaini, wanaitwa na kutumwa kupenda kama ilivyo kwa Moyo Mtakatifu wa Yesu kwa kujikita katika maboresho ya maisha ya kiroho; wakijitahidi kumsikiliza Roho Mtakatifu, huku wakiendelea kukabiliana na changamoto mamboleo kama zile za matumizi ya teknolojia ya akili unde na matumizi ya mitandao ya kijamii. Wajenge moyo wa tafakari, usikivu sanjari na kuhifadhi yote wanayosikia kutoka kwa Mungu kama ilivyokuwa kwa Bikira Maria. Wajenge moyo wa unyenyekevu, wawe ni mashuhuda wa shukrani, sadaka, furaha na upendo, wajifunze kuwa na moyo wa Msamaria mwema na wajitahidi wanapokuwa masomoni kujifunza kwa juhudi, bidii na maarifa.

Majandokasisi wamepitia katika Lango kuu la Jubilei
Majandokasisi wamepitia katika Lango kuu la Jubilei   (@Vatican Media)

Baba Mtakatifu Leo XIV amewakumbusha Majandokasisi katika Maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 2025 ya Ukristo kwamba, wao ni mahujaji na mashuhuda wa matumaini tayari kutangaza na kushuhudia kwa unyenyekevu Habari Njema ya Wokovu inayookoa, katika kipindi hiki chenye changamoto nyingi katika maisha na utume wa Mapadre, lakini kama Majandokasisi wamekubali na kuitikia wito, changamoto kwao ni kuhakikisha kwamba, wanautekeleza wito huu kwa unyenyekevu na ujasiri; wahudumu katika Kanisa ambalo liko wazi na linalojikita katika umisionari mambo msingi katika maisha na utume wa Kanisa. Wajiachilie mikononi mwa Kristo Yesu mwenyewe ili aweze kuwasindikiza katika safari ya mang’amuzi, malezi na majiundo. Baba Mtakatifu anawaalika Majandokasisi kujenga na kudumisha urafiki mwema na Kristo Yesu; hali inayogusa maisha yao yote, kama mbegu inayozikwa ardhini, ili hatimaye, waweze kuwa ni Mapadre wenye furaha na madaraja yanayowakutanisha watu wa Mungu na hivyo kumwachia nafasi Kristo Yesu aweze kukua ndani mwao, ili hatimaye, wao waweze kuwa wachungaji wema mintarafu Moyo Mtakatifu wa Yesu.

Majandokasisi wakisali wakati wa Katekesi ya Jubilei
Majandokasisi wakisali wakati wa Katekesi ya Jubilei   (@Vatican Media)

Hayati Baba Mtakatifu Francisko, tarehe 24 Oktoba 2024 alichapisha Waraka wa Kitume unaojulikana kama "Dilexit nos” yaani “Alitupenda” Waraka wa Kitume juu ya upendo wa kibinadamu na wa Kimungu wa Moyo Mtakatifu wa Yesu Kristo.” Kristo Yesu aliwapenda waja wake upeo na kuwataka kutambua kuwa, hakuna jambo lolote linaloweza kuwatenga na upendo wake, kiasi kwamba aliwaita rafiki zake. Kristo Yesu anapenda kuwapatia waja wake upendo na urafiki na kwamba, “alitupenda sisi kwanza. Rej. 1Yn 4:10. Baba Mtakatifu Leo XIV anawataka Majandokasisi kuhakikisha kwamba, wanautumia vyema muda wa malezi na majiundo yao ya Kipadre, kwa kutoa kipaumbele cha kwanza katika moyo, yaani Seminari inapaswa kuwa ni shule inayojenga mahusiano na mafungamano bora ya kijamii. Lakini katika hali na mazingira ambamo kuna vita, uchoyo na ubinafsi, kuna haja ya kujifunza kupenda na kutenda kama Kristo Yesu aliyependa kwa moyo wa kibinadamu, changamoto na mwaliko wa kutoa kipaumbele katika ujenzi wa dhamiri nyofu, mahali ambapo Mwenyezi Mungu anazungumza na waja wake! Majandokasisi warejee katika undani wa nyoyo zao, jambo ambalo si rahisi sana kwani huko kuna madonda na majeraha, lakini pia kuna chembechembe za uwepo angavu wa Mungu, anayeganga na kuponya madonda haya, tayari kuwasindikiza wale wote wanaoteseka. Undani wa maisha bora ni msingi wa maisha ya kiroho, mahali ambapo Mwenyezi Mungu anazungumza na waja wake, yaani kutoka katika undani wa moyo wa mtu!

Maaskofu wanaoshiriki katika Jubilei ya Majandokasisi
Maaskofu wanaoshiriki katika Jubilei ya Majandokasisi   (@Vatican Media)

Baba Mtakatifu Leo XIV anawaalika Majandokasisi kujifunza na kubaini yale yanayojiri kutoka katika sakafu ya maisha yao ya ndani, wawe wepesi kuratibu hisia zao, sifa kubwa kwa vijana wa kizazi kipya, kwani hisia hizi zinasaidia kuratibu maisha yao na hivyo kuonesha uhalisia wa maisha yao. Undani wa maisha ya kiroho unafumbatwa katika Sala, ukimya na upweke chanya, ili kuweza hatimaye, kukutana na kuzungumza na Kristo Yesu na hivyo kujifahamu wao wenyewe. Majandokasisi waendelee kumtegemea Roho Mtakatifu, ili kusikiliza sauti ya Mungu katika hali na mazingira mbalimbali. Waweke bidii katika masomo ya Kitaalimungu, wajenge usikivu katika tamaduni za watu na waweze kusikiliza sauti zinazotoka katika tamaduni za watu; tayari kushughulikia changamoto mambolelo kama vile: matumizi ya teknolojia ya akili unde, pamoja na mitandao ya kijamii. Majandokasisi wajenge utamaduni wa kusikiliza na kujibu kilio cha maskini, wanyonge na wale wanao dhulumiwa katika jamii kama Kristo Yesu alivyofanya katika maisha na utume wake. Wawasikilize vijana wanaotafuta maana ya maisha. Majandokasisi wawe makini katika kulinda na kutunza nyoto zao kwa kujikita katika ukimya na tafakari na katika sala, wajifunze sanaa ya kufanya mang’amuzi. Wabebe ndani ya nyoyo zao ndoto na matamanio yao halali kama ilivyokuwa kwa Bikira Maria aliyeweka maneno hayo yote, akiyafikiri moyoni mwake. Rej. Lk 2:19. 51. Mkazo wa pekee ni katika Sala na tafakari ya kina ya Neno la Mungu; wawe wapole na wanyenyekevu wa moyo. Wajitahidi kukua na kukomaa kiutu, kihisia na katika mahusiano na mafungamano ya kijamii kwa kuondokana na unafiki katika maisha kwa kila jambo kulipatia jina lake kamili, daima wakijitahidi kujenga na kudumisha mahusiano na mafungamano na Mwenyezi Mungu.

Nafasi murua kabisa ya kukutana na kuzungumza na Majandokasisi
Nafasi murua kabisa ya kukutana na kuzungumza na Majandokasisi   (@Vatican Media)

Katika ulimwengu ambamo kuna uchu wa mali na madaraka, wao kama wahudumu wa Injili wanaitwa na kutumwa wawe ni mashuhuda wa moyo wa shukrani na sadaka ya Kristo Yesu; watu wenye furaha, mapendo na huruma kutoka moyoni; wakarimu na wenye kuonesha ukaribu wa Mungu katika maisha na huduma ya ukarimu pasi na uchoyo na ubinafsi, huku wakimwachia Roho Mtakatifu "kupaka mafuta" ubinadamu wao hata kabla ya kuwekwa wakfu kuwa ni Padre. Moyo Mtakatifu wa Kristo Yesu unahuishwa na huruma kubwa: yeye ni Msamaria Mwema wa wanadamu, mwaliko wa kutenda kama alivyotenda Yeye na hivyo kuyafanya maisha yao kuwa ni zawadi ya huruma na upendo. Baba Mtakatifu Leo XIV anasema, hekima ya Mama Kanisa akisaidiwa na Roho Mtakatifu, siku zote inatafuta mbinu zinazofaa zaidi kwa ajili ya malezi ya wahudumu wa Injili, mintarafu mahitaji ya mahalia. Baba Mtakatifu anawataka Majando kasisi kujiuliza maswali ya msingi mintarafu kazi, shauku ya maisha na utume wa Kipadre; kuishi kwa kuendelea kusoma alama za nyakati, ili kuangalia siku zijazo kwa moyo wa kinabii. Ni matumaini ya Baba Mtakatifu Leo XIV kwamba, mkutano wao utaendelea kuimarisha mazungumzo yao binafsi na Kristo Yesu ili kumwomba, awasaidie kuiga hisia za Moyo wake Mtakatifu, kielelezo cha upendo kwao na kwa binadamu wote.  

Jubilei ya Waseminari 2025
24 Juni 2025, 15:37