杏MAP导航

Tafuta

Kimsingi Askofu ni kielelezo cha umoja ndani ya Kanisa mahalia, Askofu ni kiongozi anayesimika maisha na utume wake katika taalimungu; ni mtu wa imani, matumaini, anayeongozwa na upendo na busara katika shughuli za kichungaji, Kimsingi Askofu ni kielelezo cha umoja ndani ya Kanisa mahalia, Askofu ni kiongozi anayesimika maisha na utume wake katika taalimungu; ni mtu wa imani, matumaini, anayeongozwa na upendo na busara katika shughuli za kichungaji,   (@Vatican Media)

Papa Leo XIV: Katekesi Jubilei ya Maaskofu: Sifa za Askofu

Askofu ni kielelezo cha umoja ndani ya Kanisa mahalia, Askofu ni kiongozi anayesimika maisha na utume wake katika fadhila za Kimungu; ni mtu wa imani, matumaini, anayeongozwa na upendo na busara katika shughuli za kichungaji, ni kiongozi anayemwilisha ufukara wa kiinjili katika utume wake bila kusahau: useja na kwamba, anahamasishwa kuhakikisha anamwilisha fadhila za kibinadamu zinazoheshimiwa katika jamii ya kibinadamu: wema wa moyo, & unyenyekevu.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Jubilei ya Mwaka 2025 ya Ukristo inanogeshwa na kauli mbiu “Peregrinantes in spem” yaani: “Mahujaji wa Matumaini.” Matumaini ya waamini yako katika Msalaba, yaani katika Kristo Yesu, chemchemi ya wokovu wa mwanadamu aliyezaliwa katika Familia Takatifu iliyopata baraka ya kuwa na Mungu yaani Emanueli kati yake. Ni katika muktadha wa Maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 2025 ya Ukristo, tangu tarehe 23 hadi tarehe 27 Juni 2025 kunaadhimishwa matukio makuu matatu, yanayowashirikisha: Majandokasisi, Mapadre na Maaskofu kutoka sehemu mbalimbali za dunia. Jumatano tarehe 25 Juni 2025, Mama Kanisa ameadhimisha Jubilei ya Maaskofu. Hawa ni Maaskofu kutoka katika nchi mbalimbali duniani. Wamekabidhiwa mavazi ya Ibada ya Misa takatifu kama sehemu ya Maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 2025 ya Ukristo, wakafanya hija ya maisha ya kiroho kuingia kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican na hapo wakaadhimisha Ibada ya Misa Takatifu iliyoongozwa na Kardinali Marc Armand Ouellet Mwenyekiti mstaafu wa Baraza la Kipapa la Maaskofu na Rais wa Tume ya Kipapa kwa ajili ya Amerika ya Kusini.

Papa Leo XIV Katekesi kwa Jubilei ya Maaskofu
Papa Leo XIV Katekesi kwa Jubilei ya Maaskofu   (ANSA)

Baadaye, Baba Mtakatifu Leo XIV ametoa katekesi ya kina, Maaskofu wakakiri imani yao kwa Kristo Yesu na Kanisa lake, chini ya Kaburi la Mtakatifu Petro, lililoko kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican. Baba Mtakatifu Leo XIV katika Katekesi yake amewakumbusha Maaskofu kwamba, Tamko la Maadhimisho ya Jubilei ya Mwaka 2025 ya Ukristo linanogeshwa na kauli mbiu “Spes non confundit" yaani “Tumaini halitahayarishi.” Rum 5:5 na kwamba, kiini cha maadhimisho haya ni matumaini yatakayowawezesha watu waaminifu wa Mungu kutoka sehemu mbalimbali za dunia kufanya hija ya maisha ya kiroho mjini Roma sanjari na maadhimisho haya kufanyika kwenye Makanisa mahalia, ili kukutana na Yesu aliye hai na mbaye pia ni Mlango wa uzima. Kimsingi Askofu ni kielelezo cha umoja ndani ya Kanisa mahalia, Askofu ni kiongozi anayesimika maisha na utume wake katika taalimungu; ni mtu wa imani, matumaini, anayeongozwa na upendo na busara katika shughuli za kichungaji, ni kiongozi anayemwilisha ufukara wa kiinjili katika maisha na utume wake, bila kusahau: useja na kwamba, anahamasishwa na Mababa wa Kanisa kuhakikisha kwamba, anamwilisha ndani mwake fadhila za kibinadamu zinazoheshimiwa katika jamii ya kibinadamu yaani: wema wa moyo, unyofu, uthabiti wa roho na saburi, juhudi kwa ajili ya haki, ukarimu pamoja na fadhila nyinginezo kama ambavyo zinafafanuliwa na Mtakatifu Paulo, Mwalimu na Mtume wa Mataifa: “Hatimaye, ndugu zangu, mambo yo yote yaliyo ya kweli, yo yote yaliyo ya staha, yo yote yaliyo ya haki, yo yote yaliyo safi, yo yote yenye kupendeza, yo yote yenye sifa njema; ukiwapo wema wo wote, ikiwapo sifa nzuri yo yote, yatafakarini hayo.” Flp 4:8.

Maadhimisho ya Jubilei ya Maaskofu 2025
Maadhimisho ya Jubilei ya Maaskofu 2025   (@Vatican Media)

Baba Mtakatifu Leo XIV katika Katekesi yake amewakumbusha Maaskofu kwamba, Tamko la Maadhimisho ya Jubilei ya Mwaka 2025 ya Ukristo linanogeshwa na kauli mbiu “Spes non confundit" yaani “Tumaini halitahayarishi.” Rum 5:5. Huu ni mwaliko kwa Maaskofu kuwa kweli ni mashuhuda wa matumaini yanayobubujika kutoka kwa Mwenyezi Mungu, mwaliko kwa Maaskofu kuwa karibu na kuendelea kuonesha mshikamano na wale wanaoteseka, ili Roho Mtakatifu aweze kupyaisha tena ule moto wa matumaini uliokuwa unaonekana kufifia. Maaskofu wanaalikwa kuwa ni watu wa huduma, huku wakiendelea kujitambulisha na kutoa ushuhuda wenye mvuto na mashiko katika maisha na utume wa Kristo Yesu. Itakumbukwa kwamba, Askofu mahalia ni kielelezo cha umoja katika Kanisa na kwamba, ndiye anayejenga na kudumisha umoja kati ya watu wote wa Mungu pamoja na Kanisa la Kiulimwengu, ili kukua na kukomaa kwa Kanisa, tayari kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu. Askofu ni mwalimu wa imani, anatakatifuza, na ni kiongozi wa maisha ya kiroho na kwamba, ni mragibishaji wa Ufalme wa Mungu kwa ajili ya wokovu, ili kuleta mabadiliko mintarafu nguvu ya Injili.

Papa Leo XIV akiwa katikati ya Maaskofu
Papa Leo XIV akiwa katikati ya Maaskofu   (@Vatican Media)

Mababa wa Kanisa wanasema kwamba, fadhila ni tabia ya kawaida na imara ya kutenda mema. Yamruhusu mtu si kutenda mema tu bali kutoa kilicho chema kabisa cha nafsi yake. Mtu wa fadhila huelekea mema kwa hisi zake zote pamoja na nguvu za kiroho. Hutafuta mema na kuyachagua kwa matendo halisi. Kuna fadhila za kibinadamu ambayo ni hali thabiti, maelekeo imara, ukamilifu wa kawaida wa akili na utashi zinazotawala matendo ya binadamu, zinazoratibu harara na kuongoza mwenendo kufuata akili na imani. Zinawezesha raha, kujitawala na furaha katika kuishi maisha mema kimaadili. Fadhila adili hupatikana kwa juhudi za kibinadamu kuungana na upendo wa Mungu. Shabaha ya mtu mwenye fadhila ni kuwa kama Mungu. Kuna fadhila kuu ambazo hutenda kazi kama bawaba nazo ni: Busara, haki, nguvu, na kiasi. Rej. KKK 1803-1803. Kuna fadhila tatu za Kimungu: imani, matumaini na mapendo. Askofu anaongoza maisha yake kwa fadhila za Kimungu. Askofu ni mtu na shuhuda wa imani na kwamba, moyo wake daima unawaka imani. Askofu ni mtu wa matumaini na faraja kwa watu waliovunjika na kupondeka moyo, ni kiongozi anaye shuhudia uzoefu na mang’amuzi yake katika maisha ya kijumuiya, kwa wale wote wanaotamani kuinishi tunu msingi za Kiinjili. Askofu ni mtu anayeongozwa na upendo wa shughuli za kichungaji “amoris officium” katika mahubiri yake, anapofanya ziara za kichungaji, anapokutana na kuzungumza na Mapadre wake.

Sifa kuu za Askofu zinafumbatwa katika fadhila za Kimungu
Sifa kuu za Askofu zinafumbatwa katika fadhila za Kimungu   (@Vatican Media)

Askofu ni kiongozi anaye chota nguvu katika maadhimisho ya Fumbo la Ekaristi Takatifu na Maisha ya Sala, ni mfano bora wa kuigwa katika kujenga na kudumisha udugu wa kibinadamu, katika ukweli, uwazi na ukarimu. Baba Mtakatifu Leo XIV amekazia kuhusu busara ya kichungaji kwa kuthamini Jimbo lake na Mapokeo, tayari kuanzisha njia mpya. Askofu anaitwa kuwa ni shuhuda wa ufukara wa Kiinjili, kwa kutokubali kumezwa na mali pamoja na malimwengu na kwamba, anaitwa na kutumwa kuwatangazia maskini Habari Njema ya Wokovu. Rej. Lk 4:18. Askofu anapaswa kuishi kikamilifu useja na usafi wa moyo wa Kiinjili, kwa kuepuka kuwa ni chanzo cha makwazo na kashfa. Askofu anapaswa kuwa ni mtu anayesimika maisha na utume wake katika ukweli na uwazi; kwa kufurahi na wale wanaofurahi; ni mtu mwenye uvumilivu, anayesimika maisha yake katika kusikiliza na kujadiliana, tayari kujisadaka kwa ajili ya huduma. Hizi ni karama ambazo Askofu anapaswa kuzipalilia katika maisha na utume wake, kwa neema ya Roho Mtakatifu. Mwishoni mwa Katekesi yake, Baba Mtakatifu Leo XIV amewakabidhi Maaskofu wanaoadhimisha Jubilei yao chini ya ulinzi na tunza ya Bikira Maria Mama wa Kanisa na ya Mtakatifu Petro na Paulo, ili wawasaidie kuwa ni watu wanaosimika maisha yao katika umoja wa watu wa Mungu, udugu wa kibinadamu na urafiki. Haya ni mambo ambayo yanawawezesha wakleri katika maisha na shughuli zao za kichungaji kukuza na kudumisha umoja wa Kanisa mahalia.

Jubilei ya Maaskofu
25 Juni 2025, 16:21