Papa Leo XIV: Hotuba Kwa Wajumbe wa Mkutano Mkuu wa 98 wa ROACO
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Injili ya huduma upendo ni sehemu ya vinasaba vya maisha na utume wa Kanisa! Kanisa linaitwa na kutumwa kuonesha Uso wa huruma ya Mungu kwa familia ya Mungu huko Mashariki ya Kati, ili kuwaganga na kuwahudumia kwa mafuta ya faraja na divai ya matumaini, watu waliovunjika na kupondeka moyo kutokana na: vita, chuki, dhuluma, nyanyaso, ubaguzi, umaskini wa hali na kipato. Mama Kanisa anatumwa kutangaza Injili ya furaha na matumaini yanayobubujika kutoka katika Moyo wa Mungu. Hawa ni mashuhuda wa imani kwa Kristo Yesu na Kanisa lake, wenye amana na utajiri wa tamaduni na Mapokeo mbalimbali. Makanisa ya Mashariki bado yanaendelea kuvuja damu, kama hali inavyojionesha huko kwenye Ukanda wa Gaza, Mashariki ya Kati na nchini Ukraine. Kuna haja ya kutafuta na hatimaye kupata suluhu ya kudumu ya vita hii inayoendelea kusigina utu, heshima na haki msingi za binadamu. Kwa hakika, watu hawawezi kuendelea kupoteza maisha kutokana na habari za kughushi.
Hii ni sehemu ya hotuba iliyotolewa na Baba Mtakatifu Leo XVI kwa wajumbe wa Shirikisho la Mashirika ya Misaada kwa Makanisa ya Mashariki, ROACO, waliokuwa wanahudhuria mkutano mkuu wa 98 ulioanza tarehe 23 hadi tarehe 26 Juni 2025. Baba Mtakatifu Leo XIV anasema kuna haja kwa Jumuiya ya Kimataifa kujikita katika utekelezaji wa Sheria za Kimataifa, kwa kukazia misingi ya haki, amani na maridhiano; ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Ikumbukwe kwamba, hakuna taifa linaloweza kujigamba kwamba, ni bora kuliko watu wengine. Inasikitisha kuona kwamba, kuna kiasi kikubwa cha fedha kinachowekezwa kwenye utamaduni wa kifo: yaani biashara haramu ya silaha, kwani fedha hii, ingeweza kuwekezwa kwenye maboresho na ujenzi wa hospitali na shule, lakini silaha hizi zinatumika kubomoa hata zile shule na hospitali zilizokwisha kujengwa. Kuna haja ya kupaaza sauti, kusali na kuomba, kutangaza na kushuhudia Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo, kama alivyofanya Mfalme Herodi na Ponsio Pilato.
Kristo Yesu anawaalika waja wake kuganga na kuponya madonda ya historia ya mwanadamu, kwa unyenyekevu na utukufu wa Msalaba, kwa nguvu ya msamaha na matumaini, tayari kuanza upya kwa kujikita katika ukweli na uwazi, ili hatimaye kushinda kishawishi cha rushwa na ufisadi wa mali ya Kanisa; chuki na mipasuko ya kijamii. Baba Mtakatifu Leo XIV anawahamasisha Wakristo huko Mashariki ya Kati waendelee kubaki katika maeneo yao kama mashuhuda wa Kristo Yesu. Baba Mtakatifu amesikitishwa na shambulizi la kigaidi lililofanywa kwenye Kanisa la Mtakatifu Elia, huko Damasko. Anawaalika kuthamini na kuenzi uzuri wa Liturujia ya Makanisa ya Mashariki, Muziki na Maadhimisho ya Mafumbo ya Kanisa yanayosimikwa katika toba na msamaha wa kweli; wawe kweli ni mashuhuda wa mwanga huko Mashariki ya Kati ambako kwa sasa giza linaonekana kutawala. Katika mwanga wa hekima ya wokovu, Makanisa ya Mashariki yanapaswa kujenga na kudumisha umoja na ushirika, kwa kupenda, kwa kutambua amana na utajiri wa Mamlaka Fundishi ya Kanisa, kwa kuendelea kutoa malezi na majiundo mintarafu Makanisa ya Mashariki na Magharibi katika vitivo na vyuo vikuu vinavyoendeshwa na kusimamiwa na Kanisa. Viongozi wa Makanisa washirikishane sera, mipango na mikakati ya shughuli za kichungaji, ili kukuza na kudumisha utakatifu wa maisha, imani ya Kanisa Katoliki kwa wahamiaji na wakimbizi wanaolazimika kuishi mbali na nchi zao.