杏MAP导航

Tafuta

Baba Mtakatifu Leo XIV ameonesha hofu kwa kile kinachoendelea huko Mashariki ya Kati, bila kusahau vita kati ya Israeli na Palestina, ambako dharura na mahitaji msingi ya binadamu yanaendelea kuongezeka Ukanda wa Gaza. Baba Mtakatifu Leo XIV ameonesha hofu kwa kile kinachoendelea huko Mashariki ya Kati, bila kusahau vita kati ya Israeli na Palestina, ambako dharura na mahitaji msingi ya binadamu yanaendelea kuongezeka Ukanda wa Gaza.  (AFP or licensors)

Papa Leo XIV: Hofu ya Vita Kati ya Israeli, Iran na Marekani: Wajibu wa Kimaadili

Baba Mtakatifu Leo XIV anasema, hakuna mgogoro unaoweza kuonekana kuwa ni wa “mbali”, wakati heshima, utu na haki msingi za binadamu ziko hatarini na zinaendelea kusiginwa! Vita kamwe haisuluhishi shida, matatizo na migogoro ya Kimataifa, bali inakuza na kuzalisha majeraha makubwa katika maisha na historia ya watu wa Mungu, mambo ambayo huchukua miaka mingi ili kuweza kupona. Jumuiya ya Kimataifa ina dhamana na wajibu wa kimaadili wa kujenga amani.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Tangu vita kati ya Israeli, Iran na Marekani vianze taarifa zinaonesha kwamba kuna watu zaidi ya 865 waliofariki dunia na wengine 3, 396 wamejeruhiwa vibaya katika vita hii, ambayo hapo awali ilikuwa ni kati ya Israeli na Iran, lakini Marekani pia imejiingiza na kushambulia vinu vya nyuklia vya Iran vilivyoko katika maeneo ya Fordow, Natanz na Isfaham. Hili ni tukio ambalo Iran imeahidi kulipiza kisasi na hivyo kupelekea hali ya ulinzi na usalama kwa Jumuiya ya Kimataifa kuendelea kuwa tete sana. Ni katika muktadha huu wa vita kati ya Israeli, Iran na Marekani, Baba Mtakatifu Leo XIV ameonesha hofu na wasiwasi mkuu kwa kile kinachoendelea huko Mashariki ya Kati, bila kusahau vita kati ya Israeli na Palestina, ambako dharura na mahitaji msingi ya binadamu yanaendelea kuongezeka maradufu huko katika Ukanda wa Gaza.

Jumuiya ya Kimataifa ina wajibu wa kimaadili kuzuia vita duniani
Jumuiya ya Kimataifa ina wajibu wa kimaadili kuzuia vita duniani

Hayo yamesemwa na Baba Mtakatifu Leo XIV, Dominika tarehe 22 Juni 2025 wakati wa Sala ya Malaika wa Bwana kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, sanjari na maadhimisho ya Sherehe ya Ekaristi Takatifu. Baba Mtakatifu anasema, leo kuliko wakati mwingine wowote katika historia ya mwanadamu, watu wanalia na kuomba amani. Hiki ni kilio kinacho dai uwajibikaji na matumizi sahihi ya akili na wala si lazima kizimwe au kukatishwa na miungurumo ya silaha na maneno ya kejeli yanayochochea vita na migogoro. Kila mwanachama wa Jumuiya ya Kimaitafa ana wajibu na dhamana ya kimaadili: kukomesha janga la vita, kabla halijawa pengo lisiloweza kurekebishwa.

Madhara ya vita
Madhara ya vita   (ANSA)

Baba Mtakatifu Leo XIV anasema, hakuna mgogoro unaoweza kuonekana kuwa ni wa “mbali”, wakati heshima, utu na haki msingi za binadamu ziko hatarini na zinaendelea kusiginwa! Vita kamwe haisuluhishi shida, matatizo na migogoro ya Kimataifa, bali inakuza na kuzalisha majeraha makubwa katika maisha na historia ya watu wa Mungu, mambo ambayo huchukua miaka mingi ili kuweza kupona. Hakuna ushindi wa silaha unaoweza kulipa fidia kwa maumivu watu na hofu ya watoto wao kwa siku za usoni; siku mbazo zimepokwa kutoka kwa watoto hawa. Kuna haja kwa Jumuiya Kimataifa kujikita zaidi katika diplomasia ya amani na kunyamazisha silaha na kwamba, kuna haja kwa Mataifa kujikita kwa vitendo katika kutafuta na kudumisha amani, ili kukomesha vita na migogoro inayopelekea umwagaji wa damu ya watu wasiokuwa na hatia.  

Papa Leo XIV Vita
22 Juni 2025, 13:29