杏MAP导航

Tafuta

2025.06.07 Washiriki katika Kongamano la Kiekumene lililotolewa kwa ajili ya Maadhimisho ya Miaka 1700 ya Mtaguso wa Nicea. 2025.06.07 Washiriki katika Kongamano la Kiekumene lililotolewa kwa ajili ya Maadhimisho ya Miaka 1700 ya Mtaguso wa Nicea.  (@Vatican Media)

Papa Leo XIV:Mtaguso wa Nicea ni dira kuelekea umoja kamili wa Wakristo wote!

Baba Mtakatifu Leo XIV akikutana na washiriki wa Kiekumene wa Kongamano kuhusu:“Necea na Kanisa la Milenia ya tatu;kuelekea umoja wa Kikatoliki-Kiorthodox,Papa alithibitisha uwezekano wa kuadhimisha pamoja Pasaka na kukumbusha kuwa umoja ni zawadi tuliyopokea kwa nia ya tendo la Roho.Ni katika muktadha wa Maadhimisho ya Miaka 1700 ya Mtaguso wa Nicea mwaka huu.

Na Angella Rwezaula – Vatican.

Baba Mtakatifu Leo XIV Jumamosi asubuhi tarehe  7 Juni 2025  akikutana na washiriki wa Kongamano lenye mada: “Nicea na Kanisa la Milenia ya tatu: kuelekea umoja Katoliki na Orthodox”, alijikita kufafanua juu ya mada kuu tatu: Imani ya Mtaguso wa Nicea, Sinodi na tarehe ya Pasaka. Hizi ndizo zilikuwa mada ambazo zimekabiliwa katika Kongamano lao lililoanza tangu Juni 4 na kuhitimishwa mchana tarehe 7 Juni 2025 katika Taasisi ya Kipapa ya Chuo Kikuu cha Mtakatifu Thomas wa Aquino,  kwa kuandaliwa na ?cumenicum ambayo ni Taasisisi ya Mafunzo ya Kiekumene -Angelicum na Chama cha Taalimungu cha Kiorthodox kimataifa. Baba Mtakatifu  Leo XIV alizungumza kwa lugha ya kiingereza ambapo awali yote aliomba samahani ya kuchelewa kwa sababu ni karibu mwezi anajaribu kukabiliana na majukumu hayo mapya, kwa hivyo alisema kuna uzoefu mwingi wa kujifunza. Lakini alikuwa na furaha sana kuwa nao asubuhi hiyo. Kisha akaeleza kuridhika kwake kwa kubainisha jinsi Kongamano hilo linavyoelekezwa kuelekea siku zijazo.

Kongamano  kuhusu Nicea
Kongamano kuhusu Nicea   (@Vatican Media)

Papa aliendelea kusema kuwa Mtaguso wa Nicea si tukio la zamani tu bali ni dira ambayo lazima iendelee kutuongoza kuelekea kwenye umoja kamili unaoonekana wa Wakristo. Mtaguso wa Kwanza wa Kiekumene ni msingi wa safari ya pamoja ambayo Wakatoliki na Waorthodox wameifanya pamoja tangu Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican. Kwa Makanisa ya Mashariki, ambayo huadhimisha adhimisho lake katika kalenda yao ya kiliturujia, Mtaguso wa Nicea si Baraza moja tu kati ya mengine au la kwanza katika mfululizo, bali ni Baraza la ubora, ambalo lilitangaza kanuni ya imani ya Kikristo, ungamo la imani la “Mababa 318.” Mada  tatu za Kongamano lao Papa alisisitiza kuwa zinafaa hasa kwa safari yetu ya kiekumene.

Kwanza, imani ya Nicea. Kama Tume ya Kimataifa ya Kitaalimungu  ilivyoona katika Hati yake ya hivi karibuni ya ukumbusho wa 1700 wa Nicea, mwaka 2025 inawakilisha "fursa muhimu sana ya kusisitiza kwamba, kile tunachofanana kina nguvu zaidi, kiasi na ubora, kuliko kile kinachotugawanya. Kwa pamoja, tunaamini katika Mungu wa Utatu, katika Kristo kama mwanadamu na Mungu wa kweli, na katika wokovu kupitia Yesu Kristo, kulingana na Maandiko yanayosomwa katika Kanisa na chini ya uongozi wa Roho Mtakatifu. Kwa pamoja, tunaamini katika Kanisa, ubatizo, ufufuko wa wafu, na uzima wa milele.” (Yesu Kristo, Mwana wa Mungu, Mwokozi, n. 43). Papa Leo XIV amebainisha kuwa anayo hakika kwamba kwa kurudi kwenye Mtaguso wa Nicea na kuunganisha kutoka chanzo hicho cha pamoja, tutaweza kuona kwa nuru tofauti mambo ambayo bado yanatutenganisha. Kupitia mazungumzo ya kitaalimungu na kwa msaada wa Mungu, tutapata ufahamu mzuri zaidi wa fumbo linalotuunganisha. Kwa kusherehekea pamoja imani hii ya Nicea na kwa kuitangaza kwa pamoja, pia tutasonga mbele kuelekea urejesho wa ushirika kamili kati yetu.

Kongamano la Nicea
Kongamano la Nicea   (@Vatican Media)

Mada ya pili ya Kongamano lao ni sinodi. Mtaguso wa Nicea ulizindua njia ya sinodi kwa Kanisa kufuata katika kushughulikia masuala ya kitaalimungu na kanuni katika ngazi ya ulimwengu mzima. Mchango wa wajumbe ndugu kutoka Makanisa na jumuiya za kikanisa za Mashariki na Magharibi katika Sinodi ya kisinodi iliyofanyika hivi karibuni hapa mjini Vatican ilikuwa ni kichocheo chenye thamani kubwa cha kutafakari zaidi asili na utendaji wa sinodi.  Hati ya Mwisho ya Sinodi ilibainisha kwamba “mazungumzo ya kiekumene ni msingi kwa ajili ya kukuza uelewa wetu wa sinodi na umoja wa Kanisa” na iliendelea kuhimiza maendeleo ya “matendo ya sinodi ya kiekumene, ikijumuisha aina za mashauriano na utambuzi juu ya maswali ya pamoja na ya dharura” (Kwa ajili ya Kanisa la Sinodi:Umoja,  ushiriki, Utume n. 138). Kwa njia hiyo ni matumaini ya Papa Leo XIV kwamba, maandalizi na ukumbusho wa pamoja wa ukumbusho wa miaka 1700 wa Mtaguso wa Nicea  litakuwa tukio la majaliwa "kuimarisha na kukiri pamoja imani yetu katika Kristo na kuweka katika vitendo aina za sinodi miongoni mwa Wakristo wa tamaduni zote" (taz. 139).

Kongamano hilo pia lilizungumzia mada ya tatu ikiwa ni kuhusu tarehe pamoja ya Pasaka. Papa Leo XIV alibainisha kuwa kama tujuavyo, moja ya malengo ya Mtaguso wa Nicea lilikuwa kuanzisha tarehe ya pamoja ya Pasaka ili kueleza umoja wa Kanisa katika oikoumene.  Cha kusikitisha ni kwamba, tofauti katika kalenda hizo haziruhusu tena Wakristo kusherehekea pamoja sikukuu muhimu zaidi ya mwaka wa kiliturujia, na kusababisha matatizo ya kichungaji ndani ya jumuiya, kugawanya familia na kudhoofisha uaminifu wa ushuhuda wetu kwa Injili. Masuluhisho kadhaa madhubuti yamependekezwa ambayo, ingawa yanaheshimu kanuni ya Nicea, yangeruhusu Wakristo kusherehekea pamoja "Sikukuu ya Sikukuu."

Kongamano la Nicea
Kongamano la Nicea   (@Vatican Media)

Baba Mtakatifu Leo XIV alisisitiza kuwa katika mwaka huu, wakati Wakristo wote wamesherehekea Pasaka siku hiyo hiyo, walithibitisha tena uwazi wa Kanisa Katoliki katika kutafuta ufumbuzi wa kiekumene unaopendelea sherehe ya pamoja ya ufufuko wa Bwana na hivyo kutoa nguvu kubwa ya kimisionari kwa mahubiri yetu ya “jina la Yesu na wokovu uliozaliwa kwa imani katika ukweli unaookoa wa Injili” (Hotuba kwa Mashirika ya Kipapa ya kimisionari 22Mei 2025). Kwa njia hiyo Baba Mtakatifu alisisisitiza kuwa “katika fursa ya mkesha huu wa Pentekoste, tukumbuke kwamba umoja ambao Wakristo kwa muda mrefu hautakuwa hasa matunda ya juhudi zetu wenyewe, wala hautapatikana kupitia kielelezo au ramani iliyotungwa. Badala yake, umoja utakuwa zawadi inayopokelewa “kama Kristo apendavyo na kwa njia apendayo” (Sala kwa ajili ya Umoja ya  Padre Paul Couturier), kwa utendaji wa Roho Mtakatifu. Na kwa hivyo, Papa aliwaalika wote kusimama ili kusali  pamoja na kusihi karama ya Roho ya umoja. Sala ya kuomba umoja wa Roho katika maombi ambayo yanatokana na mapokeo ya Mashariki:

Ewe Mfalme wa Mbinguni, Mfariji, Roho wa Kweli, Ambaye yuko kila mahali na anajaza vitu vyote. Hazina ya Baraka, na Mpaji wa Uzima, Njoo ukae ndani yetu, na utusafishe na kila uchafu na uokoe nafsi zetu, Ewe Mwema.” Amina.

Kwa kuhitimisha, na Baraka Papa Leo XIV alisema: "Bwana awe nanyi. Baraka za Mwenyezi Mungu, ya Baba, Mwana na Roho Mtakatifu iwashukie na  na kukaa nanyi milele. Amina. Asante sana.

Kongamano la Nicea
Kongamano la Nicea   (@Vatican Media)
MTAGUSO WA NICEA
07 Juni 2025, 15:17