Papa anatoa wito kwa utamaduni wa kutovumilia dhuluma katika Kanisa
Na Salvatore Cernuzio – Vatican.
Katika ujumbe dhidi ya aina zote za unyanyasaji, Baba Mtakatifu Leo XIV alitoa wito wa mabadiliko ya kiutamaduni ndani ya Kanisa Katoliki. "Ni lazima kueneza katika Kanisa utamaduni wa kuzuia ambao hauvumilii aina yoyote ya unyanyasaji: matumizi mabaya ya mamlaka au madaraka, dhamiri au kiroho, unyanyasaji wa kijinsia", aliandika. Maneno yake yalisomwa katika onesho la igizo la Proyecto Ugaz, linaloendeshwa kwa sasa huko Lima nchini Peru. Mchezo huo unamsifia mwanahabari mpelelezi Paola Ugaz, anayejulikana kwa kuripoti juu ya Sodalitium ambayo sasa imekandamizwa, na ambaye amekabiliwa na unyanyasaji wa kudumu kwa kazi yake. Akitumia kielelezo cha Ugaz, Papa alitoa utetezi thabiti wa uhuru wa vyombo vya habari kwamba:“Popote pale mwandishi wa habari anaponyamazishwa, nafsi ya kidemokrasia ya taifa hudhoofika.”
Ujumbe wa Papa unajikita katika mada kuu mbili ambazo ni msingi wa utayarishaji wa tamthilia: mapambano dhidi ya unyanyasaji na jukumu muhimu la uandishi wa habari wa ukweli na huru. Proyecto Ugaz inaakisi uchunguzi wa miaka mingi wa Ugaz katika Sodalitium Cristianae Vitae, Harakati lenye nguvu la walei katika Amerika ya Kusini ambalo Papa Francisko alilikandamiza rasmi Aprili 14 kutokana na tuhuma nyingi za unyanyasaji na ufisadi, ikiwa ni pamoja na dhidi ya mwanzilishi wake, Luis Figari. Uchunguzi wa Vatican ulihitimisha kikundi hicho hakina karama yoyote ya kimsingi. Paola Ugaz, pamoja na mwandishi wa habari Pedro Salinas, waliandika pamoja kitabu mnamo 2015 kinachofichua ushuhuda kutoka kwa waathiriwa wa Sodalitium. Kazi yao ilichochea uchunguzi wa mamlaka ya Peru na hatimaye ikapelekea Vatican kuingilia kati. Hata hivyo, Ugaz tangu wakati huo amekabiliwa na unyanyasaji wa kisheria na mashambulizi ya mtandaoni.
Mnamo Novemba 2022, alitafuta ulinzi kwa ajili yake na waandishi wengine watatu wa habari kutoka kwa Papa Francisko, ambaye aliwapokea kibinafsi mnamo Desemba mwaka huo na kuelezea msaada wake. Sasa, chini ya Papa Leo XIV, msaada huo unaendelea na kuongezeka. Papa, mwenye ufahamu wa kutosha juu ya kesi ya Sodalitium na jukumu la Ugaz, alimkumbatia hadharani wakati wa mkutano wa mwezi Mei na waandishi wa habari walioakisi mkutano huo. Picha ya Ugaz akimkabidhi Papa skafu ya kitamaduni ya Andean ("chalina") ilinaswa wakati huo. Ni kwa hafla hiyo-iliyofanyika siku nne baada ya kuchaguliwa kwake-ambapo Papa Leo XIV alirejea katika ujumbe wake, uliosomwa kwa sauti kwenye jumba la maonyesho na Bi. Jordi Bertomeu wa Baraza la Kipapa la Mafundisho Tanzu ya Kanisa na kamishna wa kitume wa kesi ya Sodalitium.
Papa Leo XIV alianza ujumbe wake kwa maneno matatu ya shukrani: Kwa waundaji wa Proyecto Ugaz, akiita utayarishaji "sio tu ukumbi wa michezo, lakini kumbukumbu, maandamano, na zaidi ya yote, kitendo cha haki," akitoa sauti kwa "uchungu ulionyamazishwa kwa muda mrefu." “Waathiriwa wa familia ya zamani ya kiroho ya Sodalitium, pamoja na waandishi wa habari waliowaunga mkono kwa ujasiri, subira, na kujitolea kwa ukweli, wanaonyesha uso uliojeruhiwa na wenye matumaini wa Kanisa. Kupambania kwako haki pia ni vita vya Kanisa. Imani ambayo haigusi majeraha ya mwili na roho ya mwanadamu bado haijaelewa Injili,” aliandika. Kwa wale ambao wamevumilia, hata walipopuuzwa, kudharauliwa, au kushambuliwa kisheria, Papa alikumbuka Waraka kwa Watu wa Mungu wa 2018 wa Papa Francisko, ulioandikwa baada ya ziara yake ngumu nchini Chile na mikutano na waathirika wa unyanyasaji: "Uchungu wa waathiriwa na familia zao ni uchungu wetu pia, na ni muhimu kwamba tufanye upya ahadi yetu ya kulinda watoto na watu wazima walio hatarini." Papa Leo XIV alikazia kwamba mageuzi ya kweli ya kikanisa si maneno matupu bali ni njia thabiti ya unyenyekevu, ukweli, na malipizi: “Kinga na utunzaji si mbinu za kichungaji tu—ndio kiini cha Injili.”
Kwa Paola Ugaz mwenyewe, kwa ushujaa wake wa kumwendea Papa Francisko mnamo tarehe 10 Novemba 2022, na kujitetea yeye mwenyewe na wanahabari wenzake Pedro Salinas, Daniel Yovera, na Patricia Lachira, ambao walifichua dhuluma za kikundi cha kidini kinachofanya kazi katika nchi nyingi lakini zinazotokea Peru. Papa pia alikubali madhara makubwa yaliyosababishiwa na Sodalitium, ikiwa ni pamoja na matumizi mabaya ya fedha yanayoathiri jumuiya nzima kama vile Catacaos na Castilla.
Akirejea tena matamshi yake kwa wataaluma wa habari tarehe 12 Mei 2025, Papa Leo XIV, alisisitiza kwamba hii haikuwa salamu rasmi tu, bali ni uthibitisho wa jukumu takatifu la uandishi wa habari: “Ukweli si wa mtu yeyote, ni wajibu wa kila mtu kuutafuta, kuuhifadhi, na kuutumikia,” alisema. Kupitia ujumbe wake wa maandishi, uliosomwa katika ukumbi wa michezo wa kuigiza, Papa anashiriki wasiwasi na matumaini yake kwa watu wa Peru. "Katika wakati huu wa mivutano mikubwa ya kitaasisi na kijamii, kutetea uandishi wa habari huru na wenye maadili si tu kitendo cha haki, bali ni wajibu kwa wote wanaotamani demokrasia imara na shirikishi." Alitoa wito kwa mamlaka ya Peru, mashirika ya kiraia, na kila raia kuwalinda wale wanaoripoti ukweli kwa uadilifu, kutoka kwa vituo vya radio vya jamii hadi vyombo vya habari vya kawaida, kutoka maeneo ya vijijini hadi mji mkuu. "Popote mwandishi wa habari anaponyamazishwa, roho ya kidemokrasia ya nchi inadhoofika," aliandika. Papa Leo XIV alihitimisha kwa ujumbe mzito kwa wawasilianaji wote wa Peru, "Msiogope. Kupitia kazi yenu, mnaweza kuwa wajenzi wa amani, umoja na mazungumzo ya kijamii. Iweni wapandaji wa nuru katika vivuli," na alielezea matumaini yake kwa Kanisa kwamba hakuna mtu anayepaswa kuteseka kimya kimya na ambapo ukweli hauogopi, bali kukumbatiwa kama njia ya ukombozi.