Mkutano wa Papa na Rais Milei wa Argentina
Vatican News
Jumamosi tarehe 7 Juni 2025, Baba Mtakatifu Leo XIV amekutana katika Jumba la Kitume mjini Vatican na Rais wa Jamhuri ya Argentina, Bwana Javier Gerardo Milei. Kwa mujibu wa taarifa kutoka Vyombo vya Habari vya Vatican imeripoti kwamba, mkuu wa nchi ya Argentina mara tu baada ya mkutano huo na Baba Mtakatifu, pia alikutana na Kardinali Pietro Parolin, Katibu Mkuu wa Vatican akiambatana na Monsinyo Miros?aw Wachowski, Katibu Msaidizi wa Mahusiano, Ushirikiano na Mataifa na Mashirika ya Kimataifa.
"Wakati wa majadiliano ya kina katika Sekretarieti ya Vatican, kuthaminiana kwa mahusiano thabiti ya nchi mbili na nia ya kuyaimarisha zaidi kulithibitishwa,” kwa mujibu wa Ofisi ya Habari ya Vatican. Kisha majadiliano yalilenga katika “masuala ya maslahi ya pamoja, ikiwa ni pamoja na mwelekeo wa kijamii na kiuchumi, mapambano dhidi ya umaskini na kujitolea kwa mafungamano ya kijamii.”.
Na tena, “baadhi ya masuala ya kijamii na kisiasa ya kikanda na kimataifa yalishughulikiwa ikiwa ni pamoja na umakini maalum kwa migogoro inayoendelea, wakionesha umuhimu wa dhamira ya haraka ya kuunga mkono amani."