Mazungumzo ya simu kati ya Papa Leo XIV na Vladimir Putin
Angella Rwezaula, -Vatican
Alasiri hii tarehe 4 Juni 2025 "kulikuwa na mazungumzo ya simu kati ya Papa Leo XIV na Rais Putin." Hayo yalithibitishwa jioni na msemaji Mkuu wa Vyombo vya Habari vya Vatican, Dk. Matteo Bruni. “Wakati wa simu, pamoja na masuala ya kupendezwa na pande zote, uangalifu hasa ulitolewa kwa hali ya Ukraine na amani. Papa alitoa wito kwa Urusi kufanya ishara inayopendelea amani, alisisitiza umuhimu wa mazungumzo kwa ajili ya utambuzi wa mawasiliano mazuri kati ya pande hizo mbili na kutafuta suluhu la mzozo huo.” Pia walizungumza “juu ya hali ya kibinadamu, hitaji la kupendelea misaada inapobidi, juhudi zinazoendelea za kubadilishana wafungwa na thamani ya kazi ambayo Kardinali Matteo Zuppi Rais wa CEI anafanya kwa maana hii.”
Kwa kuhitimisha Dk Bruni alisema: “Papa Leo, alimrejea Patriaki Kirill, akimshukuru kwa matashi mema aliyopokea mwanzoni mwa upapa wake na akasisitiza jinsi tunu za kawaida za Kikristo zinavyoweza kuwa nuru inayosaidia kutafuta amani, kutetea uhai na kutafuta uhuru wa kweli wa kidini.”Hata hivyo Papa pia alikuwa na mazungumzo ya simu na Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky siku chache baada ya kuchaguliwa na alikutana naye wakati wa Misa ya mwanzo wa Upapa wake, tarehe 18 Mei. Papa Leo XIV alizindua miito mbalimbali kwa ajili ya amani katika Ukraine.
Tufanye kila liwalo kupata amani Ukraine
Katika Sala ya Malkia wa Mbingu kunako tarehe 11 Mei 2025, Papa alisema: “Ninabeba moyoni mwangu mateso ya watu wapendwa wa Ukraine. Hebu tufanye kila linalowezekana ili kufikia amani ya kweli, ya haki na ya kudumu haraka iwezekanavyo. Wafungwa wote waachiliwe na watoto waweze kurejea kwa familia zao.” Tarehe 16 Mei 2025, katika hotuba yake kwa Baraza la Wanadiplomasia lililoidhinishwa na Vatican, Papa Leo XIV alieleza matumaini ya “ulimwengu ambao kila mtu anaweza kutambua ubinadamu wake katika ukweli, haki na amani. Natumaini kwamba hii inaweza kutokea katika mazingira yote, kuanzia na yale yaliyojaribiwa zaidi kama Ukraine na Nchi Takatifu.
Miito mipya
Katika Sala ya Malkia wa Mbingu kunako tarehe 18 Mei 2025, Papa Leo XIV alibanisha kwamba "Ukraine inayoteswa hatimaye inangojea mazungumzo ya amani ya haki na ya kudumu." Katika hadhira ya jumla ya Mei 28, alisisitiza kwamba mawazo yake "mara nyingi huenda kwa watu wa Ukraine, waliopigwa na mashambulizi mapya, makubwa dhidi ya raia na miundombinu," akihakikishia ukaribu wake na sala zake kwa wahasiriwa wote, hasa watoto na familia: "Ninasisitiza upya wito wa kusitisha vita na kuunga mkono kila mpango wa mazungumzo na amani. Ninaomba kila mtu ajiunge kwa sababu ya vita vya amani huko Ukraine.”