Maadhimisho ya Jubilei ya Kiti Kitakatifu: Utakatifu wa Maisha
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Waamini wanahimizwa kufanya hija ya maisha ya kiroho pamoja na Bikira Maria, aliyethubutu kumfuasa Mwanaye mpendwa Kristo Yesu katika Njia ya Msalaba, ili kuambata huruma na upendo wake usiokuwa na kifani. Maria ni Bikira na Mama kwa sababu yeye ni ishara na utimilifu kamili wa Kanisa. Kanisa kwa kupokea Neno la Mungu kiaminifu linakuwa pia ni Mama na Mwalimu kwani kwa mahubiri na ubatizo linazaa watoto waliotungwa na Roho Mtakatifu na kuzaliwa na Mwenyezi Mungu kwa uzima mpya usiokufa. Hayati Baba Mtakatifu Francisko, kunako mwaka 2018 alitangaza rasmi maadhimisho ya Kumbukumbu ya Bikira Maria Mama wa Kanisa, ambayo inaadhimishwa, Jumatatu baada ya Sherehe ya Pentekoste na kwa mwaka huu ni tarehe 9 Juni 2025. Maadhimisho ya Mwaka huu, yanabeba uzito wa pekee kwani ni sehemu pia ya maadhimisho ya Jubilei ya Vatican: “Kiti kitakatifu” “Holy See.”
Maadhimisho haya yameanza kwa wafanyakazi wa Vatican kushiriki katika Ibada ya Maungamo, tafakari iliyoongozwa na Sr. Maria Gloria Riva, wa Shirika la Watawa Wanaoabudu Daima Ekaristi Takatifu, tafakari ambayo imehudhuriwa pia na Baba Mtakatifu Leo XIV, ambaye baadaye ameongoza Maandamano ya wanahija kuelekea Mlango Mtakatifu wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, huku akiwa amebeba Msalaba na hatimaye, akaongoza pia Ibada ya Misa Takatifu. Itakumbukwa kwamba, Jubilei ya Mwaka 2025 ya Ukristo inanogeshwa na kauli mbiu “Peregrinantes in spem” yaani: “Mahujaji wa Matumaini.” Baba Mtakatifu Leo XIV katika mahubiri yake amekazia kuhusu: Furaha ya kuadhimisha kumbukumbu ya Bikira Maria Mama wa Kanisa, chemchemi ya mwanga wa Roho Mtakatifu uliowashukia waamini wakati wa Maadhimisho ya Sherehe ya Pentekoste, kielelezo cha Fumbo la Kanisa linalo shuhudiwa na Mitume wa Yesu waliokuwa wakidumu kwa moyo mmoja katika kusali, pamoja nao, wanawake, na Mariamu Mama yake Yesu, na ndugu zake. Rej. Mdo 1:12,14.
Na kama Mwinjili Yohane anavyosimulia, jinsi ambavyo Bikira Maria alivyokuwa amesimama chini ya Msalaba, Kristo Yesu akamkabidhi Mama yake kwa mwanafunzi wake aliyempenda, yaani Yohane, kisha akainama kichwa, akaisalimu roho yake. Rej. Yn 19-25-34. Baba Mtakatifu Leo XIV anasema, Mtakatifu Yohane ndiye peke yake kati ya Mitume kumi na wawili, aliyethubutu kusimama pale Mlimani Kalvari, akashuhudia Kristo Yesu akimkabidhi Mama yake, ambaye sasa ni Eva mpya na huo ndio mwendelezo wa Umama wa Bikira Maria kwa njia ya Roho Mtakatifu, mwaliko na changamoto ya wafuasi wa Kristo Yesu, kumwilisha upendo huu katika uhalisia wa maisha yao. Umama wa Kanisa na wa Kiti Kitakatifu unategemea kwa kiasi kikubwa Msalaba wa Kristo Yesu, ambao unafananishwa na mbegu ndogo ya haradali unaweza kukua na kuwa mti mkubwa. Katika maadhimisho ya Kumbukumbu ya Bikira Maria Mama wa Kanisa, kuna uwiano na uhusiano mkubwa kati ya Uzao wa Bikira Maria na ule wa Kanisa unaofumbatwa katika utakatifu wa maisha unaosimikwa katika Kiti Kitakatifu na kama alivyo Mama Kanisa. Kiti kitakatifu kinahifadhi na kutunza utakatifu unaomwilishwa katika maisha ya wafanyakazi wake.
Kumbe, njia bora zaidi ya kutekeleza huduma kwenye Kiti kitakatifu “Holy See” ni kujibidiisha kuwa Mtakatifu, kila mmoja kadiri ya wito, dhamana na utume aliokabidhiwa na Mama Kanisa. Kwa Mapadre wanaweza kuwa ni watakatifu kwa kuubeba Msalaba wao kila siku, kwa kutekeleza majukumu yao kwa upendo na imani na hivyo kushiriki kikamilifu katika kuchangia utakatifu wa Kiti kitakatifu. Hivi ndivyo ilivyo pia kwa Baba au Mama wa familia anayevulimia shida, mahangaiko na matatizo ya familia yake; kwa kuwa na mtoto ambaye kwa hakika ni changamoto kubwa kwa malezi na makuzi yake; Mzazi mgonjwa, lakini wanaendelea kutekeleza dhamana na wajibu wao kwa moyo wa upendo na imani kubwa, hata wao wanachangia katika uzao wa Bikira Maria na wa Mama Kanisa.
Baba Mtakatifu Leo XIV anasema, Mwinjili Luka katika Kitabu chake cha Matendo ya Mitume, anawaonesha Mitume wa Yesu wakiwa na Bikira Maria pamoja na ndugu zake, chumba cha juu, huko walikuwa wakidumu kwa moyo mmoja katika kusali. Sehemu hii ya Maandiko Matakatifu inaonesha Umama wa Bikira Maria katika Kanisa la mwanzo, lililokuwa linazaliwa, hali ambayo imebaki katika nyakati na mahali na kwamba, haya ni matunda ya Fumbo la Pasaka, zawadi makini kutoka kwa Kristo Yesu, aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu. Roho Mtakatifu aliyewashukia Mitume kwa nguvu siku ile ya Pentekoste ya kwanza ni Roho Mtakatifu yule yule ambaye Kristo Yesu aliwapatia Mitume wake, pale alipoinama kichwa, akasalimu roho yake. Rej. Yn 19:30. Kumbe, Umama wa Kanisa daima unaunganishwa na Neema inayobubujika kutoka katika Moyo Mtakatifu wa Yesu, uliotobolewa kwa mkuki, na humo ikatoka Damu na Maji, alama za Sakramenti za Kanisa.
Baba Mtakatifu Leo XIV anasema, Bikira Maria kwa neema na utume aliokabidhiwa chini ya Msalaba na huduma kwa Kanisa la Mwanzo ni kumbukumbu hai ya Kristo Yesu anayewavuta waja wake kushiriki kikamilifu katika mchakato wa ujenzi wa amani na utulivu katika tofauti zao msingi na kwamba, wanaunganika kwa pamoja katika sala. Bikira Maria aliendelea kumuenzi Mtakatifu Petro katika maisha na utume wake na hivi ndivyo Mama Kanisa anavyoendelea kuwaenzi Makhalifa wa Mtakatifu Petro katika maisha na utume wao na kwamba, Kiti kitakatifu kinashikiliwa na hizi nguzo mbili yaani nguzo ya Bikira Maria pamoja na nguzo ya Mtakatifu Petro. Nguzo ya Bikira Maria inahakikisha uzao na utakatifu wa maisha na nguzo ya Mtakatifu Petro katika uzao wake inawahakikishia zawadi ya Kristo Yesu na ya Roho Mtakatifu. Baba Mtakatifu Leo XIV anawaalika watu wa Mungu kumsifu na kumtukuza Mwenyezi Mungu kwa Neno lake, ambalo ni taa inayoongoza mapito yao, maisha na huduma yao kwa Kiti kitakatifu na amehitimisha mahubiri yake kwa sala ifuatayo: “Ee Baba upende kulijalia Kanisa lako, likungwa mkono na upendo wa Kristo Yesu, liweze kuzaa matunda zaidi katika Roho, lifurahie utakatifu wa watoto wake na kukusanya familia nzima ya binadamu kifuani mwake.”