杏MAP导航

Tafuta

Mama Kanisa anawaalika waamini na watu wote wenye mapenzi mema kukimbilia ulinzi na tunza ya Bikira Maria, Mama wa Kanisa. Mama Kanisa anawaalika waamini na watu wote wenye mapenzi mema kukimbilia ulinzi na tunza ya Bikira Maria, Mama wa Kanisa.  (@Vatican Media)

Kumbukumbu ya Bikira Maria Mama wa Kanisa 9 Juni 2025: Jubilei Ya Vatican

Hayati Papa Francisko, kunako mwaka 2018 alitangaza rasmi maadhimisho ya Kumbukumbu ya Bikira Maria Mama wa Kanisa, ambayo inayoadhimishwa, Jumatatu baada ya Sherehe ya Pentekoste na kwa mwaka huu ni tarehe 9 Juni 2025. Maadhimisho ya Mwaka huu, yanabeba uzito kwani ni sehemu pia ya maadhimisho ya Jubilei ya Vatican: “Holy See” na Ibada ya Misa Takatifu inaongozwa na Baba Mtakatifu Leo XIV kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Mama Kanisa anawaalika waamini na watu wote wenye mapenzi mema kukimbilia ulinzi na tunza ya Bikira Maria, Mama wa Kanisa. Awe ni faraja na matumaini kwa wagonjwa, maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Waamini wanahimizwa kufanya hija ya maisha ya kiroho pamoja na Bikira Maria, aliyethubutu kumfuasa Kristo Yesu katika Njia ya Msalaba, ili kuambata huruma na upendo wake usiokuwa na kifani. Maria ni Bikira na Mama kwa sababu yeye ni ishara na utimilifu kamili wa Kanisa. Kanisa kwa kupokea Neno la Mungu kiaminifu linakuwa pia ni Mama na Mwalimu kwani kwa mahubiri na ubatizo linazaa watoto waliotungwa na Roho Mtakatifu na kuzaliwa na Mungu kwa uzima mpya usiokufa. Hayati Baba Mtakatifu Francisko, kunako mwaka 2018 alitangaza rasmi maadhimisho ya Kumbukumbu ya Bikira Maria Mama wa Kanisa, ambayo inaadhimishwa, Jumatatu baada ya Sherehe ya Pentekoste na kwa mwaka huu ni tarehe 9 Juni 2025. Maadhimisho ya Mwaka huu, yanabeba uzito wa pekee kwani ni sehemu pia ya maadhimisho ya Jubilei ya Vatican: “Holy See” na Ibada ya Misa Takatifu inaongozwa na Baba Mtakatifu Leo XIV kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican kuanzia saa 5:30 Asubuhi kwa Saa za Ulaya sawa na Saa 6:30 Mchana kwa Saa za Afrika Mashariki na Kati. Itakumbukwa kwamba, Jubilei ya Mwaka 2025 ya Ukristo inanogeshwa na kauli mbiu “Peregrinantes in spem” yaani: “Mahujaji wa Matumaini” baada ya dhoruba ya maambukizi makubwa ya Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19 pamoja na patashika nguo kuchanika kutokana na vita inayoendelea kupiganwa vipande vipande sehemu mbalimbali za dunia.

Kumbukumbu ya Bikira Maria Mama wa Kanisa
Kumbukumbu ya Bikira Maria Mama wa Kanisa   (@Vatican Media)

Jubilei hii ni muda muafaka wa kupyaisha imani, matumaini na mapendo thabiti, kwa kuishi kama ndugu wamoja, sanjari na kusikiliza pamoja na kujibu kilio cha Dunia Mama na Kilio cha Maskini. Ni muda wa toba na wongofu wa ndani na wa kiikolojia, tayari kusimama kidete kulinda na kutunza mazingira nyumba ya wote. Ni muda muafaka kwa waamini kujikita katika kutangaza na kushuhudia imani na matumaini yanayomwilishwa katika huduma ya upendo kwa Mungu na jirani; kwa kukazia umoja na utofauti wa wateule watakatifu wa Mungu. Jubilei ni muda uliokubalika na Mwenyezi Mungu wa kuhakikisha kwamba, waamini wanajitahidi kumwilisha karama na mapaji yao kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Lengo ni kutangaza na kushuhudia imani na furaha ya Injili kwa watu wa Mataifa. Ibada hii kwa Bikira Maria, inalenga kuwasaidia waamini kukumbuka kwamba, maisha ya Kikristo yanafumbatwa katika Fumbo la Msalaba linaloadhimishwa katika Ekaristi Takatifu, Kanisa linapomtolea pia sifa na heshima Bikira Maria, Mama wa Mkombozi, aliyesadaka maisha yake kwa ajili ya kushiriki kikamilifu katika kazi ya ukombozi!

Jubilei ya Vatican: "Holy See"
Jubilei ya Vatican: "Holy See"   (@Vatican Media)

Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican katika Tamko lao kuhusu Fumbo la Kanisa wanafafanua kwa kina na mapana nafasi ya Bikira Maria, Mama wa Mungu katika Fumbo la Kristo na la Kanisa: tangu Agano la Kale, Fumbo la Umwilisho, Bikira Maria katika maisha ya hadharani ya Kristo Yesu, Bikira Maria baada ya Kristo Yesu kupaa mbinguni. Wanaendelea kufafanua dhamana na nafasi ya Bikira Maria katika maisha na utume wa Kanisa kama mshiriki mwaminifu wa kazi ya ukombozi, mwombezi kwa ajili ya wokovu. Bikira Maria ni mfano wa utimilifu wa Kanisa katika maisha na utakatifu wake na kwamba, Bikira Maria ni ishara na matumaini thabiti na faraja kwa taifa la Mungu linalosafiri huku bondeni kwenye machozi! Kwa hakika, Mapokeo ya maadhimisho ya Fumbo la maisha ya Kristo ambayo kamwe hayawezi kumtenga Bikira Maria, Mama wa Kristo na Kanisa. Bikira Maria anatambulikana kuwa ni Mama wa Wakristo ambao wamezaliwa kwake kwa njia ya fadhila ya upendo na kwamba, Bikira Maria ni Mama wa Fumbo la Mwili wa Kristo, yaani Kanisa kama wanavyofundisha Mtakatifu Agostino, Askofu na Mwalimu wa Kanisa pamoja na Mtakatifu Leo Mkuu. Umama wa Kristo na Kanisa ulidhihirishwa pale chini ya Msalaba, Bikira Maria alipopokea upendo wa dhati kutoka kwa Mwanaye mpendwa na Yohane kwa niaba ya wengine wote, wakawa ni wafuasi na Mitume wa upendo kwa ajili ya Mama yake.

Kumbukumbu ya Bikira Maria Mama wa Kanisa & Jubilei ya Vatican
Kumbukumbu ya Bikira Maria Mama wa Kanisa & Jubilei ya Vatican   (@Vatican Media)

Bikira Maria aliendelea kuandamana na Kanisa katika sala wakati Mitume wakisubiria ujio wa Roho Mtakatifu. Kwa nyakati mbali mbali, waamini wamekuwa wakimheshimu na kumfanyia Ibada Bikira Maria kama: Mama wa Mitume, Mama wa waamini wa wale wote wanaozaliwa upya katika Kristo Yesu na Mama wa Kanisa kama wanavyofundisha Papa Benedikto XV pamoja na Papa Leo wa XIII. Mtakatifu Paulo VI kunako tarehe 21 Novemba 1964, Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican walipokuwa wanahitimisha Kikao cha tatu cha Mkutano huo, alitamka kwamba, Bikira Maria ni Mama wa Kanisa; yaani: ni Mama wa Wakristo wote na wachungaji wanaomkimbilia kama Mama. Kumbe, Bikira Maria, Mama wa Kanisa anapaswa kuheshimiwa na Wakristo wote. Katika maadhimisho ya Mwaka wa Upatanisho1975, kuliadhimishwa Ibada ya Misa Takatifu kwa ajili ya Bikira Maria, Mama wa Kanisa. Litania ya Bikira Maria wa Loreto ikaongeza heshima hii katika Litania. Majimbo mbalimbali yakaona kwamba, inafaa na kuomba Kiti Kitakatifu kuruhusu maadhimisho haya yaingizwe katika Kalenda ya majimbo yao! Kutokana na kukua na hatimaye, kukomaa kwa Ibada ya Bikira Maria, Mama wa Kanisa, Hayati Baba Mtakatifu Francisko akaridhia tamko lililotolewa na Baraza la Kipapa la Ibada, Nidhamu na Sakramenti na Sakramenti za Kanisa kwamba, kuanzia sasa Kumbukumbu ya Bikira Maria Mama wa Kanisa itakuwa inaadhimishwa Jumatatu baada ya Sherehe ya Pentekoste ya kila mwaka!

Bikira Maria Mama wa Kanisa
07 Juni 2025, 16:15