Hotuba ya Papa Leo XIV Kwa Mahujaji Kutoka Ukraine: Changamoto
Na Sarah Pelaji, -Vatican.
Baba Mtakatifu Leo XIV Jumamosi tarehe 28 Juni 2025 ametoa hotuba yake kwa mahujaji wa Kanisa Katoliki la Kigriki la Ukraine waliofika kwenye kaburi la Mtume Petro kama Mahujaji wa Matumaini katika maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 2025 ya Ukristo. “Awali ya yote ninamsalimu kwa heshima kubwa Mhashamu Sviatoslav Shevchuk, Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki Kyiv-Haly?, Maaskofu wote, mapadre, watawa na waamini walei. Hija yenu ni ishara ya hamu ya kufufua imani yenu ili kuimarisha mshikamano na ushirika na Askofu wa Roma, na ya kushuhudia tumaini lisilodanganya, kwa sababu linatokana na upendo wa Kristo uliomiminwa mioyoni mwetu na Roho Mtakatifu (rej. Rum 5:5). Mwaka huu wa Jubilei unatuita kuwa mahujaji wa tumaini hilo katika maisha yetu yote, licha ya matatizo ya nyakati hizi. Safari yenu hadi Roma, kupita katika Milango Mitakatifu na kutembelea makaburi ya Mitume na Wafiadini ni alama ya safari hii ya kila siku, inayolenga uzima wa milele, ambako Bwana atafuta kila chozi, wala hakutakuwa na kifo tena, wala maombolezo, wala kilio, wala uchungu (rej. Ufu 21:4).
Wengi wenu mliondoka kutoka nchi yenu nzuri, tajiri kwa imani ya Kikristo, iliyotunzwa na ushuhuda wa Injili wa watakatifu wengi na kunyweshwa damu ya wafiadini wengi, ambao kwa karne nyingi walithibitisha uaminifu wao kwa Mtume Petro na waandamizi wake kwa kujitoa maisha yao. Ndugu wapendwa, imani ni hazina ya kushirikishwa. Hata hivyo Kila zama huleta ugumu, uchovu na changamoto, lakini pia fursa za kukua katika kujiamini na kujisalimisha kwa Mungu,” amesema Papa Leo XIV huku akikiri kuwa, kwa sasa imani yao inapitia jaribu kubwa tangu kuanza kwa vita, uvamizi wa kijeshi dhidi ya Ukraine. Papa Leo XIV anasema bila shaka wengi wao wamekuwa wakijiuliza: Bwana, kwa nini haya yote? Uko wapi? Tunapaswa kufanya nini ili kuokoa familia zetu, nyumba zetu, na taifa letu? Haimaanishi kuwa na majibu yote tayari, bali kumtumainia Mungu kuwa yuko nasi na hutupatia neema yake, kwa kuwa Yeye ndiye atakayetoa neno la mwisho na maisha yatashinda mauti.
Baba Mtakatifu Leo XIV amewaweka chini ya ulinzi na tunza ya Bikira Maria, anayependwa sana na watu wa Ukraine ambaye kwa ‘ndiyo’ yake ya unyenyekevu na ujasirii, alifungua mlango wa ukombozi wa dunia, hivyo hata sasa anatuhakikishia kuwa hata “ndiyo” yetu ya leo, inayotamkwa wa imani ya kweli, inaweza kuwa chombo mikononi mwa Mungu kwa ajili ya kuleta jambo kubwa. Wakiwa wamethibitishwa katika imani na Mrithi wa Mtakatifu Petro, Papa Leo XIV anawahimiza kuishirikisha imani hiyo na wapendwa wao na watu wa Taifa na wote watakaokutana nao kwa mapenzi ya Mungu. Kusema “ndiyo” leo kunaweza kufungua upeo mpya wa imani, matumaini na amani hasa kwa wale walio katika mateso.
“Ndugu zangu wapendwa, ninapowapokea hapa, nataka kueleza ukaribu wangu na Ukraine inayoteseka hasa: watoto, vijana, wazee na familia zinazolia na kuomboleza kwa sababu ya kupoteza wapendwa wao. Nahisi maumivu yenu kwa ajili ya wafungwa na waathirika wa vita hivi visivyo na maana. Ninamkabidhi Bwana Yesu, nia zenu, jitihada zenu, mateso ya kila siku na zaidi ya yote tamaa zenu za amani na utulivu. Napenda kuwatia moyo kuendelea kutembea pamoja, wachungaji na waamini, mkimtazama Kristo Yesu ambaye ndiye wokovu wetu. Bikira Maria awaongoze na kuwalinda, yeye ambaye kwa kushiriki kwake mateso ya Mwanawe ni Mama wa Tumaini. Nawabariki kwa moyo wote, familia zenu, Kanisa lenu na watu wenu,” Papa Leo XIV alihitimisha hotuba yake.