Hotuba ya Papa Leo XIV Kwa Mapadre, Mashemasi na Majandokasisi wa Roma
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Baba Mtakatifu Leo XIV, Alhamisi tarehe 12 Juni 2025 amekutana na kuzungumza na Mapadre, Mashemasi wanaohudumia Jimbo kuu la Roma pamoja na Majandokasisi wa Jimbo kuu la Roma; amewashukuru kwa sadaka na majitoleo yao kwa ajili ya huduma kwa watu wa Mungu Jimbo kuu la Roma. Hii ni huduma inayosimikwa katika kimya kikuu na wakati mwingine, inasheheni matizo na magumu ya maisha au hata kutoeleweka. Jambo la msingi kwa Mapadre na Mashemasi hawa kukumbuka ni kwamba, wao wanathamani kubwa sana mbele ya Mungu sanjari na utekelezaji wa mpango wake. Mkutano huu ni sehemu ya mbinu mkakati wa kufahamiana kwa karibu zaidi ili waweze kutembea kwa pamoja. Jimbo kuu la Roma ni kielelezo cha upendo na umoja na kwamba, Baba Mtakatifu Leo XIV anaweza kutekeleza dhamana na wajibu wake kikamilifu kutokana na uwepo wao, huku wakiwa wameshikamana katika kifungo cha neema na Askofu wao pamoja na uwajibikaji wa watu wote wa Mungu. Jimbo kuu la Roma ni la aina yake kwani linapokea na kuwahifadhi Mapadre kutoka sehemu mbalimbali za dunia kwa ajili ya masomo, lakini pia wanashiriki katika shughuli za kichungaji maparokiani, kielelezo cha ukatoliki wa Kanisa unaosimikwa katika ukarimu. Baba Mtakatifu Leo XIV katika hotuba yake, amekazia mambo makuu mawili: Umoja na Ushirika mambo msingi yanayofumbatwa katika ile Sala ya Kikuhani, ambayo Kristo Yesu alisali, huku akimwomba Baba yake wa mbinguni ili wanafunzi wake wote wawe na umoja. Mapadre wawe ni mifano bora ya kuigwa na watu wanaoaminika.
“Kama wewe, Baba, ulivyo ndani yangu, nami ndani yako; hao nao wawe ndani yetu; ili ulimwengu upate kusadiki ya kwamba wewe ndiwe uliyenituma. Nami utukufu ule ulionipa nimewapa wao; ili wawe na umoja kama sisi tulivyo umoja. Mimi ndani yao, nawe ndani yangu, ili wawe wamekamilika katika umoja; ili ulimwengu ujue ya kuwa ndiwe uliyenituma, ukawapenda wao kama ulivyonipenda mimi.” Yn 17:21-23. Ni kwa njia ya umoja na mshikamano, wataweza kuzaa matunda na hivyo kutoa ushuhuda wenye mvuto na mashiko. Umoja na mshikamano huu, kwa Mapadre wa Roma unasimikwa katika hali ya kuishi kwa pamoja katika nyumba za Mapadre, Vyuo pamoja na makazi mengi ya Mapadre. Padre anaitwa na kuhamasishwa na Mama Kanisa kuwa ni chombo cha ushirika, unaorutubisha maisha na utume wake, kinyume kabisa cha utamaduni wa kuishi pweke unaowafanya baadhi ya Mapadre kujisikia, kujiona na kujitafuta zaidi, mambo yanayohatarisha maisha ya kiroho na hivyo kudhohofisha nguvu za utume wao kama Mapadre. Baba Mtakatifu Leo XIV amekazia sana umuhimu wa ujenzi wa ushirika na udugu wa kibinadamu kati yap Makleri na hivyo kuwa waangalifu ili wasikumbane na vikwazo vinavyoweza kutoka ndani mwao. Makleri wakuze na kudumisha mahusiano na mafungamano kati yao, hasa wakati wanapohisi kuchoka, wanaposhindwa kueleweka au hata kutokana na sababu mbalimbali. Baba Mtakatifu Leo XIV anasema, anataka kuwasaidia, ili waweze kutembea kwa pamoja, ili waweze kupata amani na utulivu wa ndani katika maisha na utume wao na kwamba, kutokana na changamoto mamboleo, anapenda kuwahamasisha Mapadre wa Jimbo kuu la Roma kujenga udugu wa kipadre unaofumbatwa katika amana na utajiri wa maisha ya kiroho; unaowawezesha kukutana na Kristo Yesu katika Sakramenti zake sanjari na kusikiliza, kutafakari na kumwilisha Neno la Mungu katika maisha na vipaumbele vyao. Kwa njia hii, Makleri wataweza kupendana kidugu, kuheshimiana kwa kuwatanguliza jirani zao, Rej. Rum 12:10 lengo likiwa ni kuboresha mahusiano ya Kikanisa.
Ushirika anasema Baba Mtakatifu Leo XIV unapaswa kumwilishwa katika dhamana na maisha ya Jimbo kuu la Roma, kwa kutambua uwepo wa karama mbalimbali, malezi na majiundo tofauti, lakini wote wakishirikishwa nguvu moja. Mkazo wa pekee utolewe katika sera na mikakati ya shughuli za kichungaji kwa Kanisa mahalia na ule wa Kanisa la Kiulimwengu. Watembee kwa pamoja, huku wakionesha uaminifu kwa Injili ya Kristo Yesu; katika amani na utulivu, huku kila mmoja, akijitahidi kutumia karama na mapaji yake katika ujenzi wa Fumbo la Mwili wa Kristo yaani Kanisa na Kristo Yesu mwenyewe ndiye kichwa cha Mwili huu. Baba Mtakatifu Leo XIV amekazia umuhimu wa Mapadre kuwa ni mfano bora wa kuigwa, kwa kusimika maisha yao katika ukweli na uwazi kama alivyosema Mtakatifu Paulo alipokuwa anaagana na wazee wa Efeso: “Ninyi wenyewe mnajua tangu siku ya kwanza nilipokanyaga hapa Asia, jinsi nilivyokuwa kwenu wakati wote, nikimtumikia Bwana kwa unyenyekevu wote, na kwa machozi, na majaribu yaliyonipata kwa hila za Wayahudi; ya kuwa sikujiepusha katika kuwatangazia neno lo lote liwezalo kuwafaa bali naliwafundisha waziwazi, na nyumba kwa nyumba, nikiwashuhudia Wayahudi na Wayunani wamtubie Mungu, na kumwamini Bwana wetu Yesu Kristo.” Mdo 20: 18-20.
Baba Mtakatifu Leo XIV kama Baba na Mchungaji mkuu, anawataka Mapadre wa Jimbo kuu la Roma kujizatiti zaidi kuwa ni Mapadre wa mfano na wanaoaminika, kwa kutambua utajiri wa karama na mapaji yao kama wanavyojulikana mbele ya Mwenyezi Mungu kuwa kweli ni Mitume na Wahudumu wa Habari Njema ya Wokovu, changamoto na mwaliko wa kuwa ni waaminifu na watakatifu, kwa kuendelea kujikita katika unyenyekevu na upatanisho tunu msingi za maisha ya Kikristo, upendo ukipewa kipaumbele cha kwanza. Fadhila ya unyenyekevu ni kikolezo na nguvu ya upyaisho wa maisha ya kiroho ya watu watakatifu wa Mungu. Baba Mtakatifu Leo XIV anawataka Makleri wa Jimbo kuu la Roma kuwa makini na changamoto mamboleo, ufunguo makini wa Unabii. Inasikitisha kuona: vita, mauaji ya watu wasiokuwa na hatia, ukosefu wa usawa, njaa, umaskini na vita, mambo yanayosigina utu, heshima na haki msingi za binadamu. Kuna mateso na mahangaiko yanayoendelea kuwakumbuka hata wananchi wanaoishi Roma. Kuna umaskini mkubwa wa hali na mali; ukosefu wa makazi ya watu pamoja na uzuri unaoendelea kutoweka kama alivyowahi kusema Baba Mtakatifu Francisko. Mji ambao una uhai una ukarimu pia kwa wote. Baba Mtakatifu Leo XIV anawaalika Makleri wa Jimbo kuu la Roma, kupokea changamoto zilizoko mbele yao na kama sehemu ya ushuhuda na shule ya ujenzi wa Ufalme wa Mungu, kwa kufuata mfano wa watakatifu waliothubutu kumwilisha tunu msingi za Injili za Injili katika historia na maisha yao.
Hawa ni akina Don Primo Mazzolari na Don Lorenzo Milani, Manabii wa haki na amani. Jimbo kuu la Roma, linayo mifano ya Mapadre kama Luigi Di Liegro aliyejipambanua katika mapambano dhidi ya umaskini wa hali na kipato, wakajisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya kutafuta na kudumisha haki, ustawi na maendeleo ya binadamu. Mapadre hawa ni mifano bora ya kuigwa na mbefu ya utakatifu wa maisha kwa mji wa Roma. Mwishoni mwa hotuba yake, Baba Mtakatifu Leo XIV amependa kuwahakikishia Makleri wa Jimbo kuu la Roma, ukaribu na uwepo wake, huku akiwaaminisha kwa Kristo Yesu, na kumwomba awasaidie kukuza na kuimarisha umoja na ushirika; wawe mifano bora ya kuigwa na waendelee kujikita katika ushuhuda wa kinabii, ili kuhudumia nyakati zao. Amewataka kulipenda, kubaki ndani ya Kanisa na kuwa ni sehemu ya Kanisa. Waendelee kumpenda Kristo Yesu Mchungaji mwena, Mchumba wake mwaminifu na asiyedanganya kamwe wala hapendi mtu yeyote apoteee. Baba Mtakatifu amewataka Makleri wa Jimbo kuu la Roma, kuendelea kusali na kuwaombea hata wale Kondoo waliopotea, ili wao pia warejee, watambue na kujisikia kuwa kwenye zizi moja na chini ya mchungaji mmoja.
Kwa upande wake, Kardinali Baldassare Reina, maarufu kama “Baldo”, Makamu Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Roma, katika hotuba yake ya kumkaribisha Baba Mtakatifu Leo XIV ili aweze kuzungumza na Makleri na Majandokasisi wa Jimbo kuu la Roma amesema kwamba, Jimbo kuu la Roma lina jumla ya Mapadre 809, Mashemasi wa Kudumu ni 149; Mapadre wanaotoka Majimbo mengine, lakini wako Roma kwa ajili ya Masomo ni 500. Mapadre wanaoishi kwenye Vyuo na Taasisi mbalimbali za Kikanisa ni 2, 347; Mashirika ya Kipadre ni 211; Watawa Mapadre 3, 914 na jumla yao ni 8020, hawa ni Mapadre na Mashemasi. Kuna Mapadre 579 wanaofanya utume wao Jimbo kuu la Roma, 132 ni Wamisionari na Mapadre 50 wameomba kupumzika na kutafakari kuhusu maisha na wito wao. Jimbo kuu la Roma lina Parokia 333. Kuna mapadre wagonjwa na wazee 50. Kuna Majandokasisi wa Jimbo kuu la Roma 84. Kimsingi Mapadre wanaishi kwa pamoja, huku wakisaidiana katika shughuli mbalimbali za kichungaji. Licha ya changamoto na matatizo mbalimbali lakini Makleri wa Jimbo kuu la Roma, wako tayari kusonga mbele kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya Kanisa la Kristo. Changamoto kubwa ni kutokana na tofauti za kitamaduni, mahali wanapotoka Mapadre hawa; malezi na majiundo tofauti; changamoto za shughuli za kichungaji, ambayo wakati mwingine inakuwa ni vigumu kuweza kutoa taswira ya pamoja. Makleri wa Jimbo kuu la Roma wametumia fursa hii, kurudia tena ahadi zao za utii kwa Khalifa wa Mtakatifu Petro, ambaye kwa sasa yuko katika nafsi ya Baba Mtakatifu Leo XIV, ili Jimbo kuu la Roma liweze kuendelea kuwa ni zuri na takatifu.