Carlo Acutis na Pier Giorgio Frassati Kutangazwa Watakatifu 7 Septemba 2025
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Baba Mtakatifu Leo XIV, Ijumaa tarehe 13 Juni 2025 ameongoza Masifu kabla ya adhuhuri kwa Baraza la Makardinali, kwa ajili ya kuwapigia kura wenye heri wanaotarajiwa kutangazwa kuwa ni Watakatifu. Kati yao ni: Askofu mkuu Ignazio Choukrallah Maloyan, Shahidi; Peter To Rot, Shahidi; Mwamini mlei na Katekista; Sr. Vincenza Maria Poloni, Mwanzilishi wa Shirika la Masista wa Huruma wa Verona (Misericordia); Sr. Maria del Monte Carmelo Rendiles Martínez, Muasisi wa Shirika la Watawa Wahudumu wa Yesu; Sr Maria Troncatti, Mtawa wa Shirika Masista Wasalesian wa Mtakatifu Yohane Bosco: “Salesian Sisters; au Daughters of Mary Help of Christians, F.M.A.” Wengine ni José Gregorio Hernández Cisneros, Mwamini mlei; Pier Giorgio Frassati, Mwamini Mlei, Utawa wa Tatu wa Mtakatifu Dominiko na hatimaye ni Bartolo Longo, Mwamini mlei.
Baba Mtakatifu Leo XIV ametangaza kwamba Mwenyeheri Pier Giorgio Frassati, Mwamini Mlei, Utawa wa Tatu wa Mtakatifu Dominiko pamoja na Mwenyeheri Carlo Acutis, Mwamini mlei waandikwe kwenye Kitabu cha Orodha ya Watakatifu Dominika tarehe 7 Septemba 2025. Wenyeheri wengine: Askofu mkuu Ignazio Choukrallah Maloyan, Peter To Rot, Sr. Vincenza Maria Poloni, Sr. Maria del Monte Carmelo Rendiles Martínez, José Gregorio Hernández Cisneros, pamoja na Bartolo Longo, Mwamini mlei waandikwe kwenye Kitabu cha Orodha ya Watakatifu wa Kanisa Dominika tarehe 19 Oktoba 2025 wakati wa maadhimisho ya Siku ya Kimisionari Ulimwenguni. Hawa ni mashuhuda wa matumaini.