杏MAP导航

Tafuta

Kardinali Giovanni Battista Re, Dekano wa Baraza la Makardinali, Jumatano tarehe 7 Mei 2025 ameongoza Ibada ya Misa Takatifu kwa ajili ya Uchaguzi wa Khalifa wa Mtakatifu Petro. Kardinali Giovanni Battista Re, Dekano wa Baraza la Makardinali, Jumatano tarehe 7 Mei 2025 ameongoza Ibada ya Misa Takatifu kwa ajili ya Uchaguzi wa Khalifa wa Mtakatifu Petro.  (@Vatican Media)

Uchaguzi wa Khalifa wa Mtakatifu Petro 2025: Mungu, Yesu, Kanisa Na Walimwengu

Amekazia: imani, matumaini na mapendo, ili kuomba nguvu za Roho Mtakatifu, kama ilivyokuwa wakati ule wa Sherehe ya Pentekoste ya kwanza, kwa Makardinali kutoa kipaumbele cha kwanza kwa Mwenyezi Mungu, Kristo Yesu, Ustawi, maendeleo na mafao ya Kanisa na binadamu katika ujumla wake, tayari kusadaka maisha yao kwa ajili ya Kristo Yesu na Kanisa lake. Rej. Yn 15:12. Huu ni wakati wa kutangaza na kushuhudia utamaduni wa upendo na mshikamano wa dhati.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baraza la Makardinali, katika mkutano wake wa tano, Jumatatu tarehe 28 Aprili 2025 liliamua kwamba, mchakato wa uchaguzi wa Khalifa wa Mtakatifu Petro uanze rasmi Jumatano tarehe 7 Mei 2025. Kuna jumla ya Makardinali 135 wenye haki ya kupiga na kupigiwa kura, lakini wanaoshiriki ni 133. Kuna Makardinali kutoka katika nchi 15 ambao wanashiriki kwa mara ya kwanza katika uchaguzi wa Khalifa wa Mtakatifu Petro. Kadiri ya Katiba ya Kitume ya “Universi Dominici Gregis” iliyotungwa na Mtakatifu Yohane Paulo II kunako tarehe 22 Februari 1996, Idadi ya Makardinali wanaopaswa kupiga au kupigiwa kura ni 120, lakini, idadi hii imekuwa ikizidi mara zote. Waamini wanaalikwa kufunga na kusali, ili kuwasindikiza Makardinali katika tukio hili lenye umuhimu wa pekee katika maisha na utume wa Kanisa. Kardinali Giovanni Battista Re, Dekano wa Baraza la Makardinali, Jumatano tarehe 7 Mei 2025 ameongoza Ibada ya Misa Takatifu kwa ajili ya Uchaguzi wa Khalifa wa Mtakatifu Petro: “Pro eligendo Romano Pontifice.” Katika mahubiri, mwanzo kabisa mwa mkutano wa kumchagua Khalifa wa Mtakatifu Petro “Conclave” amekazia: imani, matumaini na mapendo thabiti, ili kuomba nguvu za Roho Mtakatifu, kama ilivyokuwa wakati ule wa Sherehe ya Pentekoste ya kwanza, kwa Makardinali kutoa kipaumbele cha kwanza kwa Mwenyezi Mungu, Kristo Yesu, Ustawi, maendeleo na mafao ya Kanisa na binadamu katika ujumla wake, tayari kusadaka maisha yao kwa ajili ya Kristo Yesu na Kanisa lake. Rej. Yn 15:12. Huu ni wakati wa kutangaza na kushuhudia utamaduni wa upendo na mshikamano wa dhati, tayari kuleta mabadiliko makubwa katika maisha ya watu wa Mungu.

Ibada ya Misa Takatifu Kwa Ajili ya Uchaguzi wa Papa Mpya 2025
Ibada ya Misa Takatifu Kwa Ajili ya Uchaguzi wa Papa Mpya 2025   (@Vatican Media)

Mama Kanisa amesali na kuomba: Umoja na ushirika; Ujenzi wa udugu wa kibinadamu; Umoja kati ya Wakristo, Urika wa Maaskofu na Khalifa wa Mtakatifu Petro, ili kweli Kanisa liweze kuwa ni “nyumba na shule ya ushirika” kwa kuendelea kuwa aminifu kwa tunu msingi za Kiinjili. Makardinali wanakusanyika ili kumchagua Khalifa wa Mtakatifu Petro kama Kristo Yesu mwenyewe alivyosema: “Wewe ndiwe Petro na juu ya mwamba huu nitalijenga Kanisa langu” (Mt 16:18). Mamlaka na madaraka haya anayapokea kila Baba Mtakatifu, Khalifa wa Mtakatifu Petro anapochaguliwa kadiri ya Mapokeo ya Mama Kanisa. Huyu ni Mchungaji ambaye atampendeza Mungu kwa utakatifu na kuwafaidia waamini katika kuwachunga kwa bidii; kwa ajili ya ustawi, mafao na maendeleo ya Kanisa na binadamu katika ujumla wao. Kanisa linamhitaji Papa atakayeamsha dhamiri za watu wa Mungu: Kimaadili, kiroho na kijamii katika ulimwengu mamboleo ambao una maendeleo makubwa ya sayansi na teknolojia, lakini ni ulimwengu unaotaka kumweka Mwenyezi Mungu pembezoni mwa vipaumbele vyake. Walimwengu wanatarajia kuliona Kanisa likipyaisha tunu msingi za maisha ya kiroho na kiutu, kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafanikio ya kizazi cha sasa na kile kijacho.

Vipaumbele: Mungu, Yesu, Kanisa na Walimwengu
Vipaumbele: Mungu, Yesu, Kanisa na Walimwengu   (@Vatican Media)

Makardinali wako kwenye Kikanisa cha Sistina, tayari kuanza mkutano wa Uchaguzi wa Khalifa wa Mtakatifu Petro “Conclave” kwa kujifungia huko ndani kwa ufunguo.  Waamini wanaalikwa kufunga na kusali kwa ajili ya kuombea ufanisi katika uchaguzi wa Khalifa wa Mtakatifu Petro. Makardinali wanatambua dhamana na uzito wa tukio hili katika maisha na utume wa Kanisa. Katika kipindi cha miaka mia moja iliyopita, Roho Mtakatifu amelijalia Kanisa Mapapa wenye uwezo mkubwa na watakatifu. Waamini katika Sala ya Kuombea Uchaguzi wa Khalifa wa Mtakatifu Petro wamesali, ili kumwomba Mwenyezi Mungu alilinde Kanisa katika ukweli, umoja na amani; awajalie Makardinali Roho wa akili, shauri, heshima na mang’amuzi; haki, mshikamano na maridhiano. Mwenyezi Mungu awe ni faraja kwa watu wanaonyanyasika kutokana na chuki na vita pamoja na hali ya kukata tamaa; watoto wanaofyekelewa mbali kutokana na utamaduni wa kifo, waonje maisha na uzima wa milele. Wabatizwa wote wawe watii, wanyenyekevu, wajisadake na hatimaye, wajikite katika Injili ya upendo.  

Mchungaji anayempendeza Mungu kwa utakatifu wa maisha
Mchungaji anayempendeza Mungu kwa utakatifu wa maisha   (@Vatican Media)

Kama vile Mtakatifu Petro na wale Mitume walivyounganika, kwa agizo la Kristo Yesu, katika urika mmoja tu, kwa jinsi ilivyo sawa, Askofu mkuu wa Roma aliye Khalifa wa Mtakatifu Petro, na Maaskofu walio waandamizi wa Mitume, wanaungana pamoja. Askofu wa Kanisa la Roma, ambaye katika yeye linadumu jukumu lililokabidhiwa na Bwana kwa Petro tu, mkuu wa Mitume, linalotakiwa kurithishwa kwa waandamizi wake, ni mkuu wa urika wa Maaskofu, Wakili wa Kristo Yesu na Mchungaji mkuu wa Kanisa lote zima hapa duniani; hivyo kwa nguvu ya jukumu lake anayo mamlaka ya kawaida ya juu kabisa, kamili, inayojitegemea kwa uhuru. Rej. Kanuni 330-332. Baba Mtakatifu ajaye, lazima awe ni mtu anayeonesha uwepo na ukaribu wake kwa watu wa Mungu; awe ni daraja na mwongozo katika mchakato wa ujenzi wa umoja na ushirika kati ya watu wa Mungu. Ni kiongozi anayepaswa kuwa ni shuhuda wa imani, atakayesimama kidete kulinda na kutetea: haki, amani na utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote; tayari kuchochea tunu msingi za maisha ya ndoa na familia; miito mitakatifu ndani ya Kanisa; elimu, malezi na majiundo makini kwa vijana wa kizazi kipya. Waamini wamemwombea pia Hayati Baba Mtakatifu Francisko.

Kanisa lipyaishe tunu msingi za maisha ya kiroho, kiutu na kijamii
Kanisa lipyaishe tunu msingi za maisha ya kiroho, kiutu na kijamii   (@Vatican Media)

Mwenyezi Mungu katika Maandiko Matakatifu anasema: “Nitajiinulia kuhani mwaminifu atakayefanya sawasawa na mambo yote niliyo nayo katika moyo wangu, na katika nia yangu; nami nitamjengea nyumba iliyo imara; naye atakwenda mbele yangu siku zote.” 1Sam 2:35. Katika Kolekta Mama Kanisa anasali akisema, “Ee Mungu, uliye mchungaji wa milele, unaliongoza kundi lako kwa ulinzi wa daima.  Ulijalie Kanisa lako, kwa wema wako mkuu, mchungaji ambaye atakupendeza kwa utakatifu na kutufaidia sisi kwa kutuchunga kwa bidii.  Kwa njia ya Bwana wetu Yesu Kristo Mwanao, anayeishi na kutawala nawe katika umoja wa Roho Mtakatifu, Mungu, milele na milele.” Katika Sala ya kuombea dhabihu, Mama Kanisa anasali kwa kusema, “Ee Bwana, wingi wa rehema yako ushuke juu yetu, ili kwa sadaka takatifu tunayokutolea kwa heshima utujalie tufurahie kupata mchungaji atakayekupendeza wewe mtukufu katika kulisimamia Kanisa takatifu. Kwa njia ya Kristo Bwana wetu.” Mama Kanisa anamwomba Mwenyezi Mungu, ili aweze kulijalia Kanisa Mchungaji mkuu, atakayewafundisha kwa fadhila zake watu wa Taifa la Mungu, kwa kuwamiminia mioyoni mwao ukweli wa Kiinjili.

Umoja na Ushirika, Udugu wa Kibinadamu, Urika wa Maaskofu na Uaminifu
Umoja na Ushirika, Udugu wa Kibinadamu, Urika wa Maaskofu na Uaminifu   (@Vatican Media)

Baraza la Makardinali katika mikutano yake elekezi kama sehemu ya maandalizi ya uchaguzi wa Khalifa wa Mtakatifu Petro “Conclave” linawaalika watu wa Mungu, kukiishi kipindi hiki cha neema na utambuzi wa maisha ya kiroho sanjari na kusikiliza mapenzi ya Mungu. Makardinali wakitambua ukubwa na unyeti wa kazi na dhamana iliyoko mbele yao, wanatambua kwamba, kuna haja ya kuungwa mkono na kusindikizwa na sala za waamini. Hii ndiyo nguvu ya kweli ambayo inakuza ndani ya Kanisa umoja wa viungo vyote vya Fumbo la Mwili wa Kristo yaani Kanisa. Rej. 1Kor 12: 12. Baraza la Makardinali linatambua uzito wa kazi kubwa iliyoko mbele yao kwa wakati huu, kwanza kabisa Makardinali wenyewe wanapenda kujinyenyekesha, ili waweze kuwa ni vyombo vya hekima isiyokuwa na kikomo na kwa maongozi ya Baba yao wa milele na kwa unyenyekevu wa utendaji wa Roho Mtakatifu. Makardinali wanakaza kusema, kwa hakika Roho Mtakatifu ndiye Mhusika mkuu wa maisha ya watu wa Mungu, changamoto na mwaliko wa kumsikiliza na kuitikia kile ambacho anasema Roho Mtakatifu kwa Mama Kanisa. Rej. Ufu 3:6. Bikira Maria Mama wa Kanisa awasindikize kwa sala, kwa ulinzi na tunza yake ya Kimama. Kuanzia tarehe 7 Mei 2025 Saa 9:00 Alasiri kwa Saa za Ulaya sawa na Saa 10 Alasiri kwa Saa za Afrika Mashariki na Kati mawasiliano yote kwa njia ya simu na mitandao ya kijamii yatazimwa mjini Vatican, na yatarudishwa tena, wakati wa kumtangaza Khalifa wa Mtakatifu Petro wa 267, atakayeliongoza Kanisa baafa ya kifo cha Baba Mtakatifu Francisko kilichotokea Jumatatu ya Pasaka, tarehe 21 Aprili 2025.

Sala ya Kanisa
07 Mei 2025, 14:01