杏MAP导航

Tafuta

Kardinali Giovanni Battista Re, Dekano wa Baraza la Makardinali, Jumatano tarehe 7 Mei 2025 anaongoza Ibada ya Misa Takatifu kwa ajili ya Uchaguzi wa Khalifa wa Mtakatifu Petro: “Pro eligendo Romano Pontifice.” Kardinali Giovanni Battista Re, Dekano wa Baraza la Makardinali, Jumatano tarehe 7 Mei 2025 anaongoza Ibada ya Misa Takatifu kwa ajili ya Uchaguzi wa Khalifa wa Mtakatifu Petro: “Pro eligendo Romano Pontifice.”  

Uchaguzi wa Baba Mtakatifu wa 267 wa Kanisa Katoliki 2025

Makardinali 135 wenye haki ya kupiga na kupigiwa kura, lakini wanaoshiriki ni 133. Kuna Makardinali kutoka katika nchi 15 ambao wanashiriki kwa mara ya kwanza katika uchaguzi wa Papa. Muda wa kumaliza uchaguzi huu, bado unaendelea kubaki kitendawili. Kadiri ya Katiba ya Kitume ya “Universi Dominici Gregis” iliyotungwa na Yohane Paulo II kunako tarehe 22 Februari 1996, Idadi ya Makardinali wanaopaswa kupiga au kupigiwa kura ni 120, lakini, idadi hii imekuwa kubwa.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baraza la Makardinali, katika mkutano wake wa tano, Jumatatu tarehe 28 Aprili 2025 liliamua kwamba, mchakato wa uchaguzi wa Khalifa wa Mtakatifu Petro uanze rasmi Jumatano tarehe 7 Mei 2025. Kuna jumla ya Makardinali 135 wenye haki ya kupiga na kupigiwa kura, lakini wanaoshiriki ni 133. Kuna Makardinali kutoka katika nchi 15 ambao wanashiriki kwa mara ya kwanza katika uchaguzi wa Khalifa wa Mtakatifu Petro. Muda wa kumaliza uchaguzi huu, bado unaendelea kubaki kitendawili. Kadiri ya Katiba ya Kitume ya “Universi Dominici Gregis” iliyotungwa na Mtakatifu Yohane Paulo II kunako tarehe 22 Februari 1996, Idadi ya Makardinali wanaopaswa kupiga au kupigiwa kura ni 120, lakini, idadi hii imekuwa ikizidi mara zote. Waamini wanaalikwa kufunga na kusali, ili kuwasindikiza Makardinali katika tukio hili lenye umuhimu wa pekee katika maisha na utume wa Kanisa.

Baaddhi ya Maafisa wakila kiapo kabla ya uchaguzi wa Papa 2025
Baaddhi ya Maafisa wakila kiapo kabla ya uchaguzi wa Papa 2025

Kardinali Giovanni Battista Re, Dekano wa Baraza la Makardinali, Jumatano tarehe 7 Mei 2025 anaongoza Ibada ya Misa Takatifu kwa ajili ya Uchaguzi wa Khalifa wa Mtakatifu Petro: “Pro eligendo Romano Pontifice.” Ibada hii ya Misa Takatifu inaanza majira ya Saa 4:00 Asubuhi kwa Saa za Ulaya, sawa na Saa 5:00 kwa Saa za Afrika Mashariki na Kati. Jumatano jioni, majira ya Saa 10: 30 za Jioni kwa Saa za Ulaya sawa na Saa 11:30 kwa Saa za Afrika Mashariki na Kati, Makardinali wataanza kuingia kwenye Kikanisa cha Sistina, tayari kuanza mkutano wa Uchaguzi wa Khalifa wa Mtakatifu Petro “Conclave” kwa kujifungia huko ndani kwa ufunguo.  Waamini wanaalikwa kufunga na kusali kwa ajili ya kuombea ufanisi katika uchaguzi wa Khalifa wa Mtakatifu Petro.

Waamini wanaalikwa kusali na kufunga kwa ajili ya kuombea uchaguzi wa Papa
Waamini wanaalikwa kusali na kufunga kwa ajili ya kuombea uchaguzi wa Papa   (@Vatican Media)

Kama vile Mtakatifu Petro na wale Mitume walivyounganika, kwa agizo la Kristo Yesu, katika urika mmoja tu, kwa jinsi ilivyo sawa, Askofu mkuu wa Roma aliye Khalifa wa Mtakatifu Petro, na Maaskofu walio waandamizi wa Mitume, wanaungana pamoja. Askofu wa Kanisa la Roma, ambaye katika yeye linadumu jukumu lililokabidhiwa na Bwana kwa Petro tu, mkuu wa Mitume, linalotakiwa kurithishwa kwa waandamizi wake, ni mkuu wa urika wa Maaskofu, Wakili wa Kristo Yesu na Mchungaji mkuu wa Kanisa lote zima hapa duniani; hivyo kwa nguvu ya jukumu lake anayo mamlaka ya kawaida ya juu kabisa, kamili, inayojitegemea kwa uhuru. Rej. Kanuni 330-332. Baba Mtakatifu ajaye, lazima awe ni mtu anayeonesha uwepo na ukaribu wake kwa watu wa Mungu; awe ni daraja na mwongozo katika mchakato wa ujenzi wa umoja na ushirika kati ya watu wa Mungu. Ni kiongozi anayepaswa kuwa ni shuhuda wa imani, atakayesimama kidete kulinda na kutetea: haki, amani na utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote; tayari kuchochea tunu msingi za maisha ya ndoa na familia; miito mitakatifu ndani ya Kanisa; elimu, malezi na majiundo makini kwa vijana wa kizazi kipya.

Ibadaya Misa takatifu kwa ajili ya kuombea uchaguzi wa Papa
Ibadaya Misa takatifu kwa ajili ya kuombea uchaguzi wa Papa   (@Vatican Media)

Mwenyezi Mungu anasema: “Nitajiinulia kuhani mwaminifu atakayefanya sawasawa na mambo yote niliyo nayo katika moyo wangu, na katika nia yangu; nami nitamjengea nyumba iliyo imara; naye atakwenda mbele yangu siku zote.” Katika Kolekta Mama Kanisa anasali akisema, “Ee Mungu, uliye mchungaji wa milele, unaliongoza kundi lako kwa ulinzi wa daima.  Ulijalie Kanisa lako, kwa wema wako mkuu, mchungaji ambaye atakupendeza kwa utakatifu na kutufaidia sisi kwa kutuchunga kwa bidii.  Kwa njia ya Bwana wetu Yesu Kristo Mwanao, anayeishi na kutawala nawe katika umoja wa Roho Mtakatifu, Mungu, milele na milele.” Katika Sala ya kuombea dhabihu, Mama Kanisa anasali kwa kusema, “Ee Bwana, wingi wa rehema yako ushuke juu yetu, ili kwa sadaka takatifu tunayokutolea kwa heshima utujalie tufurahie kupata mchungaji atakayekupendeza wewe mtukufu katika kulisimamia Kanisa takatifu. Kwa njia ya Kristo Bwana wetu.” Mama Kanisa anamwomba Mwenyezi Mungu, ili aweze kulijalia Kanisa Mchungaji mkuu, atakayewafundisha kwa fadhila zake watu wa Taifa la Mungu, kwa kuwamiminia mioyoni mwao ukweli wa Kiinjili.

Makardinali wanaoshiriki uchaguzi wa Papa ni 133
Makardinali wanaoshiriki uchaguzi wa Papa ni 133

Baraza la Makardinali katika mikutano yake elekezi kama sehemu ya maandalizi ya uchaguzi wa Khalifa wa Mtakatifu Petro “Conclave” linawaalika watu wa Mungu, kukiishi kipindi hiki cha neema na utambuzi wa maisha ya kiroho sanjari na kusikiliza mapenzi ya Mungu. Makardinali wakitambua ukubwa na unyeti wa kazi na dhamana iliyoko mbele yao, wanatambua kwamba, kuna haja ya kuungwa mkono na kusindikizwa na sala za waamini. Hii ndiyo nguvu ya kweli ambayo inakuza ndani ya Kanisa umoja wa viungo vyote vya Fumbo la Mwili wa Kristo yaani Kanisa. Rej. 1Kor 12: 12. Baraza la Makardinali linatambua uzito wa kazi kubwa iliyoko mbele yao kwa wakati huu, kwanza kabisa Makardinali wenyewe wanapenda kujinyenyekesha, ili waweze kuwa ni vyombo vya hekima isiyokuwa na kikomo na kwa maongozi ya Baba yao wa milele na kwa unyenyekevu wa utendaji wa Roho Mtakatifu. Makardinali wanakaza kusema, kwa hakika Roho Mtakatifu ndiye Mhusika mkuu wa maisha ya watu wa Mungu, changamoto na mwaliko wa kumsikiliza na kuitikia kile ambacho anasema Roho Mtakatifu kwa Mama Kanisa. Rej. Ufu 3:6. Bikira Maria Mama wa Kanisa awasindikize kwa sala, kwa ulinzi na tunza yake ya Kimama. Kuanzia tarehe 7 Mei 2025 Saa 9:00 Alasiri kwa Saa za Ulaya sawa na Saa 10 Alasiri kwa Saa za Afrika Mashariki na Kati mawasiliano yote kwa njia ya simu na mitandao ya kijamii yatazimwa mjini Vatican, na yatarudishwa tena, wakati wa kumtangaza Khalifa wa Mtakatifu Petro wa 267, atakayeliongoza Kanisa baafa ya kifo cha Baba Mtakatifu Francisko kilichotokea Jumatatu ya Pasaka, tarehe 21 Aprili 2025.

Uchaguzi wa Papa

 

 

 

06 Mei 2025, 13:54