Ratiba ya maadhimisho ya Misa za Papa Leo XIV kwa mwezi Juni 2025
Vatican News
Jubilei, sherehe, mkutano wa kawaida wa makardinali na mengine zaidi. Ndiyo ambayo Mshehereheshaji wa Maadhimisho ya Liturujia za Kipapa, Askofu Mkuu Diego Ravelli, alitangaza tarehe 21 Mei 2025, katika Ratiba za kiliturujia zitakazoongozwa na Baba Mtakatifu Leo XIV kwa mwezi Juni. Papa Leo XIV ataadhimisha Misa yake ya kwanza katika Dominika, tarehe 1 Juni 2025, saa 4:30 asubuhi, majira ya Ulaya katika Uwanja wa Mtakatifu Petro, kwa ajili ya Maadhimisho ya Jubilei ya Familia, Watoto, Mababu na Wazee. Ni mahali ambapo pia Papa ataadhimisha Misa Dominika itakayofuata, tarehe 8 Juni 2025 katika maadhimisho ya Pentekoste.
Liturujia hiyo itaona ushiriki wa waamini ambao watakuwa Roma kwa ajili ya Jubilei ya Harakati, Vyama na Jumuiya mpya itakayofanyika tarehe 7 na 8 Juni 2025. Tarehe 9 Juni 2025, ni kumbu kumbu ya Bikira Maria, Mama wa Kanisa, ambapo Papa ataongoza misa takatifu katika Kanisa Kuu la Mtakatifu Petro, saa 5.30 asubuhi kwa ajili ya Jubilei ya Makao Matakatifu ya Vatican.
Mkutano wa Makardinali kwa ajili ya kuwatangaza watakatifu
Ijumaa tarehe 13 Juni 2025, saa 3.00 kamili asubuhi masaa ya Ulaya, katika ukumbi wa mikutano ya uchaguzi Papa Leo XIV ataitisha Mkutano wa kawaida wa umma kwa ajili ya kura ya baadhi wa kutangazwa watakatifu. Kisha, Dominika tarehe 15 Juni saa 4:30 majira ya Ulaya kwenye Uwanja wa Mtakatifu Petro, kutakuwa na maadhimisho ya Utatu Mtakatifu, ambapo Baba Mtakatifu ataadhimisha Ibada ya Misa Takatifu kwa ushiriki wa wanahija wa Jubilei ya Michezo
Dominika tarehe 22 Juni 2025 siku ambayo Mama Kanisa anaadhimisha siku kuu ya Mwili na Damu Takatifu ya Yesu Kristo, Papa Leo XIV atahamia katika Kanisa Kuu la Mtakatifu Yohane wa Laterano ambako, saa 11.00 jioni masaa ya Ulaya, ataongoza Ibada ya Misa na kufuatiwa na maandamano ya kuelekea Kanisa kuu la Mtakatifu Maria Mkuu ambako hatimaye, atatoa baraka.
Misa yenye baraka ya pallium tarehe 29 Juni
Papa atarejea kwenye Uwanja wa Mtakatifu Petro siku ya Ijumaa, tarehe 27 Juni 2025, kwa ajili ya Maadhimisho ya Moyo Mtakatifu wa Yesu ambapo saa 3.00 kamili asubuhi masaa ya Ulaya kwa ajili ya Ibada ya Misa Takatifu ambayo pia inaadhimisha Jubilei ya Mapadre.
Hatimaye, Dominika tarehe 29 Juni 2025, siku ambayo Mama Kanisa anaadhimisha Ukulu wa Watakatifu Petro na Paulo, Baba Mtakatifu Leo XIV ataongoza Ibada ya Misa Takatifu katika Kanisa Kuu la Mtakatifu Petro saa 3:30 asubuhi majira ya Ualya na pia kubariki Pallium kwa Maaskofu wakuu wapya wa makanisa makuu duniani.