Papa Leo XIV:Yesu ni Neno,yeye ndiye Mbegu na ili izae lazima ife
Na Angella Rwezaula – Vatican.
Katika mzunguko wa Katekesi ya Papa kuhusu Jubilei 2025: Yesu Kristo tumaini letu; Maisha ya Yesu.Baba Mtakatifu Leo XIV ameendeleza sehemu ya sita ya mpanzi. Yesu alizungumza na kwa misemo mingi (Mt 13,3a). Mara baada ya Somo la Injili kutoka Mt 13, 1-9) Papa Leo XIV, Jumatano tarehe 21 Mei 2025 akiwageukia waamini na mahujaji zaidi ya 40,000 waliokusanyika katika Uwanja wa Mtakatifu Petro mjini Vatican alisema: “Ndugu wapendwa, ninayofuraha ya kuwakaribisha katika Katekesi yangu ya kwanza. Tunaendelenza mzunguko wa Katekesi ya kijubilei kuhusu mada ya “Yesu Kristo Tumaini letu, iliyoanzishwa na Papa Francisko. Leo tuendelea kutafakari mifano ya Yesu, ambayo hutusaidia kugundua tena tumaini, kwa sababu inatuonesha jinsi Mungu anavyofanya kazi katika historia. Leo ningependa kuzingatia mfano fulani, kwa sababu ni aina ya utangulizi wa mifano yote. Ninarejeea ile ya mpanzi ( Mt 13:1-17). Kwa namna fulani, katika historia hii tunaweza kutambua njia ya Yesu ya kuwasiliana, ambayo ina mengi ya kutufundisha kwa ajili ya kutangaza Injili leo.
Kila mfano unasimulia historia ambayo imechukuliwa kutoka katika maisha ya kila siku, lakini inataka kutuambia kitu zaidi, inatuelekeza kwa maana ya ndani zaidi. Mfano huo unazua maswali ndani yetu, unatualika tusiishie kwenye mwonekano wa kijuu juu. Mbele ya historia inayosimuliwa au picha niliyopewa, ninaweza kujiuliza: niko wapi katika historia hii? Je, picha hii inasema nini katika maisha yangu? Neno fumbo linatokana na kitenzi cha Kigiriki paraballein, ambacho kinamaanisha kutupa mbele. Mfano huo unanitupia neno linaloniudhi na kunisukuma kujiuliza. Mfano wa mpanzi unazungumza kwa usahihi kabisa juu ya mienendo ya neno la Mungu na athari zake. Kwa hakika, kila neno la Injili ni kama mbegu iliyotupwa katika udongo wa maisha yetu. Mara nyingi Yesu anatumia mfano wa mbegu, na maana tofauti.
Katika sura ya 13 ya Injili ya Mathayo, mfano wa mpanzi unatanguliza mfululizo wa mifano mingine midogo, ambayo baadhi yake huzungumza kwa usahihi juu ya kile kinachotokea katika udongo: ngano na magugu, mbegu ya haradali, hazina iliyofichwa shambani. Kwa hivyo udongo huu ni nini? Ni moyo wetu, lakini pia ni ulimwengu, jumuiya, Kanisa. Neno la Mungu, kiukweli, hutia mbolea na kuchochea kila ukweli. Hapo mwanzo, tunamwona Yesu akiondoka nyumbani na umati mkubwa unakusanyika kumzunguka(Mt 13:1). Neno lake linavutia na kufurahisha. Ni wazi kuna hali nyingi tofauti kati ya watu. Neno la Yesu ni kwa kila mtu, lakini linafanya kazi kwa kila mmoja kwa njia tofauti. Muktadha huu unatuwezesha kuelewa vyema maana ya mfano huo. Mpanzi, asili kabisa, anakwenda kupanda, lakini hana wasiwasi juu ya mahali ambapo mbegu itaanguka. Anapanda mbegu hata mahali ambapo haziwezekani kuzaa matunda: barabarani, kati ya miamba, kati ya miiba. Mtazamo huu huwashangaza wale wanaosikiliza na kuwaongoza kuuliza: kwa nini?
Tumezoea kuhesabu vitu, na wakati mwingine ni muhimu, lakini hii haitumiki kwa upendo! Njia ambayo mpanzi huyu “mpotevu” atupavyo mbegu ni mfano wa jinsi Mungu anavyotupenda. Ni kweli kwamba hatima ya mbegu pia inategemea jinsi udongo unavyoikaribisha na hali inayopatikana ndani yake, lakini kabla ya yote mfano huu Yesu anatuambia kwamba Mungu hutupa mbegu ya neno lake juu ya kila aina ya udongo, yaani, katika hali zetu zozote, wakati mwingine sisi ni wa juu juu zaidi na wa kukengeushwa, wakati mwingine tunachukuliwa na shauku, wakati mwingine tunakandamizwa na wasiwasi wa maisha, lakini pia kuna nyakati ambazo tunapatikana na kukaribisha. Mungu ana uhakika na anatumaini kwamba punde au baadaye mbegu hiyo itasitawi.
Anatupenda hivi: hatungojei tuwe udongo bora, yeye hutupa neno lake kila wakati. Labda kwa kuona kwamba anatuamini, tamaa ya kuwa udongo bora itazaliwa ndani yetu. Haya ni matumaini, yanayosimikwa juu ya mwamba wa ukarimu na huruma ya Mungu. Kwa kutaja njia ambayo mbegu hiyo huzaa matunda, Yesu anazungumza pia kuhusu maisha yake. Yesu ni Neno, yeye ndiye Mbegu. Na mbegu, ili izae matunda, lazima ife. Kwa hiyo, mfano huu unatuambia kwamba Mungu yuko tayari “kupoteza” kwa ajili yetu na kwamba Yesu yuko tayari kufa ili kubadilisha maisha yetu. Papa Leo XIV aidha amebainisha kuwa: “Ninakumbuka mchoro huo mzuri wa Van Gogh: The Sower at Sunset.” Picha hiyo ya mpanzi chini ya jua kali pia inazungumza nami juu ya taabu ya mkulima. Na inanishangaza kwamba, nyuma ya mpanzi, Van Gogh amewakilisha ngano iliyokomaa tayari.
Inaonekana kwangu kuwa picha ya matumaini: kwa njia moja au nyingine, mbegu imezaa matunda. Hatujui jinsi gani hasa, lakini ndivyo ilivyo. Katikati ya tukio hilo, hata hivyo, hakuna mpanzi, ambaye yuko kandoni, lakini mchoro mzima unatawaliwa na picha ya jua, labda kutukumbusha kwamba ni Mungu anayesongesha historia, hata ikiwa nyakati fulani anaonekana hayupo au yuko mbali. Ni jua ambalo hupasha joto madongoa ya ardhi na kufanya mbegu kukomaa. Wapendwa kaka na dada, ni katika hali gani ya maisha neno la Mungu linatufikia leo? Tumwombe Bwana neema ya kukaribisha daima mbegu hii ambayo ni neno lake. Na tukitambua kwamba sisi si udongo wenye rutuba, tusikate tamaa, bali tumwombe atufanyie kazi zaidi ili tuwe udongo bora.”