杏MAP导航

Tafuta

2025: Maadhimisho ya kumbukizi ya Miaka 70 tangu kuanzishwa kwa CELAM, Miaka 40 ya Maadhimisho ya Mkutano mkuu wa CELAM, 2025: Maadhimisho ya kumbukizi ya Miaka 70 tangu kuanzishwa kwa CELAM, Miaka 40 ya Maadhimisho ya Mkutano mkuu wa CELAM,  

Papa Leo XIV Ujumbe Kwa CELAM Kumbukizi Miaka 70 Ya Uhai Wake

Kumbukizi ya Miaka 70 tangu kuanzishwa kwa CELAM, Miaka 40 ya Maadhimisho ya Mkutano mkuu wa CELAM, Miaka 10 tangu Hayati Papa Francisko achapishe Waraka wa Kitume wa “Laudato si” yaani “Sifa iwe kwako” juu ya utunzaji wa nyumba ya wote”, Jubilei ya Mwaka 2025 ya Ukristo sanjari na Mwelekeo wa Kanisa mintarafu Mkutano wa Kimataifa wa Mabadiliko ya Hali ya Hewa COP30 utakaofanyika huko Belèm, Eneo la Amazon, nchini Brazil, Mwezi Novemba 2025.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Amerika ya Kusini na Caribbean CELAM, ni matokeo ya mkutano mkuu wa Maaskofu wa Amerika ya Kusini, waliokutana kuanzia tarehe 25 Julai hadi tarehe 4 Agosti mwaka 1955 huko Rio de Janeiro, Brazil na Katiba yake ikapitishwa na Papa Pio XII tarehe 2 Novemba 1955. Mkutano huu, pamoja na mambo mengine ulipania kujenga na kuimarisha urika wa Maaskofu Katoliki Amerika ya Kusini, katika mchakato wa mang’amuzi ya shughuli za kichungaji, tayari kusikiliza na kujibu changamoto mamboleo katika maisha na utume wa Kanisa. Hii ni changamoto ya kujenga na kudumisha Kanisa la Kisinodi na Kimisionari, tayari kujikita katika kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu hadi miisho ya dunia.

Kumbukizi ya Miaka 70 ya CELAM: Urika wa Maaskofu Amerika ya Kusini
Kumbukizi ya Miaka 70 ya CELAM: Urika wa Maaskofu Amerika ya Kusini

Ni katika muktadha huu, wa maadhimisho ya kumbukizi ya Miaka 70 tangu kuanzishwa kwa CELAM, Miaka 40 ya Maadhimisho ya Mkutano mkuu wa CELAM, Kumbukizi ya Miaka 10 tangu Hayati Baba Mtakatifu Francisko achapishe Waraka wa Kitume wa “Laudato si” yaani “Sifa iwe kwako” juu ya utunzaji wa nyumba ya wote”, Maadhimisho ya Jubilei ya Mwaka 2025 ya Ukristo sanjari na Mwelekeo wa Kanisa mintarafu Mkutano wa Kimataifa wa Mabadiliko ya Hali ya Hewa COP30 utakaofanyika huko Belèm, Eneo la Amazon, nchini Brazil, Mwezi Novemba 2025, CELAM kuanzia tarehe 27 hadi 30 Mei 2025 Wajumbe wake wanakusanyika huko huko Rio de Janeiro, Brazil. Baba Mtakatifu Leo XIV ametumia fursa hii, kuwatumia ujumbe kwa kuendelea kukazia umuhimu wa kujenga na kudumisha urika wa Maaskofu, kusoma alama za nyakati kwa kutambua changamoto zinazolikabili Kanisa katika Ulimwengu mamboleo; Kutafuta majibu makini yatakayosaidia kuleta ufanisi katika utatuzi wa changamoto za kimaadili na utu wema.

Ujenzi wa Kanisa la Kimisionari na Kisinodi kwa kutemba pamoja
Ujenzi wa Kanisa la Kimisionari na Kisinodi kwa kutemba pamoja

Kwa hakika anasema Baba Mtakatifu Leo XIV kwamba Mkutano huu ni alama ya umoja na ushirika wa Maaskofu wa Amerika ya Kusini na Caribbean, katika mchakato wa uinjilishaji wa kina unaogusa mahitaji ya mtu mzima: kiroho na kimwili sanjari na utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote. Huu ni mkutano unaochambua pamoja na mambo mengine: umaskini unaosigina utu, heshima na haki msingi za mamilioni ya watu wa Mungu huko Amerika ya Kusini. Lakini, watu wa Mungu Amerika ya Kusini, hawana budi kukumbuka kwamba, Kristo Mfufuka, yuko kati yao, analilinda na kuliongoza Kanisa na kwamba, “na tumaini halitahayarishi; kwa maana pendo la Mungu limekwisha kumiminwa katika mioyo yetu na Roho Mtakatifu tuliyepewa sisi.” Rum 5:5. Baba Mtakatifu Leo XIV anawapongeza Maaskofu wa CELAM kwa kuendelea kupyaisha utume na shughuli za kimisionari zinazofanyika Barani humo. Anawasihi Maaskofu waendelee kuwa waaminifu katika huduma na upendo kwa Kanisa, hasa katika ulimwengu wa utandawazi na maendeleo makubwa ya sayansi na teknolojia. Hatimaye, Baba Mtakatifu Leo XIV amewaweka wajumbe wa Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Amerika ya Kusini na Caribbean CELAM, chini ya ulinzi na tunza ya Bikira Maria wa Guadalupe, Mlinzi na Msimamizi wa Amerika ya Kusini.

CELAM Miaka 70

 

29 Mei 2025, 14:14