Papa Leo XIV:Shukrani kwa Papa Francisko,Salamu maalum kwa Kanisa la Roma
Na Angella Rwezaula – Vatican.
Kardinali Shemasi Dominique Mamberti, ametangaza jina la Papa wa 267 aliyechaguliwa saa 12:07 jioni kwenye kura ya nne wakati wa Mkutano Mkuu wa 76 uliokuwa na watu wengi zaidi wa Kanisa lote la Ulimwengu, yaani Makardinali wapiga kura 133 waliokusanyika tangu tarehe 7 Mei alasiri katika Mkutano Mkuu kwenye Kikanisa cha Sistine.“ Amani iwe kwenu, “ Haya ndiyo yalikuwa ni maneno ya kwanza ya Kardinali Robert Francis Prevost, hadi wakati huo ambaye amechaguliwa kuwa Papa wa 267 katika historia ya Kanisa, na Papa wa kwanza wa Marekani.
“Ndugu wapendwa, hii ni salamu ya kwanza ya Kristo Mfufuka, Mchungaji Mwema aliyetoa maisha yake kwa ajili ya kundi la Mungu,” alisema Papa Leo XIV, jina lililochaguliwa na huyo wa Shirika la Mtakatifu Agostino kuwa Papa wa Kanisa Katoliki. "Nami pia ningependa salamu hii ya amani iingie mioyoni mwenu, iwafikie familia zenu, watu wote, popote walipo, watu wote na kila nchi iliyo na alama ya vita," aliendelea Baba Mtakatifu mpya: "Amani iwe nanyi! Hii ndiyo amani ya Kristo, amani iliyonyimwa kwa silaha na amani ambayo inahitaji, unyenyekevu na kudumu. Inatoka kwa Mungu, ambaye anatupenda sisi sote bila masharti."
"Bado tunaweka mioyoni mwetu sauti hiyo dhaifu lakini ya ujasiri ya Papa Francisko, ambaye aliibariki Roma," alikumbuka mtangulizi wake Papa Leo XIV kwamba: "Papa aliyebariki Roma na kutoa baraka zake kwa ulimwengu wote, asubuhi ile ya Pasaka. Niruhusu nifuatilie baraka hiyo hiyo: Mungu anatupenda, Mungu anawapenda ninyi nyote na uovu hautashinda! Sote tuko mikononi mwa Mungu. Kwa hivyo, katika mikononi mwake tunamwachia Mungu kama wanafunzi wa Kristo. Kristo anatutangulia. Ulimwengu unahitaji nuru yake, ubinadamu unamhitaji kama daraja la kufikiwa na Mungu na upendo wake. Pia tusaidiane kujenga madaraja, kwa mazungumzo, kwa kukutana, kutuunganisha sote kuwa watu wamoja, kwa amani daima."
Papa Leo XIV hata hivyo alijitambulisha kwamba: "Mimi ni mtoto wa Mtakatifu Agostino. 'Pamoja nanyi mimi ni Mkristo na kwa ajili yenu mimi askofu” ikiwa ni, rejeo la wasifu wake: "Kwa maana hii sote tunaweza kutembea pamoja, kuelekea nchi hiyo ambayo Mungu ametuandalia." Papa Leo XIV alisisitiza tena kwamba “Salamu za pekee kwa Kanisa la Roma”, papa mpya alisema, hayo huku akishangiliwa na nderemo.
Wasifu wake
Kardinali Robert Francis Prevost alizaliwa tarehe 14 Septemba 1955 huko Chicago (Illinois, Marekani). Mnamo mwaka wa 1977 alijiunga na Shirika la Mtakatifu Augostino, katika jimbo la Mama Yetu wa Shauri jema huko Mtakatifu Louis. Mnamo tarehe 29 Agosti 1981 alifunga nadhiri za daima. Alisoma katika Taalimungu katika Chuo kikuu Katoliki cha Chicago na kupata diploma ya taalimungu. Akiwa na umri wa miaka 27 alitumwa na Shirika kuja Roma kusomea sheria za Kaniza za Kanoni katika Chuo Kikuu cha Kipapa cha Mtakatifu Thomas Aquinas. Alipewa daraja la Upadre tarehe 19 Juni 1982. Alipata leseni ya sheria ya Kanoni mwaka 1984, kisha akatumwa kufanya kazi utume, huko Piura, nchini Peru (1985-1986). Mnamo 1999 alichaguliwa kuwa mkuu wa Kanda ya "Mama wa Shauri jema"(Chicago). Baada ya miaka miwili na nusu, Mkutano Mkuu wa Shirika ulimchagua kuwa mkuu wa awali wa , huduma ambayo shirika lilimkabidhi tena katika Mkutano Mkuu 2007. Mnamo Oktoba 2013 alirejea jimboni kwake (Chicago) hadi Papa Francisko alipomteua, mnamo tarehe 3 Novemba 2014, kuwa msimamizi wa kitume wa jimbo la Chiclayo nchini (Peru). Alipewa Uaskofu tarehe 12 Desemba 2014 na kuwa Askofu wa Callao tarehe 26 Septemba 2015. Tarehe 15 Aprili 2020, Papa alimteua kuwa msimamizi wa kitume wa jimbo la Chiclayo. Tangu tarehe 30 Januari 2023, akateuliwa kuwa Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Maaskofu na Rais wa Tume ya Kipapa ya Amerika ya Kusini. Aliundwa na kutangazwa kuwa Kardinali katika Baraza la Makardinali tarehe 30 Septemba 2023.
Kauli mbiu:Ingawa sisi ni wakristo wengi,katika Kristo mmoja sisi ni wamoja
Kauli mbiu yake ya kiaskofu ni “In Illo uno unum,” maneno ambayo Mtakatifu Augustino alitamka katika mahubiri yake, Ufafanuzi wa Zaburi 127 , ili kueleza kwamba “ingawa sisi Wakristo ni wengi, katika Kristo mmoja sisi ni wamoja.”
Salamu za kwanza za Papa Leo XIV
Ndugu msikilizaji wa Vatican News, kwa Papa wa 267 ambaye amechaguliwa na makardinali tarehe 8 Mei 2025, ninapenda kuwakumbusha maneno yote kamili aliyotamka kwa siku ya kwanza akiwa katikati ya Kanisa Kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican mbele ya umati mkubwa wa watu waliomsubiri kuanzia asubuhi mpaka wakati huo kwa shangawe:
Amani kwenu!
Kaka na dada wapendwa, hii ni salamu ya kwanza ya Kristo Mfufuka, mchungaji mwema aliyetoa maisha yake kwa ajili ya kundi la Mungu. Nami pia ningependa salamu hii ya amani iingie mioyoni mwenu, iwafikie familia zenu, watu wote, popote walipo, kwa mataifa yote, duniani kote. Amani iwe nanyi! Hii ndiyo amani ya Kristo Mfufuka, amani iliyovuliwa silaha na amani isiyo na silaha, yenye unyenyekevu na yenye kudumu. Inatoka kwa Mungu, Mungu ambaye anatupenda sisi sote bila masharti. Bado tunaiweka masikioni sauti ile dhaifu lakini ya ujasiri ya Baba Mtakatifu Francisko akibariki Roma! Papa aliyebariki Roma alitoa baraka zake kwa ulimwengu, kwa ulimwengu wote, asubuhi hiyo ya Pasaka.
Niruhusu nitoa baraka hiyo hiyo: Mungu anatupenda, Mungu anawapenda ninyi nyote, na uovu hautashinda! Sote tuko mikononi mwa Mungu. Kwa hiyo, bila woga, tukiwa tumeungana kwa kushikana mkono kwa mkono na Mungu na sisi wenyewe kati yetu, tusonge mbele. Sisi ni wanafunzi wa Kristo. Kristo anatutangulia. Ulimwengu unahitaji nuru yake. Ubinadamu unamhitaji Yeye kama daraja la kufikiwa na Mungu na upendo Wake. Tusaidie hata nyinyi, kisha sisi kwa sisi kujenga madaraja, kwa mazungumzo, kwa kukutana, kutuunganisha sote kuwa watu wamoja daima kwa ajili ya amani. Asante Papa Francisko!
Ninapenda pia kuwashukuru ndugu Makardinali wote ambao wamenichagua kuwa Mrithi wa Petro na kutembea pamoja nanyi, kama Kanisa lenye umoja linalotafuta daima amani, haki, daima likijaribu kufanya kazi kama wanaume na wanawake waaminifu kwa Yesu Kristo, bila woga, kutangaza Injili, kuwa wamisionari. Mimi ni mtoto wa Mtakatifu Augostino, Mwaagostino, ambaye alisema: "Pamoja nanyi mimi ni Mkristo na kwa ajili yenu ni askofu".
Kwa maana hiyo sote tunaweza kutembea pamoja kuelekea nchi ya asili ambayo Mungu ametuandalia. Kwa Kanisa la Roma salamu maalum! [Makofi…] Ni lazima tutafute pamoja jinsi ya kuwa Kanisa la kimisionari, Kanisa linalojenga madaraja, mazungumzo, daima lililo wazi kwa kukaribisha kama Uwanja huu kwa mikono miwili. Kila mtu, wale wote wanaohitaji upendo wetu, uwepo wetu, mazungumzo na upendo.
Maneno ya kihispania
Y si me permiten también, una palabra, un saludo a todos aquellos y en modo particular a mi querida diócesis de Chiclayo, en el Perú, donde un pueblo fiel ha acompañado a su obispo, ha compartido su fe y ha dado tanto, tanto para seguir siendo Iglesia fiel de Jesucristo.
Na mkiniruhusu neno moja, salamu kwa wote na hasa kwa jimbo langu pendwa la Chiclayo, nchini Peru, ambako watu, waamini walisindikiza Askofu wao, walishiriki imani yao na kutoa mengi sana, kiasi cha kuendelea kuwa Kanisa aminifu la Yesu Kristo.”
Salamu kwa Roma, Italia na dunia nzima
Kwenu ninyi nyote, ndugu wa Roma, Italia, wa dunia nzima, tunataka kuwa Kanisa la kisinodi, Kanisa linalotembea, Kanisa ambalo daima linatafuta amani, ambalo daima linatafuta upendo, ambalo daima linajaribu kuwa karibu na wale wanaoteseka.
Leo ni siku ya Maombi kwa Mama Yetu wa Pompei. Mama yetu Maria daima anataka kutembea nasi, kuwa karibu, kutusaidia kwa maombezi yake na upendo wake. Kwa hiyo ningependa kusali pamoja nanyi. Tuombe pamoja kwa ajili ya utume huu mpya, kwa ajili ya Kanisa zima, amani duniani na tuombe neema hii ya pekee kwa Maria, Mama yetu.
Salamu Maria….