Papa Leo XIV,nembo na kauli mbiu iliyochapishwa
Vatican News
Nembo na kauli mbiu ya Papa Leo XIV, pamoja na sura ya Papa mpya aliyechaguliwa hivi karibuni, zimechapishwa Jumamosi tarehe 10 Mei 2025. Nembo hiyo inaonesha ngao iliyogawanywa katika sehemu mbili: ya juu yenye rangi ya blu kuna ua la lily jeupe; wakati huo huo sehemu ya chini madhari yake ni nyeupe ambayo inakumbuka Shirika la Mtakatifu Agostino ikiwa na picha ya kitabu kilichofungwa ambacho juu yake kuna moyo uliochomwa na mshale.
Picha hiyo inakumbusha tukio la kuongoka kwa Mtakatifu Agostino, ambalo yeye mwenyewe alilieleza kwa maneno ya: “Vulnerasti cor meum verbo tuo”, yaani:“Umenichoma moyo kwa Neno lako.”
Katika vipengele vyake muhimu, kwa hiyo, Papa Leo XIV alithibitisha nembo ya awali, iliyochaguliwa kwa ajili ya kuwekwa wakfu kwake wa kiaskofu pamoja na kauli mbiu yenye maneno ya kilatini: "In Illo uno unum." Haya ni maneno ambayo Mtakatifu Augostino alitamka katika mahubiri, wakati wa ufafanuzi wa Zaburi 127, kueleza kwamba: “ingawa sisi Wakristo ni wengi, katika Kristo mmoja sisi ni wamoja.”
Katika mahojiano na vyombo vya habari vya Vatican mnamo Julai 2023, Kardinali Prevost wa wakati ule mwenyewe alieleza kwamba: “Kama inavyoonekana kutoka katika kauli mbiu yangu ya uaskofu, umoja na ushirika ni sehemu ya karama ya Shirika la Mtakatifu Agostino na pia njia yangu ya kutenda na kufikiri. Nadhani ni muhimu sana kukuza ushirika katika Kanisa na tunajua vyema kwamba umoja, ushiriki na utume ni maneno matatu muhimu ya Sinodi. Kwa hiyo, kama Muagostiniani, kwangu mimi kuendeleza umoja na ushirika ni jambo la msingi. Mtakatifu Agostino anazungumza mengi kuhusu umoja katika Kanisa na haja ya kuuishi.”