Papa Leo XIV:kwa maombezi ya Maria tuombee watu wote wanaoteseka!
Na Angella Rwezaula – Vatican.
Baba Mtakatifu Leo XIV, mara baada ya sala ya Malkia wa Mbingu akiwageukia waamini na mahujai wengi waliofika katika Uwanja wa Mtakatifu Petro mjini Vatican, Dominika tarehe 25 Mei 2025 alisema “ Wapendwa kaka na Dada! Jana huko Poznań (Poland) Stanislaus Kostka Streich alitangazwa kuwa mwenyeheri, Padre wa jimbo aliyeuawa kwa kuchukiwa imani mwaka 1938, kwa sababu kazi yake kwa niaba ya maskini na wafanyakazi iliwakasirisha wafuasi wa itikadi ya kikomunisti. Mfano wake uweze kuwatia moyo hasa mapadre kutumikia kwa ukarimu kwa ajili ya Injili na kwa ajili ya ndugu zao.”
Papa akiendelea alisema “Pia jana(Jummosi 24 Mei 2025), iliadhimishwa kumbukumbu ya kiliturujia ya Bikira Maria Msaada wa Wakristo, sambamba na Siku ya Kuombea Kanisa nchini China, iliyoanzishwa na Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita. Katika makanisa na vihekalu vya China na duniani kote, sala ziliinuliwa kwa Mungu kama ishara ya kujali na upendo kwa Wakatoliki wa China na ushirika wao na Kanisa la ulimwengu wote. Kwa njia hiyo Maombezi ya Maria Mtakatifu zaidi yapate kwa ajili yao na kwetu sisi neema ya kuwa mashuhuda wa Injili wenye nguvu na furaha, hata katikati ya majaribu, ili kudumisha amani na maelewano daima,” Papa Leo alisisitiza.
Kwa kuongeza alisema “Kwa hisia hizi maombi yetu yanawakumbatia watu wote wanaoteseka kwa sababu ya vita; tunaomba ujasiri na ustahimilivu kwa wale wanaojishughulisha na mazungumzo na kutafuta amani kwa dhati.” “Miaka 10 iliyopita Papa Francisko alitia saini Waraka wa Laudato, unaojikita juu ya utunzaji wa nyumba yetu ya pamoja. Imekuwa na mtawanyiko wa ajabu, ikihamasisha juhudi nyingi na kufundisha kila mtu kusikiliza kilio cha pande mbili za Dunia na maskini. Ninawasalimia na kuwatia moyo Harakati ya Laudato si’ na wale wote wanaotekeleza ahadi hii.
Baba Mtakatifu Leo XIV kadhalika alitoa salamu: “Ninawasalimu ninyi nyote kutoka Italia na kutoka sehemu nyingi za dunia, hasa mahujaji kutoka Valencia na wale kutoka Poland, kwa baraka kwa wale wa Poland ambao wanashiriki katika hija kuu ya Madhabahu ya Maria wa Piekary ?l?skie.
Nawasalimu waamini wa Pescara, Sortino, Paternò, Caltagirone, Kaskazini Massarosa, Malnate, Palagonia na Cerello, na wale wa parokia ya Mioyo Mitakatifu ya Yesu na Maria huko Roma. Ninawasalimu kwa upendo vijana wa Jimbo Kuu la Genova, vijana wa kimapimara wa Mtakatifu Teodori, katika Jimbo la Tempio-Ampurias, waendesha baiskeli wa Paderno Dugnano na Bersaglieri wa Palermo.” Kwa kuhitimisha aliwatakia Dominika njema!