Papa Leo XIV,Kanisa Kuu Mtakatifu Maria Mkuu:Ni fursa kupyaisha ibada kwa Maria Salus Populi Romani!
Na Angella Rwezaula – Vatican.
Siku ya Baba Mtakatifu Leo XIV, Dominika tarehe 25 Mei 2025 imehitimishwa kwa kutembelea Kanisa Kuu la Mtakatifu Maria Mkuu jijini Roma ambapo ilikuwa ni tendo la kutoa heshima kwa Picha ya Bikira Maria Salus Populi Romani( Afya ya Waroma) pendwa sana kwa wazalendo wa Roma ambao wamekuwa wakisali kwa karne nyingi kuomba msaada wake. Na kwa namna hiyo Baba Mtakatifu kuanzia leo hii, amekuwa baba na mchungaji wa watu wa Roma na ndiyo maana alihitimisha siku hiyo kwa kwenda chini ya miguu ya yule Mama Bikira ambaye kwa karne nyingi amewalinda wakazi wa jiji la Roma na kuheshimika sana kama “Afya ya watu wa Roma.”
Ziara hiyo ilianzia saa 10 kamili na heshima kwa mji wa Roma aliyopokea akiwa katikati ya manispaa ya jiji na Meya wa Mji na kuendelea na safari hadi Laterano mahali ambapo aliongoza ibada ya misa Takatifu katika Kanisa Kuu la Mtakatifu Yohane huko Laterano, ambalo ndilo Kanisa Kuu lake kama Askofu wa Roma.
Baada ya kufika katika Kanisa kuu la Bikira Maria Mkuu zilifuatia sala zilizosindikizwa na kwaya nzuri sana na baada ya kumaliza Papa Leo XIV alikwenda kusali mbele ya Kaburi la Baba Mtakatifu Francisko aliyezikwa humo tangu tarehe 26 Aprili 2025 kwa utashi wake.
Papa Leo XIV kisha alipanda katikati ya dirisha la Kanisa Kuu la Mtakatifu Maria Mkuu mahali ambapo aliwasalimia waamini. Akianza salamu hizo alisema: “ Kaka na dada, amani iwe nanyi! Habari za jioni kwenu nyote. Asante kwa kuwa hapa! Asanteni kwa kuwa hapa, mbele ya Kanisa hili, mchana wa leo, jioni ya leo, tunaposherehekea, wote tumekusanyika, tukiwa washiriki wa Jimbo la Roma, uwepo wa Askofu wake mpya. “Nimefurahi sana kuwakuta nyinyi nyote hapa na ninawashukuru kutoka ndani ya moyo wangu. Ninawashukuru wale wote wanaofanya kazi katika Kanisa hili, Makardinali wawili wanaofuatana nami jioni hii na watu wengi ambao wamejitolea kutusaidia kuishi maisha yetu ya sala, ya kujitolea, na ambao zaidi ya yote wanatusaidia kumkaribia Mama wa Yesu, kwa Mama wa Mungu, Maria Mtakatifu zaidi,” alisema Askofu wa Roma.
Papa Leo XIV alikazia kusema: “ Ni fursa nzuri ya kupyaisha ibada hii kwa Maria, Salus Popoli Romani, ambaye amewasindikiza watu wa Roma mara nyingi sana katika mahitaji yao. Tumwombe Mungu kwa maombezi ya Mama yake, awabariki ninyi nyote, familia zenu, wapendwa wenu na atusaidie sote kutembea pamoja katika Kanisa, tukiwa na umoja kama familia moja ya Mungu.” Kwa kuhitimisha Papa Leo alisema “tuseme pamoja: “ Salamu Maria, Umejaa neema….) Mara baada ya sala, Papa alitoa baraka na kuwatakia wote jioni njema na shukrani nyingi!