杏MAP导航

Tafuta

Baba Mtakatifu Leo XIV, Jumamosi tarehe 31 Mei 2025, ametoa Daraja Takatifu ya Upadre kwa Mashemasi kumi na moja wa Jimbo kuu la Roma. Baba Mtakatifu Leo XIV, Jumamosi tarehe 31 Mei 2025, ametoa Daraja Takatifu ya Upadre kwa Mashemasi kumi na moja wa Jimbo kuu la Roma.  (@Vatican Media)

Papa Leo XIV Atoa Daraja ya Upadre Kwa Mashemasi 11 wa Jimbo Kuu la Roma

Baba Mtakatifu Leo XIV katika mahubiri yake amekazia, furaha ya watu wa Mungu kwa kuwapata Mapadre wapya, waliotoka kati yao na wataendelea kukua pamoja nao na kwamba, utambulisho wa wito na utume wa Mapadre unategemea kwa kiasi kikubwa mahusiano na mafungamano yao na Kristo Yesu, Kuhani mkuu na wa milele. Hii ni furaha kwa Mama Kanisa anayetafakari furaha inayobubujika kutoka katika utenzi wa Bikira Maria, mwishoni mwa Mwezi Mei. Huduma!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Leo XIV, Jumamosi tarehe 31 Mei 2025, Sikukuu ya Bikira Maria Kumtembelea Elizabeti kwa mara ya kwanza kama Khalifa wa Mtakatifu Petro na Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Roma, ametoa Daraja Takatifu ya Upadre kwa Mashemasi kumi na moja wa Jimbo kuu la Roma. Ibada hii imeadhimishwa kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican. Tukio hili lilitanguliwa na mkesha wa Sala kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Yohane wa Laterano kwa kunogeshwa pia na shuhuda za Mapadre watarajiwa. Mashemasi hawa wamepewa Daraja Takatifu ya Upadre wakati Mama Kanisa anaadhimisha kumbukumbu ya Bikira Maria kumtembelea Elizabeti, yaani tarehe 31 Mei 2025 na mwisho wa mwezi Mei, uliotengwa na Kanisa kwa Ibada ya Bikira Maria, Sanduku la Agano Jipya na la Milele. Kwa hakika ni Mama wa Mkombozi anayekwenda kumtembelea Elizabeti Hapa wanawake wawili wanaohifadhi ndani mwao Injili ya uhai wanakutana. Bikira Maria ni mtumishi wa Bwana na Elizabeti ni kielelezo cha matumaini mapya kwa Waisraeli. Rej. Lk 1:36.

Papa Leo XIV akitoa Daraja ya Upadrisho kwa Mashemasi 11 wa Roma
Papa Leo XIV akitoa Daraja ya Upadrisho kwa Mashemasi 11 wa Roma   (@Vatican Media)

Baba Mtakatifu Leo XIV katika mahubiri yake amekazia, furaha ya watu wa Mungu kwa kuwapata Mapadre wapya, waliotoka kati yao na wataendelea kukua pamoja nao na kwamba, utambulisho wa wito na utume wa Mapadre unategemea kwa kiasi kikubwa mahusiano na mafungamano yao na Kristo Yesu, Kuhani mkuu na wa milele. Hii ni furaha kwa Mama Kanisa anayetafakari furaha inayobubujika kutoka katika utenzi wa Bikira Maria, mwishoni mwa Mwezi Mei. Mapadre wapya watambue wao ni wahudumu wa watu wa Mungu na kwa kuwekewa mikono, wamempokea Roho Mtakatifu, ili kuendeleza utume wa Kristo Yesu unaofumbatwa katika ushuhuda wenye mvuto na mashiko, mashuhuda wa matumaini na upatanisho. Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican wanasema, Kristo Yesu ni kichwa cha Taifa la Kimasiha na taifa hilo, hali yake ni heshima na uhuru wa watoto wa Mungu, ambao ndani ya mioyo yao Roho Mtakatifu hukaa kama katika hekalu lake. Sheria yake ni amri mpya ya kupendana kama Kristo Yesu alivyowapenda. Rej. Yn 13:34. Mapadre wapya ni mashuhuda wa watu walioitwa na Mwenyezi, ili kushiriki katika mchakato wa furaha ya watu wa Mungu inayoleta mabadiliko, na kuwashirikisha ukaribu wa Mungu kwa waja wake, chemchemi ya utenzi wa Bikira Maria, alama ya watu waliotembelewa na neema ya Mungu.

Papa Leo XIV akitoa Daraja Takatifu ya Upadre
Papa Leo XIV akitoa Daraja Takatifu ya Upadre   (@Vatican Media)

Roho Mtakatifu anaimarisha mahusiano na mafungamano ya watu wa Mungu, na sala inapata nguvu zaidi kuliko kifo. Mahusiano haya ndiyo yaliyopelekea hata Injili kuweza kuwafikia watu wengi. Mapadre wapya wamewekwa wakfu kuwa ni: Makuhani, Wafalme na Manabii kwa ajili ya kuwahudumia watu wa Mungu, kama ilivyokuwa kwa Kristo Yesu, bila hata ya mastahili yao. Hii ni changamoto kwa Mapadre wapya kujisadaka bila ya kujibakiza, kwa kuondokana na uchoyo na ubinafsi, changamoto iliyokuwa ikitolewa mara kwa mara na Hayati Baba Mtakatifu Francisko. Mapadre wapya ni wahudumu wa Fumbo la Ekaristi Takatifu na hivyo amewakirimia pia nguvu ya kufanyika watoto wateule wa Mungu. Kristo Yesu katika maisha na utume wake, aliwawekea mikono watoto, akawaponya wagonjwa na Mapadre wapya kwa kuwekewa mikono wamempokea Roho Mtakatifu, ili kujenga umoja unaosimikwa katika uhuru wao binafsi na kwamba, Roho Mtakatifu amewaweka wao kuwa waangalizi ndani yake. Rej. Mdo 20:28.

Mapadre ni sehemu ya watu wa Mungu kwa ajili ya mambo ya Kimungu
Mapadre ni sehemu ya watu wa Mungu kwa ajili ya mambo ya Kimungu   (@Vatican Media)

Kristo Yesu aliyeteswa, akafa, amefufuka kwa wafu na kwamba, kupaa kwake mbingu ni alama ya uwepo wake usioonekana, changamoto na mwaliko kwa Mapadre wapya kutoa mwanya kwa maisha na utume wa Kristo Yesu, ili Kristo Mfufuka aweze kuwatembelea na kuwa karibu na waja wake na kwamba, idadi ya watu wa Mungu ni kubwa. Mtakatifu Paulo Mtume katika hotuba yake ya kuagana na wazee anakazia kwa namna ya pekee ukweli na uaminifu katika maisha, ili kweli waweze kuwa ni mashuhuda amini, wenye mvuto na mashiko, ili hatimaye, kujenga na kudumisha Kanisa linaloaminika, Kanisa lenye makovu, linalotumwa kwa binadamu waliojeruhiwa pamoja na kazi ya uumbaji yenye kujeruhiwa, lakini Mapadre wapya wanapaswa kuwa waaminifu.

Mapadre wajenge na kudumisha ari na moyo wa Kanisa la Kisinodi
Mapadre wajenge na kudumisha ari na moyo wa Kanisa la Kisinodi   (@Vatican Media)

Baba Mtakatifu Leo XIV anasema, Kristo Yesu anawaonesha Madonda yake Matakatifu, lakini kwa binadamu si rahisi kuupokea ujumbe huu. Lakini Kristo Yesu anaendelea kuwasamehe na kuwatuma kama anavyoendelea kufanya hata sasa, Rej. Yn 20: 22 ili hatimaye waweze kuwa ni wamisionari wa matumaini, umoja na alama ya upatanisho. Baba Mtakarifu Leo XIV anakaza kusema, upendo wa Mungu umewakumbatia na kuwaambata wote na kuwaokoa na kwamba, wao ni watu wa Mungu wanaopendwa na Mwenyezi Mungu aliyeupenda ulimwengu hata akamtuma Mwanaye wa pekee, ili kila mtu amwaminiye asipotee, bali awe na uzima milele. Rej Yn 3:16. Huu ni ushuhuda wa Mapadre wapya wanaosadaka maisha yao, mwaliko wa kumshukuru Mungu kwa kuwaita katika huduma ya Kikuhani, ili waweze kuunganisha mbingu na dunia. Bikira Maria, Mama wa Kanisa anayewezesha Ukuhani wao kung’ara kwa kuwainua wanyenyekevu, anawawezesha kuitwa wenye heri. Bikira Maria wa Matumaini na Mama wa Shauri Jema aendelee kuwaombea.

Daraja Takatifu
31 Mei 2025, 15:13