Papa Leo XIV akutana na Patriaki umuhimu wa kuimarisha majadiliano ya kitaalimungu!
Na Angella Rwezaula – Vatican.
Papa Leo XIV alimhakikishia Patriaki wa Kiekumeni Bartholomew I shauku yake ya dhati ya kusafiri hadi Uturuki, ndani ya mwaka huu na tarehe itakayopangwa, kuadhimisha pamoja na Patriaki kumbu kumbu ya miaka 1700 tangu kufanyika kwa Mtaguso wa kwanza wa Kiekumene wa Nicea." Hivi ndivyo Patriaki wa Kiekumene alitangaza katika taarifa yake iliyotolewa kwenye ukurasa wao wa upatriaki kuhusiana na mkutano ambao Patriaki huyo alikuwa nao Jumatatu tarehe 19 Mei 2025 mjini Vatican na Papa Leo XIV.
Katika taarifa hiyo aidha inabainisha kuwa wakati wa mkutano huo mzuri, Patriaki Bartholomew binafsi alimpongeza Papa mpya Leo XIV kwa kuchaguliwa kwake na katika mazungumzo hayo alisisitiza, pamoja na mambo mengine, umuhimu wa kuendelea kukuza na kuimarisha mazungumzo ya kitaalimungu kati ya Makanisa mawili, yaani ya Kiorthodox na Kanisa Katoliki la Roma, pamoja na ushirikiano wao katika masuala ya maslahi ya kijamii, kama vile kurejesha na kudumisha amani duniani, kusaidia watu wanaoteseka na mazingira. Patriaki huyo pia alitaja uhusiano na ushirikiano wa kidugu aliokuwa nao na hayati Papa Francisko, ambaye alikutana naye zaidi ya mara kumi.
Baba Mtakatifu Leo XIV hata hivyo alitoa shukrani zake kwa Patriaki huyo kwa uwepo wake katika Misa ya ufunguzi wa huduma yake ya Mfuasi wa Mtume Petro na pia kusisitiza umuhimu wa kukuza mazungumzo na ushirikiano wa kiekumene. Kuhusu hija ya Nicea, Upatriaki wa kiekumene ulikumbusha kwamba Patriaki Bartholomw I pia alikuwa amemwalika Hayati Papa Francisko kwa kusudi hilo na kwa hivyo akafanya kwa upya mwaliko wake kwa mrithi wake Papa Leo XIV.
Wakati wa kubadilishana zawadi, Patriaki wa Kiekumene alimpatia Papa Leo XIV sanamu ya Bikira Maria Hodegetria, iliyochorwa kwenye Mlima Athos, uvumba wa miski uliotayarishwa na watawa wa Athonite na vitabu vyake. Papa alimpatia Patriaki Bartholomew uwakilishi wa kisanii wa ubatizo wa Bwana. Baadaye, katika Ukumbi wa Clementine mjini Vatican, Papa aliwakaribisha na kuzungumza na wawakilishi wa Makanisa na dini nyingine, waliohudhuria Dominika tarehe 18 Mei 2025 katika ibada ya Misa ya kuanza kwake huduma ya Mfuasi wa Petro ambapo aliwasalimia mjumbe mmoja moja.
Kutembelea kaburi la Papa Francisko
Mapema alasiri, Patriaki na wasaidizi wake walitembelea Ubalozi wa Jamhuri ya Uturuki. Kutoka hapo, Patriaki wa Kiekumene alikwenda moja kwa moja kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Maria Mkuu, ambako alisali na kuweka maua meupe kwenye kaburi la Hayati Baba Mtakatifu Francisko. Patriaki baada ya hapo alitembelea kwa hisia Taasisi ya Kipapa ya Mafunzo ya Mashariki, ambako alisomea katika miaka ya 1963-1966, akibobea katika Sheria za Kanisa.