Papa kwa vyuo vikuu vya Amerika Kaskazini,Kusini na Kati:viwe madaraja ya ushirikiano
Vatican News
Baba Mtakatifu Leo XIV Jumanne tareeh 20 Mei 2025 alituma ujumbe kwa njia ya video kwa wakuu wa vyuo vikuu zaidi ya 200 vya Kaskazini, Kusini, Amerika ya Kati na Peninsula ya Iberia waliokusanyika, kuanzia Mei 20 hadi tarehe 24 Mei 2025 katika Chuo Kikuu cha Kipapa Kikatoliki cha Rio de Janeiro (PUC-Rio) kwa mkutano wa sinodi ulioandaliwa na Mtandao wa Vyuo Vikuu kwa ajili ya Huduma ya Nyumba ya Pamoja kwa msaada wa Tume ya Kipapa ya Amerika ya Kusini. Hizi ni siku nne za mazungumzo, utambuzi na mapendekezo ya hatua za kushughulikia mzozo wa kijamii na kimazingira, katika maadhimisho ya miaka kumi ya waraka wa Papa Francisko Laudato si’ na kujiandaa kwa Cop30, itakayofanyika Belém, Brazili, Novemba ijayo mwaka huu.
Katika ujumbe huo kwa lugha ya kihispania Papa Leo XIV anasema kuwa “Ndugu wapendwa, ninataka kutuma salamu hii, salamu kubwa, kwa Mtandao wa Vyuo Vikuu kwa ajili ya Utunzaji wa Nyumba ya Pamoja. Najua kwamba mmekusanyika katika Chuo Kikuu cha Kipapa cha Kikatoliki cha Rio de Janeiro na kwamba mna tukio hili nzuri la kumbukumbu ya miaka 10 ya waraka wa Baba Mtakatifu Francisko, wa Laudato si'. Ninajua kwamba mnakaribia kufanya kazi ya sinodi ya utambuzi katika matayarisho ya COP30.
Mtatafakari pamoja juu ya uwezekano wa kusamehewa kwa deni la umma na deni la kiikolojia, pendekezo ambalo Papa Francisko alikuwa amependekeza katika ujumbe wake kwa Siku ya Amani Duniani. Na katika Mwaka huu wa Jubilei, mwaka wa matumaini, ujumbe huu ni muhimu sana. Papa Leo XIV alikazia kusema kuwa “Ningependa kuwatia moyo, wakuu wa vyuo vikuu, katika dhamira hii ambayo mmechukua ya kuwa wajenzi wa madaraja ya ushirikiano kati ya Amerika na Peninsula ya Iberia, kufanya kazi kwa haki ya kiikolojia, kijamii na mazingira. Nawashukuru nyote kwa juhudi zenu na kazi zenu. Ninawahimiza muendelee kujenga madaraja. Kwa kuhitimisha Papa Leo XIV alisema: “Na ningependa kumalizia kwa baraka, nikitumaini kwamba neema ya Mungu iko pamoja nanyi daima: Baraka ya Mwenyezi Mungu, Baba, Mwana na Roho Mtakatifu iwashukie na kuwasindikiza daima. Amina.”