Papa Leo XIV kwa PMS ni njia kuu ya kuamsha uwajibu wa kimisionari kwa wabatizwa!
Na Angella Rwezaula – Vatican.
Ulimwengu wetu uliopigwa na kujeruhiwa kwa vita, vurugu na ukosefu wa haki inahitaji haraka kusikiliza na kuona ahadi ya kiinjili ya amani ya kweli na ya kudumu. Kanisa, katika tangazo lake, linaitwa kuvunja mipaka iliyoamriwa na parokia, majimbo na mataifa, ili kutafuta ushirika kamili na maelewano katika Kristo. Wakurugenzi watembee majimbo, maparokia na maeneo yote ili kuelewesha utume wa PMS haya namengine zaidi yamo katika hotuba ya Baba Mtakatifu Leo XIV asubuhi tarehe 22 Mei 2025 na wahusima wa Mkutano Mkuu wa Mashirika ya Kimissionari ya Kipapa,(PMS) katika Ukumbi wa Clementina Mjini Vatican.
Baada ya utangulizi wa salamu kwa kiitaliano, Papa Leo XIV aliendelea na hotuba yake kwa lugha ya kiingeza akisema ninawakaribisha nyote mliokusanyika kutoka zaidi ya nchi mia moja na ishirini ili kushiriki katika Mkutano Mkuu wa mwaka wa Mashirika ya Kimisionari ya Kipapa. Ninataka kuanza kwa kutoa shukrani zangu kwenu na kwa washirika wenu kwa ajili ya huduma yenu ya kujitolea, ambayo ni ya lazima kwa utume wa Kanisa la uinjilishaji, kama ninavyoweza binafsi kuthibitisha kutokana na uzoefu wangu wa kichungaji katika miaka ya huduma ya kuhudumu nchini Peru. Mashirika ya Kimissionari ya Kipapa kwa hakika ndiyo “njia ya msingi” ya kuamsha wajibu wa kimisionari kati ya jumuiya zote za kikanisa zilizobatizwa na kuunga mkono katika maeneo ambayo Kanisa ni changa (taz. Ad Gentes, 38).
Papa Leo XIV alisema kuwa "Tunaona haya katika Jumuiya ya Kueneza Imani, ambayo hutoa msaada kwa mafunzo ya kichungaji na katekesi, ujenzi wa makanisa mapya, huduma za afya, na mahitaji ya elimu katika maeneo ya utume. Shirika la Utoto Mtakatifu pia, hutoa msaada kwa ajili ya programu za malezi ya Kikristo kwa watoto, pamoja na kujali mahitaji yao msingi na ulinzi. Vilevile, Shirika la Mtakatifu Petro Mtume linasaidia kuhamasisha miito ya kimisionari ya kipadre na kitawa, wakati Umoja wa Wamisionari unajizatiti kuunda mapadre, wanaume na wanawake watawa, na watu wote wa Mungu kwa ajili ya shughuli za kimisionari za Kanisa. Uhamasishaji wa bidii ya kitume kati ya Watu wa Mungu bado ni kipengele muhimu cha upyaisho wa Kanisa kama inavyotazamiwa na Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican, na ni wa dharura zaidi katika siku zetu hizi. Ulimwengu wetu, uliojeruhiwa na vita, vurugu na ukosefu wa haki, unahitaji kusikia ujumbe wa Injili ya upendo wa Mungu na kupata uzoefu wa nguvu ya upatanisho ya neema ya Kristo."
Kwa kukazia zaidi Papa alisema "Kwa maana hiyo, Kanisa lenyewe, katika washiriki wake wote, linazidi kuitwa kuwa “Kanisa la kimisionari linalofungua mikono yake kwa ulimwengu, linalotangaza neno … na kuwa chachu ya maelewano kwa wanadamu” (Homilia, Misa ya Mwanzo wa Upapa, 18 Mei 2025). Tunapaswa kuwapelekea watu wote, kwa hakika kwa viumbe vyote, ahadi ya Injili ya amani ya kweli na ya kudumu, ambayo inawezekana kwa sababu, kwa maneno ya Baba Mtakatifu Francisko, “Bwana ameushinda ulimwengu na mapambano yake ya kudumu ‘kwa kufanya amani kwa damu ya msalaba wake’” (Evangelii Gaudium, 229). Kwa hiyo tunaona umuhimu wa kukuza roho ya uanafunzi wa kimisionari kwa wote waliobatizwa na hisia ya uharaka wa kumpeleka Kristo kwa watu wote. Kwa maana hiyo, Baba Mtakatifu Leo XIV alipenda kuwashukuru wao na washirika wao kwa jitihada zao za kila mwaka katika kutangaza Dominika ya Umisionari Duniani katika Dominika ya pili hadi ya mwisho wa Oktoba, “ambayo ni msaada mkubwa kwangu katika maombi yangu kwa ajili ya Makanisa katika maeneo ambayo yapo chini ya uangalizi wa Baraza la Kipapa la Uinjilishaji.”
Baba Mtakatifu alibainisha kuwa: "Leo hii, kama ilivyokuwa katika siku za baada ya Pentekoste, Kanisa, likiongozwa na Roho Mtakatifu, linaendelea na safari yake katika historia kwa uaminifu, furaha na ujasiri linapotangaza jina la Yesu na wokovu unaozaliwa kwa imani katika ukweli unaookoa wa Injili. Mashirika ya Kimisionari ya Kipapa ni sehemu muhimu ya juhudi hii kubwa. Katika kazi yao ya kuratibu malezi ya kimisionari na kuhuisha moyo wa kimisionari katika ngazi mahalia, Papa amewaomba Wakurugenzi wa Kitaifa kutoa kipaumbele kwa kutembelea Majimbo, parokia na jumuiya, na kwa njia hii kuwasaidia waamini kutambua umuhimu wa kimsingi wa umisionari na kusaidia kaka na dada zetu katika maeneo yale ya ulimwengu wetu ambapo Kanisa ni changa na linakua.
Kabla ya kuhitimisha maneno hayo akiwa pamoja nao asubuhi ya hiyo Papa, alipenda kutafakari pamoja nao vipengele viwili bainifu vya utambulisho wao kama Mashirika ya Kimisionari ya Kipapa, yanavyoweza kuelezewa kuwa ni umoja na ushirika. Kwa vile Mashirika yaliyojitolea kushiriki katika jukumu la kimisionari la Papa na Baraza la Maaskofu, wanaalikwa kukuza na kuhamasisha zaidi ndani ya washiriki wao maono ya Kanisa kama ushirika wa waamini, wanaotiwa nguvu na Roho Mtakatifu, anayetuwezesha kuingia katika ushirika mkamilifu na kupatana na Utatu uliobarikiwa. Hakika, ni katika Utatu kwamba vitu vyote vinapata umoja wao. “Hali hii ya maisha na utume wetu wa Kikristo iko karibu na moyo wangu, na inaonekana katika maneno ya Mtakatifu Agostino niliyochagua kwa ajili ya huduma yangu ya uaskofu na sasa kwa ajili ya huduma yangu ya upapa: In Illo uno unum. Kristo ni Mwokozi wetu na ndani yake sisi ni wamoja, familia ya Mungu, zaidi ya wingi wa lugha, tamaduni na uzoefu wetu.”
Kuthamini ushirika wetu kama washiriki wa Mwili wa Kristo hutufungua kwa kawaida kwa mwelekeo wa ulimwengu wote wa utume wa Kanisa wa uinjilishaji, na hututia moyo kuvuka mipaka ya parokia zetu binafsi, majimbo na mataifa, ili kushiriki na kila taifa na watu utajiri unaopita wa maarifa ya Yesu Kristo (taz.8 Fil 3:8). Mtazamo mpya wa umoja wa Kanisa na ulimwengu wote unalingana kabisa na karama halisi ya Mashirika ya Kimisionari ya Kipapa(PMS). Kwa hivyo, inapaswa kuhamasisha mchakato wa upyaishaji wa sheria ambazo yameanzisha. Kwa maana hiyo, Papa ameeleza imani yake kwamba mchakato huu utawathibitisha wanajumuiya wa Mashirika duniani kote katika wito wao wa kuwa chachu ya ari ya kimisionari ndani ya Watu wa Mungu.
Kwa kutazama Jubilei kuu inayoendelea Papa Leo XIV alisema: "Wapendwa, maadhimisho yetu ya Mwaka huu Mtakatifu yanatupatia changamoto sisi sote kuwa “mahujaji wa matumaini.” Nikichukua maneno ambayo Papa Francisko aliyachagua kama mada ya Siku ya Utume Duniani mwaka huu, ningehitimisha kwa kuwatia moyo kuendelea kuwa “wamisionari wa matumaini miongoni mwa watu wote.” Nikiwapongeza, wafadhili wenu na wote wanaohusika na kazi yenu muhimu kwa maombezi ya upendo ya Maria, Mama wa Kanisa, ninawapa kwa moyo mkunjufu Baraka yangu ya Kitume kama ahadi ya furaha na amani ya kudumu katika Bwana.