杏MAP导航

Tafuta

Nafasi ya mtume Petro,katekesi ya Francisko katika mahojiano

Rekodi ya 2021,ambayo ilikuwa ijumuishwe katika waraka,itatangazwa na kituo cha televisheni cha ESNE "El Sembrador,Nueva Evangelización."Papa akitafakari juu ya vifungu vya Biblia vya mazungumzo kati ya Yesu na mfuasi wake,kwa mara nyingine tena alionesha hamu ya Kanisa kuwa mtumishi mnyenyekevu katikati ya dunia.

Vatican News

Imani kamili kwa Mungu, mwamko wa kuwa dhaifu na wenye dhambi, wito mpya kwa mapadre kumtumikia kila mtu, pongezi zake kwa wafiadini wa siku hizi na kujali kwake wahamiaji, ni baadhi ya mada ambazo Papa Francisko alizungumzia mwaka 2021 katika mazungumzo na Noel Díaz huko nyumba ya Mtakatifu Marta mjini Vatican. Noel Díaz ndiye mwanzilishi wa chama cha waamini wa  “El Sembrador, Nueva Evangelización” kinachotangaza Neno la Mungu kupitia televisheni na radio.

Yafuatayo ni mahojiano kamili.

Leo wewe ni mrithi wa mtu huyo aitwaye Simoni. Maandiko haya yanakukumbusha nini, Baba Mtakatifu?

Mambo mengi! Kwamba Yesu anamwita Simoni kati ya watu, hamtenganishi na watu. Kuna watu wengi na Yesu anahubiri, na watu wanakwenda kumsikiliza Yesu kwa sababu wana kiu ya Neno la Mungu. Na Yesu anazungumza kama mtu aliye na mamlaka. Kwanza, Yesu daima huwaita makuhani wake kutoka katika watu, kati ya watu. Ikiwa Petro angesahau asili yake, angesaliti mpango wa Yesu, angeanzisha wasomi. Hapana! Mchungaji lazima awe pamoja na kondoo. Ndiyo maana yeye ni mchungaji. Pili, ishara ambazo Yesu anafanya, si mamlaka ya Neno lake tu. Ili wapate kumwamini Yeye, anafanya muujiza huo wa ajabu, na hakuna mtu aliyetarajia. Popote alipo Yesu, nguvu zake zinaonekana; na Petro, wakati ana shaka, wakati hana nguvu, atakumbuka, muujiza huu, kwamba Bwana ana uwezo wa kubadilisha mambo.

Je Petro anafanya nini anapomwona Yesu akifanya hivyo? Anapiga magoti mbele Yake, hajisikii chochote, mnyenyekevu, anatambua kwamba ana mipaka, kwamba yeye ni mwenye dhambi. "Bwana, ondoke kwangu, kwa maana mimi ni mwenye dhambi." Na hapo ndipo Yesu anafika anapotaka kufika. Safari ya Petro ni kuwa pamoja na watu kumsikiliza Bwana. Kwenda kuvua samaki kulingana na agizo la Bwana na kufanya muujiza huu. Tatu, kutambua udogo wake, kutokuwa na kitu kwake, na kumwambia Bwana: "Ondoka, kwa maana mimi ni mwenye dhambi." "Kwa kuwa wewe ni mwenye dhambi, kwa sababu umenifuata mimi, sasa nitakufanya kuwa mvuvi wa watu." Hii ni hatua ya nne. Yesu anapomtia mafuta, askofu, kuhani, anamtia mafuta kwa sababu yeye ni mchungaji. Hampaki mafuta ili kumpandisha cheo, kuwa mkuu wa ofisi. Hampaki mafuta kupanga nchi kisiasa. Hapana. Anamtia mafuta kuwa mchungaji…. na [Petro] anaacha kila kitu.

Na unahisije kuhusu kuchukua nafasi ya Petro?

Ninahisi kwamba Bwana ananisindikiza, kwamba ndiye anayechagua, ndiye aliyeanzisha historia hii. Alianza na mimi, Alinialika, Akanisindikiza. Na licha ya dhambi zangu, kwa sababu mimi ni mwenye dhambi kama Petro, Yeye haniachi. Kisha ninahisi kwamba Yeye ananitunza.

(Noel Díaz anatanguliza usomaji wa Biblia ambamo Yesu anawauliza mitume wake watu wasemavyo kuhusu Yeye. Kisha Petro anamtambua hadharani kuwa ndiye Masiha)

Hapo Yesu anaanza na uchunguzi, anataka kusikiliza. Na anasema: "Watu wanasema nini juu yangu?" "Wanasema wewe ni nabii, ya kuwa wewe ni Yohane Mbatizaji, kwamba umefufuka." Baada ya kuwauliza watu wanasema nini, Yesu anawauliza: “Lakini ninyi?”, yaani, anawauliza maswali. Yesu anatugeukia na kutuuliza hata sisis: “Wewe wasema nini juu yako mwenyewe, wasema nini kunihusu? Ni mazungumzo na Yesu. Anatuita kwa majina. Na Petro alikuwa tayari amejitambulisha kuwa kiongozi, kwa sababu Yesu alimwambia siku ya kwanza, alipokutana naye na kubadili jina lake: "Wewe ni Simoni, lakini utaitwa Petro.” Alikuwa amemweka kama jiwe la msingi la kundi. Na Petro anafanya kukiri kwake  imani, anajiweka kwenye mstari kabisa. Hebu tufikirie tukio la kumwambia mtu: "wewe si ‘Tizio’ wala ‘Caio’, wewe ni Mungu, Mwana wa Mungu" (yaani majina dhania bali…). Ikiwa wewe utajimbulisha hivyo leo hii, watakupeleka hospitali ya magonjwa ya akili, watasema amerukwa na akili.

Alijiweka kabisa mbele na kuthubutu, na Yesu anaeleza kwa nini alikuwa na ujasiri wa kujiweka mbele: "kwa sababu uliyosema hayakufunuliwa kwako na sayansi yoyote, bali na Baba kwa Roho wake." Na kwa hiyo anapomwona Petro akijiweka katika mstari wa mbele, anathibitisha hilo kwa jina lake: “Wewe, Simoni, mwana wa Yona, uliye mwamba, juu ya mwamba huu nitalijenga Kanisa langu.” Juu ya udhaifu wa mtu ambaye ana uimara wa mwamba kiasi cha kutegemea neno la Yesu. Anapojitenga na neno la Yesu, anafanana na mtu mwingine yeyote, hana uimara wa jiwe. Hii ndiyo sababu anamchagua, kwa sababu ana uimara kama wa jiwe. Petro anashangazwa na kile Yesu anachomwambia: "Baba yangu alikufunulia hili.” Kisha Yesu anasema, “Vema, jueni kwamba sasa nitakwenda Yerusalemu na mambo mabaya yananingojea huko. Watanihukumu, wataniua, watanisulubisha, lakini nitafufuka tena.”

Kisha Petro, ambaye tayari alijisikia kidogo kama kiongozi wa kundi, anamwita kando.” Injili inasema: “Bwana, tafadhali, si hivyo” Naye Yesu, ambaye alikuwa amemsifu Petro, ambaye alikuwa amemwambia: "Ninyi ni kipokezi cha ufunuo wa Baba yangu", anamkemea. Alimwambia: “Nenda nyuma yangu, Shetani!” neno baya zaidi. Kwa nini? Kwa sababu anataka kumtenga na njia yake ya msalaba. Haya yalikuwani masahihisho makubwa kwa Papa wa kwanza, kwa Petro. Hata kwetu sisi Mapapa, Yesu, ikiwa nyakati fulani tunajitenga na mpango wake wa wokovu, anasema: “Hii si njia yangu, ni njia ya Shetani.” Kwa nini? Kwa sababu sisi ni wenye dhambi na tunaweza kujitenga wenyewe. Historia inatuonesha baadhi ya Mapapa ambao wamependelea njia tofauti, hata kama hawajawahi kamwe kufanya makosa katika imani yao. Ni kweli, kamwe, hata kama wameishi maisha ya kidunia. Na [Petro] anapofanya makosa katika imani yake, anasema: "Hapana, hii ni ya Shetani. Njia yangu ni msalaba." Yaani tumaini langu limewekwa katika neno la Yesu anitiaye nguvu anaponichagua na kunipiga makofi ninapokosea.

Ni vigumu sana wakati mwingine kukabiliana na changamoto na mashambulizi ya ulimwengu wa kidunia, lakini nina hakika kwamba ni chungu zaidi kukabiliana na mashambulizi kutoka ndani. Hivi ndivyo “Wewe ni Petro” anasema. Sasa wewe ni mrithi wa Petro na, hata mashambulizi haya yote yakija, nguvu hazitashinda, linasema Neno la Mungu. Ni nguvu zipi ambazo Yesu anasema hazitashinda? Yesu anasema nini?

Nguvu za uovu. Za uovu, za kuzimu! Hiyo ni, unapoweka tumaini lako si katika ufunuo wa Baba wala katika uchaguzi wa Yesu, lakini kwa njia nyingine, katika fedha, kwa mfano. "Tuko vizuri kwa sababu wana pesa.  Hebu tumfikirie padre, askofu anayesema: “Kanisa letu linaendelea vizuri, tuna watu wa kawaida wanaotupatia pesa, na linaendelea mbele.” Usiweke tumaini lako hapo kwa sababu vinginevyo utaanguka. Ni nguvu za kuzimu, sio nguvu za ufunuo wa Baba. Walimtukana Yesu, wakamsulubisha, na kama walimtendea yeye, je  mimi ni nani hata wasinitendee? Ikiwa walimtendea Mwalimu hivyo, mwanafunzi yeyote kati yenu, hahitaji kuwa Papa, haombi kitu kingine chochote. Wafiadini wengi sana Kanisani hutufundisha hili.

(Noel Díaz anamruhusu ajibu andiko la Yohane 21, ambamo Yesu anamwuliza Petro kama anampenda, basi amthibitishe katika utume wake, lakini pia kumwambia kwamba njia haitakuwa rahisi)

Uthibitisho na ahadi. Petro alipokiri hivyo, Yesu alikuwa amemuahidi kwamba milango ya kuzimu haitashinda, kwamba angebaki imara maadamu yuko juu ya mwamba. Hapa anathibitisha mara tatu. Petro anahuzunika kwa sababu anakumbuka zile mara tatu alizomkana, kisha anahuzunika, na mwishowe Bwana anathibitisha hilo kwa mara ya tatu. Je, labda anamwambia “kuanzia sasa hakuna kibaya kitakachokupata, sasa utakuwa na uwezo wote, sasa utakuwa na pesa zote, sasa watu watakufuata”? Labda anamwambia hivi? Hapana! Anamwambia: “Endelea, maana utakapokuwa mzee utakwenda usipotaka, watakupeleka usipotaka, watakuvua nguo na utaishia kama mimi niliyesulubiwa”. Bwana anamuahidi Petro njia yake, njia ya msalaba, njia ya utoaji kamili, njia ya kuweka imani kwake tu. Inashangaza kwamba wakati Petro anakiri kwamba Yesu ni Mwana wa Mungu - nguvu za Roho Mtakatifu humfanya akiri hivyo - basi anapoteza uwezo wake. Na Yesu anapozungumza juu ya msalaba, anajaribu kumsadikisha vinginevyo. Petro anaanguka katika mawazo ya kidunia na jambo lile lile linatokea hapa. Yesu anamwambia hivyo, anakubali, kisha [Petro] amgeukia Yohane na kumuuliza: “Bwana, akiwa hapa, itakuwaje kwake? Ni Petro msengenyaji, Petro ambaye anasahau wakati huo kile ambacho Bwana alimwambia kusengenya juu ya mtu mwingine.

Tuko hivi, lakini Bwana hututunza kwa uweza wake, hata inapobidi tukabiliane na kifo cha kishahidi, anatusindikiza kwa mkono wake. Na nikizungumzia kifo cha kishahidi, ningependa kumalizia kwa kuwazungumzia wafiadini wa leo. Kuna wafia imani wengi leo hii kuliko mwanzo wa Kanisa. Wakristo wafiadini waliokatwa vichwa kwa sababu tu ya kuwa Wakristo na wanaomkiri Yesu. Wafiadini ambao wako gerezani kwa kumkiri Yesu. Ni ndugu zetu! Ni Kanisa la mashahidi. Hili ndilo Kanisa linaloshinda, si Kanisa lenye pesa katika benki. Hili ndilo Kanisa linaloshinda, Kanisa la wafia imani, la ushuhuda. Kwa sababu kifo cha kishahidi kinamaanisha ushuhuda. Nilitaja wale wanaotoa maisha yao, lakini pia kwamba mwanamume, yule mwanamke anayefanya kazi kila siku kuwasomesha watoto wake katika maisha ya Kikristo na kuwatolea ushuhuda, ni shahidi. " Hapana, baba, anawezaje kuwa shahidi ikiwa hawakumuua?" Hapana, shahidi maana yake ni shahidi. Kuuawa kwa imani ni ushuhuda, ni tafsiri ya neno la Kigiriki. Shahidi yeyote wa Yesu ni shahidi, yaani, anashuhudia. Na pia analipeleka Kanisa mbele. Mungu awabariki nyote na mniombee tafadhali.

(Noel Díaz anaomba baraka kwa kila mtu)

Na kwa ninyi nyote, mnaotazama na kusikiliza mazungumzo haya, ninatumaini kwamba Bwana atafungua mioyo yenu na kuruhusu Neno lake kuingia humo. Kwa hivyo ninawabariki kwa moyo wangu wote. Ninakubariki. Nawapeni baraka zangu kama baba, kama kaka mkubwa, kama mtumishi wenu nyote. Mwenyezi Mungu awabariki, Baba, Mwana na Roho Mtakatifu. Na tafadhali, mniombee. Asante.

(Noel Díaz anaomba baraka ya pili kwa wahamiaji). Haya yote yanawakilisha wahamiaji, niliwaambia nitaomba baraka zake.

Kufikiria wahamiaji, wale ambao wamelazimika kuondoka katika nchi yao, ambao wanakaribishwa na watu wengi wazuri au watu wasiojali, ambao wako kwenye njia ya uhamishoni, mbali na nchi yao, ambao wanahisi hamu ya marafiki, familia, uzuri wa nchi yao: kwa wote ninawapa baraka yangu kwa jina la Baba, Mwana na Roho Mtakatifu.

Mazungumzo ya Dias na Papa Francisko

 

03 Mei 2025, 11:51