Papa Leo XIV akutana na Rais wa Colombia
Vatican News
Baba Mtakatifu Jumatatu 19 Mei 2025 amekutana na Rais wa Jamhuri ya Colombia, Bwana Gustavo Francisco Petro Urrego, aliyefika Roma kwa ajili ya maadhimisho ya Ekaristi ya mwanzo wa huduma ya Mfuasi wa Mtume Petro, Papa Leo XIV, Dominika tarehe 18 Maggio kwenye Uwanja wa Mtakatifu Petro.
Baada ya mkutano na Papa kwa mujibu wa taarifa za Ofisi ya Waandishi wa Habari ya Vatican - Rais alikwenda katika Sekretarieti ya Vatican na kuzungumza na Askofu Mkuu Paul Richard Gallagher, Katibu wa Mahusiano na Mataifa na Mashirika ya Kimataifa. Wakati wa mkutano huo walionesha kuridhika kwa uhusiano mzuri kati ya Colombia na Vatican, wakisisitiza ushirikiano mzuri na wa kudumu kati ya Kanisa na Vatican katika kuunga mkono michakato ya amani na upatanisho".
Amani, upatanisho na uhamiaji
Mada zilizojadiliwa pia zilijumuisha hali ya kijamii na kisiasa ya Colombia na Kanda, kwa kuzingatia hasa changamoto zinazohusiana na usalama, uhamiaji na mabadiliko ya tabianchi. Mara ya mwisho Rais wa nchi hiyo ya Amerika Kusini alipokuwa Vatican ilikuwa tarehe 19 Januari 2024 alipokutana na Papa Francisko.
Na hiyo ilikuwa ni mazungumzo ya kwanza baada ya kuchaguliwa kuwa mkuu wa nchi mwezi Agosti 2022. Mnamo Februari mwaka huo tayari alikuwa amemwona Papa alipokuwa mgombea wa kiti cha urais wa Colombia na hata kabla ya hapo, mwaka 2015, akiwa meya wa Bogota, alikuwa amekuja Vatican kwa ajili ya tukio juu ya masuala ya utumwa mamboleo na mabadiliko ya hali ya tabianchi.