Maombolezo Kifo cha Papa Francisko: Makanisa ya Mashariki
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Mkristo anayekufa katika Kristo Yesu huuacha mwili ili kwenda kukaa pamoja na Mwenyezi Mungu, milele yote! Kwa Mkristo, siku ya kifo huanzisha, mwishoni mwa maisha yake ya Kisakramenti, utimilifu wa kuzaliwa kwake upya kulikoanzishwa na Sakramenti ya Ubatizo, kufanana kamili na sura ya Mwana, kulikotolewa kwa Mpako wa Roho Mtakatifu na ushirika katika karamu ya Ufalme, uliotangulizwa katika Ekaristi, hata kama ana lazima bado kutakaswa zaidi ili kuvikwa vazi la arusi! Waamini wanahamasishwa kulitafakari Fumbo la kifo, kama sehemu ya matumaini ya Kikristo kwani, Kristo Yesu mwenyewe anasema, ndiye ufufuo na uzima na kwamba, yeyote anayemwamini ajapokufa atakuwa anaishi na kwamba, heri yao wale wote wanaokufa katika Kristo Yesu. Matumaini ya Kikristo yawasaidie waamini kukabiliana na Fumbo la kifo kwa imani na matumaini na kwamba, hata ustaarabu wa watu wa kale umepitia katika fumbo hili na kwa hakika, ibada ya kifo ni sehemu ya vinasaba vya maisha ya binadamu. Ndugu msikilizaji wa Radio Vatican “Sacrum novendiale, Novendia” ni kipindi cha siku tisa za maombolezo kinachofuatia kifo cha Baba Mtakatifu na kuanza mara baada ya mazishi ya Khalifa wa Mtakatifu Petro na tarehe yake hupangwa na Baraza la Makardinali na maadhimisho haya yanafanyika kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican. Ni katika muktadha huu, Kardinali Pietro Parolin, aliyekuwa Katibu mkuu wa Vatican, Dominika tarehe 27 Aprili 2025 ameongoza Ibada ya Misa Takatifu, Siku ya pili ya Novendia, maalum kwa wafanyakazi pamoja na raia wanaoishi mjini Vatican. Kardinali Parolin katika mahubiri yake amegusia kuhusu: Majonzi makubwa katika kipindi hiki cha maombolezo ya Baba Mtakatifu Francisko, lakini jambo la msingi ni furaha ya Pasaka; changamoto mamboleo katika maisha ya vijana, lakini wanapaswa kujikita katika upendo ambao hustahimili yote. Upendo wenye huruma ni kiini cha mafundisho ya Baba Mtakatifu Francisko, chemchemi ya imani, matumaini na mapendo na kwamba, Kanisa ni chombo na shuhuda wa huruma ya Mungu.
Kardinali Baldassare Reina, maarufu kama “Baldo”, Makamu Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Roma, Jumatatu jioni tarehe 28 Aprili 2025 akiwa ameungana na waamini wa Jimbo kuu la Roma, ameadhimisha Ibada ya Misa Takatifu, Siku ya Tatu ya Novendia. Katika mahubiri yake amegusia majonzi makubwa kwa watu wa Mungu Jimbo kuu la Roma ambao wanaomboleza kwa kuondokewa na Mchungaji wao mkuu, sasa wamekuwa kama kondoo wasiokuwa na mchungaji, huyu ni mchungaji aliyewapenda sana kondoo wake, lakini wakumbuke kwamba, Kristo Yesu ndiye mchungaji wa kweli, aliyeleta mageuzi katika historia ya ukombozi wa mwanadamu, anatambua uzito wa mchakato wa uinjilishaji wa kina unaogusa mahitaji msingi ya binadamu. Kipindi hiki cha majonzi ni muda muafaka wa kupyaisha imani, matumaini na mapendo kwa Kristo Yesu na Kanisa lake, kwani maisha yana nguvu zaidi ya kifo.
Kardinali Mauro Gambetti, O.F.M. Conv., Makamu Askofu mkuu mjini Vatican, akiwa ameungana na wahudumu wa Makanisa makuu Jimbo kuu la Roma, Jumanne jioni tarehe 29 Aprili 2025 ameadhimisha Ibada ya Misa Takatifu kwa ajili ya kumwombea Hayati Baba Mtakatifu Francisko. Katika mahubiri yake, Kardinali Gambetti anasema, Mama Kanisa anasadiki na kufundisha kwamba, toka huko, Kristo Yesu atakuja kuwahukumu wazima na wafu na Ufalme wake hautakuwa na mwisho. Yeye ni Bwana wa ulimwengu na wa historia. Ndani yake historia ya mwanadamu na pia kazi nzima ya uumbaji hujumlishwa na kutimilizwa kwa namna iliyo bora kabisa. Ukombozi ni chemchemi ya mamlaka ya Kristo Yesu ambayo anayatekeleza kwa nguvu ya Roho Mtakatifu juu ya Kanisa. Manabii na hatimaye, Yohane Mbatizaji alitangaza katika mafundisho yake kuhusu hukumu ya siku ya mwisho. Hapo matendo ya kila mmoja yatafunuliwa pamoja na siri za nyoyo za watu. Kumbe, huu ni wakati muafaka wa kutumia vyema neema ya Mungu inayomwilishwa katika matendo ya huruma na mapendo kwani hiki ndicho kitakachokuwa ni kipimo Siku ya hukumu ya mwisho.
Kardinali Leonardo Sandri, Mwenyekiti Mstaafu wa Baraza la Kipapa kwa ajili ya Makanisa ya Mashariki ambaye pia ni Makamu wa Dekano wa Baraza la Makardinali, tarehe 30 Aprili 2025 ameongoza Ibada ya Misa Takatifu kwa ajili ya maombolezo ya Hayati Baba Mtakatifu Francisko kwa wahudumu wa Kikanisa cha Kipapa. Katika mahubiri yake anasema, Fumbo la Pasaka ni utimilifu wa Fumbo la Umwilisho kwa ajili ya ukombozi wa mwanadamu kutoka katika lindi la dhambi na mauti! Kwa njia ya mateso, kifo na ufufuko wa Kristo Yesu, Mwenyezi Mungu amewakirimia wanadamu dunia mpya inayoambata wokovu ulioletwa na Kristo Yesu. Huu ndio mwanga unaowaangaza watakatifu na mashuhuda wa imani walioenea sehemu mbalimbali za dunia. Fumbo la Pasaka ni sababu na kiini cha imani, furaha na matumaini ya Wakristo hapa duniani kwani kwa njia ya mateso, kifo na ufufuko wake amemkomboa mwanadamu kutoka katika lindi la dhambi na mauti na kuwakirimia maisha ya uzima wa milele, mwaliko wa kudumisha upendo.
Kardinali Víctor Manuel Fernández, Mwenyekiti Mstaafu wa Baraza la Kipapa la Mafundisho Tanzu ya Kanisa, Mei Mosi, 2025 amewaongoza wafanyakazi wa Sekretarieti kuu ya Vatican katika Ibada ya Misa ya Maombolezo ya kifo cha Hayati Baba Mtakatifu Francisko: Ufufuko wa Kristo Yesu kutoka wafu; ni kilele cha ukweli wa imani katika Kristo Mfufuka; Ni ufunuo wa Uungu wa Kristo Yesu unaowapatia waamini maisha ya uzima mpya na hivyo kuhesabiwa haki pamoja na kufanywa wana wateule wa Mungu. Ufufuko wa Kristo ni msingi wa ufufuko wa miili na uzima wa milele ijayo! Ndiyo maana Pasaka ni Sherehe kubwa katika Kanisa. Hii ni Sherehe ya upendo, huruma na msamaha wa Baba wa milele unaofumbatwa katika Msalaba, chemchemi ya matumaini. Hayati Baba Mtakatifu Francisko alikazia: Utu, heshima, haki ya wafanyakazi na haki ya watu wasiokuwa na fursa za ajira. Familia ya Mungu inakumbushwa kwamba, utu, heshima na haki msingi za wafanyakazi zinapaswa kulindwa na kudumishwa, kwani ni sehemu muhimu sana ya mchakato wa maendeleo endelevu ya binadamu na jamii katika ujumla wake. Kazi ndicho kipimo cha utu wa mtu, mwenye mahusiano na binadamu wengine. Lengo la kazi ni kumsaidia mwanadamu na sio mwanadamu ageuke kuwa mtumwa wa kazi. Mahusiano yake na mwanadamu mwingine yasigeuke kuwa ni chukizo mbele ya Mungu, badala ya kuwa furaha, faraja na utimilifu wa utu wa mtu mwenyewe! Kwa ufupi kabisa, haki msingi za binadamu zinafumbatwa katika utu na heshima ya kila mwanadamu. Kazi ni utimilifu wa utu wa mwanadamu na inapaswa kuheshimiwa kwa kuzingatia pia utu wa mfanyakazi. Hakuna umaskini mkubwa katika jamii kama ukosefu wa fursa za ajira, utu na heshima ya wafanyakazi, wanaojisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya familia zao.
Baba Mtakatifu Francisko anawakumbusha waamini kwamba wanaitwa kuwahudumia watu walioko kwenye hatari za aina mbalimbali hapa duniani. Lakini muundo wa sasa, pamoja na msisitizo wake wa mafanikio na kujitegemea, hauonekani kuwa wenye kupendelea uwekezaji katika juhudi za kuwasaidia wale wanaokwenda taratibu, walio wanyonge au wasiokuwa na vipaji vikubwa ili wawe na fursa katika maisha. Rej. Evangelii gaudium, 209. Utu, heshima na haki msingi ni kwa ajili ya watu wote. Hayati Baba Mtakatifu Francisko ni mfano wa wafanyakazi bora, aliyejisadaka bila ya kujibakiza ili kutekeleza dhamana na wajibu wake hata dakika ya mwisho wa maisha yake, akathubutu kwenda kuwatembelea wafungwa. Hayati Baba Mtakatifu Francisko ni kiongozi ambaye hakupendelea kujipatia likizo, kwake kazi ilikuwa ni utimilifu wa maisha na utume wake, kama kielelezo cha upendo angavu wa Mungu, kwa hakika ajilitahidi kuishi kwa ajili ya wengine, changamoto na mwaliko wa kuhakikisha kwamba, utu, heshima, haki msingi na fursa za ajira zinapatikana kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi, ili kuwajengea watu wa Mungu matumaini ya leo na kesho iliyo bora zaidi. Wafanyakazi wa Sekretarieti kuu ya Vatican watambue kwamba, kazi ni sehemu ya mchakato wa ukomavu na utakatifu wa maisha yao. Baba Mtakatifu Francisko alikuwa na Ibada kubwa kwa Mtakatifu Yosefu aliyemfundisha Kristo Yesu stadi za maisha sanjari na kuitegemeza Familia Takatifu ya Nazareti.
Kardinali Claudio Gugerotti, aliyekuwa Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa kwa ajili ya Makanisa ya Mashariki, Ijumaa tarehe 2 Mei 2025 amewaongoza waamini kutoka Makanisa ya Mashariki katika Ibada ya maombolezo ya kifo cha Hayati Baba Mtakatifu Francisko. Katika mahubiri yake amekazia kuhusu imani Mateso, kifo na ufufuko wa Kristo Yesu kuwa ni kiini cha imani ya Kanisa, kwani ni matendo yanayoonesha ushindi wa Kristo Yesu dhidi ya dhambi na mauti na kwa njia hii, Kristo Yesu anawafungulia waamini njia ya maisha mapya. Kwa kuzaliwa upya katika Sakramenti ya Ubatizo; waamini wanapokea mapaji ya Roho Mtakatifu na hivyo kufanyika waana wateule wa Mungu. Kwa njia hii, Mwenyezi Mungu anakuwa ni Baba yao! Kazi ya uumbaji ni kati ya tema ambazo Hayati Baba Mtakatifu Francisko alizipatia uzito wa hali ya juu katika maisha na utume wake kama Khalifa wa Mtakatifu Petro, changamoto na mwaliko kwa watu wa Mungu kulinda na kutunza mazingira nyumba ya wote, kuachana na chuki, uhasama na vita ili kujikita katika ujenzi wa jamii inayosimikwa katika haki, amani na mshikamano wa udugu wa kibinadamu. Kwa Fumbo la Umwilisho sanjari na Ujio wa Roho Mtakatifu, unaowafanya waamini kujisikia kwamba wanapendwa na kuthaminiwa na Mungu Baba Mwenyezi, anawasikiliza kwa umakini mkubwa, mwaliko kwa waamini kuzama katika undani wao, ili kujisikia kwamba, kweli wanapendwa na kuthaminiwa na Mungu Baba Mwenyezi. Hayati Baba Mtakatifu Francisko anawahimiza waamini kuwa ni vyombo vya haki, amani na upatanisho, na hivyo kuendelea kuwa ni mashuhuda wa mateso, kifo na ufufuko wa Kristo Yesu kwa wafu. Makanisa ya Mashariki ni ushuhuda wa umoja na utofauti wa Kanisa Katoliki; amana na utajiri wa Mama Kanisa.
Waamini wa Makanisa ya Mashariki kwa miaka mingi wamekuwa wakinyanyaswa na kudhulumiwa, na hawa ndio ambao ni mashuhuda wa imani kama watakatifu na wafiadini. Hayati Baba Mtakatifu Francisko ana wataka waamini kuheshimu, kuthamini na kudumisha umoja katika tofauti zao msingi, daima wakiendelea kujikita katika huruma ya Mungu inayofumbatwa katika mateso, kifo na ufufuko wa Kristo Yesu kutoka kwa wafu. Kanisa la Mashariki linamshukuru Baba Mtakatifu Francisko kwa kumtangaza Mtakatifu Gregori wa Narek kuwa Mwalimu wa Kanisa.Mtakatifu huyu alikuwa ni Mtawa, aliyezaliwa huko mjini Andzevatsik, wakati huo ukijulikana kama Armenia ambayo ndiyo nchi ya Uturuki kwa sasa. Ni mtawa na mwanataalimungu mahiri, aliyejipambanua kwa maandishi na mtunga mashairi maafuru; alikuwa mwaminifu na mtiifu kwa Mapokeo ya Mama Kanisa, akaonesha bidii na heshima kubwa kwa Bikira Maria, Mama wa Mungu. Inasadikiwa kwamba, Bikira Maria alimtokea Mtakatifu Gregori. Kati ya kazi zake kuu ambazo wengi wanazikumbuka ni kuhusu "Hotuba ya Masifu kwa Bikira Maria" pamoja na Sala 80 ambazo zilipewa jina, "Kutoka katika undani wa moyo wangu, majadiliano na Mama wa Mungu." Sehemu hii ya sala inaonesha jinsi ambavyo Mtakatifu Gregori baada ya kukabiliwa na magumu pamoja na machungu ya maisha yaliyomkatisha tamaa, mwishoni alifanikiwa kuona upendo kutoka kwa Bikira Maria, akatambua msaada wake wa daima. Gregori wa Narek alifariki dunia kunako mwaka 1005. Kanisa nchini Armenia kwa miaka mingi lilikuwa linamtambua kuwa ni Mwalimu wa Kanisa kutokana na utakatifu uliojikita katika mafundisho makuu ya imani kama anavyokumbukwa katika Orodha ya Watakatifu wa Kanisa, tarehe 27 Februari.