Moshi mweusi:Hakuna Papa aliyechaguliwa baada ya kura ya kwanza ya Mkutano Mkuu wa kumchagua Papa wa 267
Vatican News
Moshi mweusi uliibuka kutoka kwenye bomba la moshi juu ya kikanisa cha Sistine saa 3:00, Jumatano usiku tarehe 7 Mei 2025, kuashiria kwamba kura ya kwanza imepigwa kwenye mkutano huo na imekamilika bila kuchaguliwa kwa Papa. Kwa mujibu wa taarifa ni kwamba takriban watu 45,000 walikuwa wamekusanyika katika uwanja wa Mtakatifu Petro wakisubiri tangazo hilo.
Miongoni mwao alikuwa Shemasi Nicholas Nkoronko kutoka Tanzania. Akizungumza na Vatican News, alisema: "Jukumu letu hapa ni kusali na kuungana na Wakristo wengine, Wakatoliki wengine, kumwomba Roho Mtakatifu aongoze mchakato mzima." "Popote anapotoka Papa mpya", Shemasi Nkoronko alisisitiza, "iwe ni Afrika, Asia, Amerika, tunachohitaji tunahitaji Papa Mtakatifu. Tunahitaji Papa ambaye ataliongoza Kanisa na atakuwa mchungaji wa Kanisa."
Ratiba ya Alhamisi
Kesho asubuhi, Alhamisi tarehe 8 Mei 2025, ratiba kama ilivyopangwa, Makardinali wapiga kura watakusanyika kabla ya tarehe 2, katika Jumba la Kitume, ili kuadhimisha Misa na Masifu ya Asubuhi katika kikanisa cha Pauline.
Baadaye wataingia saa 3:15 katika kikanisa cha Sistine ili kusali masifu ya tatu na kisha kuendelea kupiga kura. Chakula cha mchana kinatarajiwa kuwa karibu saa 6:30 mchana huko Mtakatifu Marta, na kuondoka huko saa 9:45 alasiri hadi Jumba la Kitume, kisha saa 10:30 jioni,masaa ya Ulaya ni kuingia tena katika kikanisa cha Sistine na kura mbili zaidi na mwisho zinatarajiwa ambapo (karibu saa 1:30) jioni maadhimisho ya masifu ya jioni yatafanyika.
Kuna moshi mara mbili uliopangwa kwa siku tofauti: mmoja mwishoni mwa asubuhi, na mmoja jioni, yaani, mwisho wa kura za asubuhi na alasiri.