Kard.Makrickas:Pamoja na Francisko kuna mguso na ukaribu wa huruma ya Mungu!
Na Angella Rwezaula – Vatican.
Kwa muda wa miaka kumi na miwili, Kanisa zima, kwa njia tofauti, kwa njia ya ishara muhimu za Baba Mtakatifu Francisko, maneno yake ya busara na tabasamu lake la kung’aa limeweza kuonja ukaribu, huruma na upole wa Mungu. Na mtiririko usio na mwisho wa watu ambao kwa karibu mwezi mzima katika Kanisa Kuu la Mtakatifu Maria Mkuu wameonesha shukrani kwa kila kitu ambacho Papa Francisko ametuacha, huku wakisali kwenye kaburi lake, wanafanya kwa ishara zake hizo, kwa maneno yake hayo, kwa tabasamu lake hilo. Lakini zaidi ya yote kwa sababu maisha yake daima yaliunganishwa na yale ya Yesu: kama tawi lililounganishwa na mzabibu. Hayo na mengine ndiyo maneno ya kumbukumbu ya kusisimua ya Kardinali Roland Makrickas, Mkuu Mwenza wa Kanisa kuu la Mtakatifu Maria Mkuu wakati wa mahubiri ya Misa Takatifu kwa ajili ya Baba Mtakatifu Francisko, iliyoongozwa kwenye Kanisa Kuu hilo mwezi mmoja baada ya kifo chake kilichotokea tarehe 21 Mei 2025 siku ya Pili ya Pasaka Takatifu.
Muungano wa kina na Yesu
Kardinali Roland akidadavua Injili ya siku iliyosomwa tarehe 21 Mei 2025 alisema kuwa Injili ya leo Yesu anatumia picha ya kaaida sana, ambayo ilikuwa machoni pa wote ile ya “ mzabibi na matawi.”Yesu anatuambia maneno ya kugusa sana: “Kaeni ndani yangu nami ndani yenu, kaeni katika pendo langu...”“Tawi haliwezi kuzaa peke yake, lisipokaa ndani ya mzabibu, mimi ni mzabibu, ninyi ni matawi, akaaye ndani yangu nami ndani yake, huzaa sana; kwa maana pasipo mimi ninyi hamwezi kufanya neno lo lote.” Maisha ya muungano wa kina na Yesu ni uhakika kwamba tunaweza kutambua mapenzi yake, yaani, mema bora kwa roho zetu na kwa ulimwengu wote. “Pasipo mimi ninyi hamwezi kufanya neno lo lote”: hivi ndivyo Yesu anatuambia, kwa upendo mkuu lakini pia kwa uwazi mkuu.
Mfano wa watakatifu wengi
Wakati fulani tunaweza kuwa na hisia, udanganyifu au kishawishi cha kufikiri kwamba tunaweza kufanya mambo mengi peke yetu, hata bila Mungu. Yesu hakusema maneno yasiyo na maana, yuko wazi sana na maneno yake lazima yachukuliwe kwa uzito, kwa sababu ndani yake kuna ukweli na sio udanganyifu. Bila mimi huwezi kufanya chochote, lakini pamoja nami unaweza kufanya mengi, unaweza kufanya kila kitu. Tunao mfano wa Watakatifu wengi, ambao waliungana na Kristo waliweza kufanya mambo makuu na kulitolea Kanisa na wanadamu wote matunda mazuri ya mema. Neno la Mungu hutusaidia kuelewa na kuishi uhusiano wetu na Mungu: matawi yaliyounganishwa na mzabibu. Pia inatusaidia kuelewa na kuishi uhusiano wetu na wengine, kwa sababu sisi sote ni sehemu ya shamba moja la mizabibu la Bwana, shamba la mizabibu linalotunzwa na Bwana na Roho wake.
Papa Francisko:Mtawa,Askofu, Kardinali na Papa
Kumwamini Yesu na kupendana: hii ni kuishi amri yake ya kukaa ndani ya Mungu. Hebu tufikirie watu wengi wa ajabu, watakatifu wakuu na watakatifu wa maisha ya kawaida. Ushuhuda wa watu wengi ambao, hata baada ya uzoefu mgumu sana, huja karibu na Bwana na kufanya mema mengi daima ni wa kushangaza. Mnaweza kufanya mengi na kuzalisha matunda mengi, mkikaa katika muungano na Bwana wetu. Hata huduma rahisi na ya unyenyekevu ina thamani kubwa machoni pa Mungu. Badala yake, kila wakati unapotoa upendeleo kwa mipango yako mwenyewe ya kibinadamu, unaachwa mikono mitupu. Kardinali Roland alisema kuwa kwetu sisi leo ni siku muhimu sana kwa sababu tunakumbuka kifo cha mcha Mungu cha Papa Francisko, hasa mwezi mmoja uliopita. Hasa katika kumbukumbu yake maneno haya ya Yesu yanakuwa hai na dhahiri zaidi mbele yetu. Baba Mtakatifu Francisko, baada ya maisha marefu ya huduma kwa watu wa Mungu, kama Padre, Mjesuit mtawa, Askofu na Papa, amepita katika utimilifu wa maisha na sasa mwili wake, kwa kukumbatiwa mara kwa mara na upendo wa Waroma na waaminifu kutoka sehemu zote za dunia, unatulia ndani ya Kanisa Kuu la Maria. Roho katika nyumba ya Baba na mwili katika nyumba ya Maria. Jinsi gani ilivyo nzuri! Maisha na utume wa Baba Mtakatifu Francisko umeleta na unaendelea kuleta matunda mengi kwa Kanisa, kwa sababu yalikuwa ni maisha ambayo daima yameunganishwa na yale ya Yesu: kama tawi lililounganishwa na mzabibu.
Maneno na ishara za Baba Mtakatifu Francisko
Maneno na ishara za Baba Mtakatifu Francisko zimeingia kwa undani ndani ya mioyo ya waamini kwa sababu kweli alikuwa mmoja na Kristo, bila kutenganishwa, katika furaha na maumivu - kama tawi la mzabibu. Kila siku yake ilianza na saa ya kuabudu, na adhimisho la Ekaristi na sala ya kibinafsi. Alianza pia kwa kukabidhi kila siku ulinzi wa mama wa Maria, Mama wa Mungu. Kwa muda wa miaka kumi na miwili, Kanisa zima, kwa njia tofauti, kupitia ishara zake muhimu, maneno yake ya busara na tabasamu lake la kung'aa limeweza kupata uzoefu wa ukaribu, huruma na huruma ya Mungu. Kwa muda wa mwezi mmoja tumekuwa tukisukumwa na mtiririko usio na mwisho wa watu ambao, kwa subira, wanangoja kuingia hapa kwa sababu wanataka kweli kuonyesha shukrani zao kwa kila kitu ambacho Papa Francisko amebakisha.
Ishara zake
Kwa ishara zake, kwa maneno yake, kwa tabasamu lake. Wanaunganishwa naye na kwa njia yake na Kristo kwa sababu Baba Mtakatifu Francisko ameweza kumfanya Kristo awepo kwa kila mtu, akimshuhudia kila siku, hadi saa yake ya mwisho. Umoja na Papa, kuunganishwa na Kristo. Kama matawi yaliyo na mzabibu. Usiku huu tunamwomba Mama wa Mungu, Salus Populi Romani, atusaidie kila mmoja wetu kuunganishwa na Bwana wetu, kwa unyenyekevu wa dhati na ukarimu katika huduma yake takatifu. Tunamwombea mwanga wa milele Baba Mtakatifu Francisko, mtumishi mnyenyekevu, mwenye hekima na mwaminifu wa Injili na Baba Mtakatifu mpya Leo XIV, aweze kudumu katika huduma ya Mtume wa Mtakatifu Petro. Amina.