Mwadhama Kardinali Robert Francis Prevost, Baba Mtakatifu Leo wa XIV
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Mwadhama Kardinali Robert Francis Prevost, wa Shirika la Mtakatifu Augustino, O.S.A. ndiye Baba Mtakatifu, wa 267 aliyechaguliwa na Baraza la Makardinali katika mkutano wa uchaguzi wa Khalifa wa Mtakatifu Petro, Askofu mkuu wa Roma, kama alivyotangazwa na Kardinali Shemasi Dominique Mamberti, Alhamisi tarehe 8 Mei 2025 na amechagua jina la Leo wa XIV. Mara vikosi vya ulinzi na usalama vikajitokeza kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro, huku umati mkubwa wa watu wa Mungu wakiendelea kusheheni katika Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican. Baba Mtakatifu Robert Francis Prevost, wa Shirika la Mtakatifu Augustino, O.S.A., Leo wa XIV, alizaliwa tarehe 14 Septemba 1955, Jimbo kuu la Chicago, Illinois, nchini Marekani. Tarehe 29 Agosti 1981 akaweka nadhiri za daima kwenye Shirika la Mtakatifu Augustino, O.S.A. Tarehe 19 Juni 1982 akapewa Daraja Takatifu ya Upadre. Tarehe 14 Septemba 2001 akachaguliwa kuwa ni Mkuu wa Shirika la Mtakatifu Augustino hadi tarehe 4 Septemba 2013. Tarehe 26 Septemba 2015, Hayati Baba Mtakatifu Francisko akamteuwa kuwa Askofu wa Jimbo Katoliki la Chiclayo, nchini Perù.
Tarehe 30 Januari 2023 Baba Mtakatifu Francisko akamteuwa kuwa Rais wa Baraza la Kipapa kwa Ajili ya Maaskofu na Rais wa Tume ya Kipapa kwa ajili ya Amerika ya Kusini na kumpandisha cheo na hivyo kuwa ni Askofu mkuu. Tarehe 12 Aprili 2023 akasimikwa rasmi kuwa Rais wa Baraza la Kipapa kwa Ajili ya Maaskofu na Rais wa Tume ya Kipapa kwa ajili ya Amerika ya Kusini na hivyo kuchukua nafasi ya Kardinali Marc Armand Ouellet, aliyekuwa ni Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa kwa ajili ya Maaskofu. Tarehe 30 Septemba 2023 akasimikwa kuwa Kardinali. Kardinali Robert Francis Prevost katika mahojiano maalum na Vatican News anazungumzia kuhusu: Dhamana na wajibu wa Maaskofu kwanza kabisa ni kutangaza na kushuhudia uzuri na furaha ya kukutana na hatimaye kumfahamu Kristo Yesu; mchakato wa ujenzi wa umoja na Khalifa wa Mtakatifu Petro, Askofu na mchakato wa Sinodi na kwamba, Askofu anapaswa kuwa ni mratibu na msimamizi mwaminifu wa rasilimali na mali ya Kanisa. Kardinali Robert Francis Prevost anasema, dhamana na utume wake ni kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu kwa watu wa Mataifa. Kwa wakati huu, amepewa dhamana ya kufanya kazi kwa karibu zaidi na Baba Mtakatifu katika Baraza la Kipapa kwa ajili ya Maaskofu. Daima amekuwa tayari kujisadaka kwa ajili ya utume na maisha ya Kanisa, kama ilivyokuwa nchini Perù, kwa kufanya utume wake kwa muda wa miaka 8 kama Askofu na Miaka 30 kama mmisionari.
Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican umelipuka kwa furaha baada ya moshi mweupe kutokea na kengele kuanza kupigwa kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Petro. Huu ni uchaguzi ambao umekwenda haraka sana kuliko hata ilivyotarajiwa na wengi. Kwa kweli watu wa Mungu wamesali na kufunga, ili Kanisa liweze kumpata Baba Mtakatifu mpya. Kama vile Mtakatifu Petro na wale Mitume walivyounganika, kwa agizo la Kristo Yesu, katika urika mmoja tu, kwa jinsi ilivyo sawa, Askofu mkuu wa Roma aliye Khalifa wa Mtakatifu Petro, na Maaskofu walio waandamizi wa Mitume, wanaungana pamoja. Askofu wa Kanisa la Roma, ambaye katika yeye linadumu jukumu lililokabidhiwa na Bwana kwa Petro tu, mkuu wa Mitume, linalotakiwa kurithishwa kwa waandamizi wake, ni mkuu wa urika wa Maaskofu, Wakili wa Kristo Yesu na Mchungaji mkuu wa Kanisa lote zima hapa duniani; hivyo kwa nguvu ya jukumu lake anayo mamlaka ya kawaida ya juu kabisa, kamili, inayojitegemea kwa uhuru. Rej. Kanuni 330-332. Baba Mtakatifu mpya, lazima awe ni mtu anayeonesha uwepo na ukaribu wake kwa watu wa Mungu; awe ni daraja na mwongozo katika mchakato wa ujenzi wa umoja na ushirika kati ya watu wa Mungu. Ni kiongozi anayepaswa kuwa ni shuhuda wa imani, atakayesimama kidete kulinda na kutetea: haki, amani na utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote; tayari kuchochea tunu msingi za maisha ya ndoa na familia; miito mitakatifu ndani ya Kanisa; elimu, malezi na majiundo makini kwa vijana wa kizazi kipya.
Mwenyezi Mungu anasema: “Nitajiinulia kuhani mwaminifu atakayefanya sawasawa na mambo yote niliyo nayo katika moyo wangu, na katika nia yangu; nami nitamjengea nyumba iliyo imara; naye atakwenda mbele yangu siku zote.” Katika Kolekta Mama Kanisa anasali akisema, “Ee Mungu, uliye mchungaji wa milele, unaliongoza kundi lako kwa ulinzi wa daima. Ulijalie Kanisa lako, kwa wema wako mkuu, mchungaji ambaye atakupendeza kwa utakatifu na kutufaidia sisi kwa kutuchunga kwa bidii. Kwa njia ya Bwana wetu Yesu Kristo Mwanao, anayeishi na kutawala nawe katika umoja wa Roho Mtakatifu, Mungu, milele na milele.” Katika Sala ya kuombea dhabihu, Mama Kanisa anasali kwa kusema, “Ee Bwana, wingi wa rehema yako ushuke juu yetu, ili kwa sadaka takatifu tunayokutolea kwa heshima utujalie tufurahie kupata mchungaji atakayekupendeza wewe mtukufu katika kulisimamia Kanisa takatifu. Kwa njia ya Kristo Bwana wetu.” Mama Kanisa anamwomba Mwenyezi Mungu, ili aweze kulijalia Kanisa Mchungaji mkuu, atakayewafundisha kwa fadhila zake watu wa Taifa la Mungu, kwa kuwamiminia mioyoni mwao ukweli wa Kiinjili.
Baraza la Makardinali katika mikutano yake elekezi kama sehemu ya maandalizi ya uchaguzi wa Khalifa wa Mtakatifu Petro “Conclave” liliwaalika watu wa Mungu, kukiishi kipindi hiki cha neema na utambuzi wa maisha ya kiroho sanjari na kusikiliza mapenzi ya Mungu. Makardinali wakitambua ukubwa na unyeti wa kazi na dhamana iliyoko mbele yao, wanatambua kwamba, kuna haja ya kuungwa mkono na kusindikizwa na sala za waamini. Hii ndiyo nguvu ya kweli ambayo inakuza ndani ya Kanisa umoja wa viungo vyote vya Fumbo la Mwili wa Kristo yaani Kanisa. Rej. 1Kor 12: 12. Baraza la Makardinali lilitambua uzito wa kazi kubwa iliyokuwa mbele yao kwa wakati huu, kwanza kabisa Makardinali wenyewe walipenda kujinyenyekesha, ili waweze kuwa ni vyombo vya hekima isiyokuwa na kikomo na kwa maongozi ya Baba yao wa milele na kwa unyenyekevu wa utendaji wa Roho Mtakatifu. Makardinali wanakaza kusema, kwa hakika Roho Mtakatifu ndiye Mhusika mkuu wa maisha ya watu wa Mungu, changamoto na mwaliko wa kumsikiliza na kuitikia kile ambacho anasema Roho Mtakatifu kwa Mama Kanisa. Rej. Ufu 3:6.