Diplomasia ya Baba Mtakatifu Leo XIV: Amani, Haki na Ukweli!
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Diplomasia ya Vatican na Kanisa Katoliki katika ujumla wake, inatoa kipaumbele cha pekee kwa uhuru wa kidini, utu na heshima ya binadamu aliyeumbwa kwa sura na mfano wa Mungu, bila kusahau utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote. Hii ndiyo dhamana inayotekelezwa na Vatican katika medani mbalimbali za Kimataifa. Kutambua na kuheshimu haki msingi za binadamu ni hatua muhimu sana ya maendeleo fungamani ya binadamu, kwani mizizi ya haki za binadamu inafumbatwa katika hadhi, heshima na utu wa binadamu aliyeumbwa kwa sura na mfano wa Mungu. Hizi ni haki za wote zisizoweza kukiukwa wala kutenguliwa. Ni za binadamu wote bila kujali: wakati, mahali au mhusika. Haki msingi za binadamu zinapaswa kulindwa na kudumishwa na wote. Haki ya kwanza kabisa ni uhai tangu pale mtoto anapotungwa mimba tumboni mwa mama yake hadi pale anapofariki dunia kadiri ya mpango wa Mungu. Mkazo umewekwa katika haki ya uhuru wa kidini inayofafanuliwa katika uhuru wa kuabudu. Hiki ni kiini cha haki msingi kinachofumbata haki nyingine zote. Kuheshimu na kuthamini haki hii ni alama ya maendeleo halisi ya binadamu katika medani mbalimbali za maisha. Haki inakwenda sanjari na wajibu! Mama Kanisa anakazia kwa namna ya pekee kabisa umuhimu wa kuheshimu haki msingi za binadamu, kichocheo muhimu sana cha amani na utulivu miongoni mwa binadamu. Kanisa linapenda kusimama kidete: kulinda na kudumisha haki na amani sehemu mbalimbali za dunia kwa njia ya mwanga na chachu ya tunu msingi za Kiinjili! Uhuru wa kidini ni sehemu muhimu sana ya Tamko la Haki Msingi za Binadamu lililopitishwa na Umoja wa Mataifa kunako mwaka 1948.
Tangu mwanzo wa utume wake kama Khalifa wa Mtakatifu Petro, Baba Mtakatifu Leo XIV, Ijumaa tarehe 16 Mei 2025, kwa mara ya kwanza amekutana na kuzungumza na wanadiplomasia pamoja na wawakilishi wa Mashirika ya Kimataifa mjini Vatican. Ametumia fursa hii kuzishukuru nchi mbalimbali zilizotuma salam za rambirambi kutokana na kifo cha Baba Mtakatifu Francisko pamoja na kumpongeza baada ya kuchaguliwa kuliongoza Kanisa Katoliki.Hizi ni salam na matashi mema kutoka hata katika nchi ambazo hazina uhusiano wa kidiplomasia na Vatican. Amesema, diplomasia ya Khalifa wa Mtakatifu Petro na Vatican katika ujumla wake inasimikwa katika mchakato wa sera na mipango yake ya shughuli za kichungaji, ambayo kamwe haitafuti upendeleo bali ni sehemu ya vinasaba vyake vya Uinjilishaji na huduma kwa binadamu. Diplomasia hii inapania pamoja na mambo mengine, kuondokana na mifumo yote isiyojali wala kuguswa na mahangaiko ya wengine; kwa kuamsha dhamiri nyofu, ili kusikiliza na kujibu kilio cha Maskini, Dunia Mama na wale wote waliotengwa na kusukumizwa pembezoni mwa jamii, pamoja na kuendelea kushughulikia changamoto mamboleo kuanzia ulinzi na utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote pamoja na teknolojia ya akili unde.
Hii imekuwa ni fursa kwa Baba Mtakatifu Leo XIV kujikita zaidi na zaidi katika mambo makuu matatu: Ukweli, Haki na Amani kama uzoefu na mang’amuzi ya kuweza kukutana na watu pamoja na tamaduni mbalimbali. Katika maisha na utume wake kama Khalifa wa Mtakatifu Petro anapania kuimarisha majadiliano katika ukweli na uwazi; kuendelea kufahamu amana na utajiri wa nchi mbalimbali na hivyo kupata fursa ya kuweza kuwaimarisha ndugu zake katika imani sanjari na kuendelea kujenga madaraja ya kuwakutanisha watu. Amekazia: Amani, Haki na Ukweli kama nguzo muhimu za shughuli za kimisionari zinazotekelezwa na Mama Kanisa sehemu mbalimbali za dunia na kama sehemu ya diplomasia ya Vatican. Amesema, amani si ukosefu wa vita, bali ni sehemu ya vinasaba vya maisha ya mwanadamu na kwamba, amani inapokosekana hapo migogoro, vita na kinzani huibuka. Amani ni zawadi kutoka kwa Kristo Yesu kwa wafuasi wake: “Amani yangu nawapa.” Yn 14:27. Amani ni changamoto ya kitamaduni na kidini na kwamba, amani ya kweli inajengwa kutoka katika sakafu ya moyo wa mwanadamu kwa kutupilia mbali kiburi na jeuri; tabia ya kutaka kulipiza kisasi pamoja na kuwa waangalifu wa kuchagua maneno ya kuzungumza, kwani maneno yana nguvu ya kuua kuliko hata silaha. Baba Mtakatifu Leo XIV anasema, jambo la pili ni haki na kwamba, maisha na utume wake kama Khalifa wa Mtakatifu Petro anapenda kujikita katika Mafundisho Jamii ya Kanisa kama yalivyoasisiwa na Papa Leo XIII katika Waraka wake wa Kitume “Rerum novarum” yaani “Mambo mapya.” Kanisa Katoliki lina amana na utajiri mkubwa wa Mafundisho Jamii ya Kanisa yanayopata chimbuko lake katika Waraka wa Kichungaji wa Papa Leo XIII; Mambo Mapya; “Rerum novarum.” Alisema, kazi ni utimilifu wa utu na heshima ya binadamu, ina thamani na heshima yake ya asili.
Papa Leo XIII aligusia haki msingi za wafanyakazi, mshahara wa haki na wajibu wa wafanyakazi; Umiliki binafsi wa mali; wajibu wa Serikali ni pamoja na kuhakikisha haki, sanjari na kuwalinda wanyonge ndani ya jamii; Kwa kukazia ustawi na maendeleo kwa ajili ya wote, lakini maskini wapewe kipaumbele cha kwanza. Kanuni ya auni inapaswa kuzingatiwa! Baba Mtakatifu Leo XIV anasema, Vatican itaendelea kusimama kidete kupaaza sauti za wanyonge, ili kuleta maboresho katika maisha na hivyo kuondokana na ukosefu wa haki msingi za binadamu. Kumbe kuna haja kwa viongozi wa Jumuiya ya Kimataifa kufanya kazi kwa amani sanjari na kudumisha amani duniani na hivyo kuondokana na kinzani pamoja na mipasuko. Hii ni changamoto kwa Serikali kuwekeza katika ujenzi wa misingi ya tunu bora ya maisha ya ndoa na familia yanayosimikwa katika uhusiano kati ya Bwana na Bibi. Watu wajikite katika kulinda, kutetea na kudumisha utu, heshima na haki msingi za binadamu, tangu pale mtoto anapotungwa mimba tumboni mwa mama yake hadi mauti inapomfika kadiri ya mapngo wa Mungu. Huu ni mwaliko pia wa kuwaheshimu na kuwathamini wagonjwa na wazee; watu wasiokuwa na kazi, raia pamoja na wakimbizi na wahamiaji. Baba Mtakatifu Leo XIV anasema, hata yeye ni mtoto wa wahamiaji. Katika historia ya maisha, mwanadamu anaweza kujikuta akiwa mgonjwa, amepata ajira au amekosa fursa za ajira; anaweza kujikuta akiwa anaishi katika nchi yake ya asili au ugenini, jambo la msingi ni utu, heshima na haki msingi za binadamu kadiri ya mpango na upendo wa Mungu.
Baba Mtakatifu Leo XIV anasema, amani na mahusiano ya kimataifa hayana budi kuzingatia malengo yake na kwamba, Kanisa linapenda kuwa ni chombo na shuhuda wa ukweli, ili kuwawezesha watu wa Mungu kukutana na Kristo Yesu. Ukweli ni changamoto inayowataka watu kujenga umoja, mshikamano na madaraja yanayowakutanisha watu. Ukweli uwasaidie watu kuiangalia changamoto ya wimbi kubwa la wakimbizi na wahamiaji; kuendelea kujikita katika kanuni, maadili na utu wema katika matumizi ya teknolojia ya akili unde pamoja na utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote. Hizi ni changamoto zinazohitaji majitoleo, ushirikiano na mshikamano wa watu wote, kwani si rahisi sana kwa mtu mmoja mmoja, kuweza kuzishughulikia.Baba Mtakatifu Leo XIV anasema ana anza maisha na utume wake kama Khalifa wa Mtakatifu Petro kati kati ya Maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 2025 ya Ukristo yanayonogeshwa na kauli mbiu “Peregrinantes in spem” yaani “Mahujaji wa matumaini.” Hiki ni kipindi cha toba, wongofu wa ndani pamoja na upyaisho wa maisha ya kiroho; ni mwaliko wa kujenga, kudumisha na kutangaza Injili ya amani; umoja na mshikamano, ili kuwawezesha watu wote wa Mungu kuishi katika ukweli, haki na amani. Ni matumaini ya Baba Mtakatifu Leo XIV kwamba, ukweli huu utajidhihirisha nchini Ukraine pamoja na Nchi Takatifu. Amewashukuru Mabalozi na wawakilishi wa Mashirika ya Kimataifa kwa kujenga na kudumisha madaraja yanayoziunganisha nchi zao na Vatican na hatimaye, akawapatia baraka zake za kitume.