杏MAP导航

Tafuta

Baraza la Makardinali linatambua kwamba, mchakato wa Uinjilishaji wa kina unaogusa mahitaji msingi ya binadamu: kiroho na kimwili kilikuwa ni kitovu cha “Magisterium” ya Hayati Papa Francisko. Baraza la Makardinali linatambua kwamba, mchakato wa Uinjilishaji wa kina unaogusa mahitaji msingi ya binadamu: kiroho na kimwili kilikuwa ni kitovu cha “Magisterium” ya Hayati Papa Francisko.  (ANSA)

Baraza la Makardinali: Vipaumbele Vya Mama Kanisa

Vipaumbele: kuendelea kujikita katika ujenzi wa umoja na ushirika wa Kanisa; kwa kuwekeza zaidi katika utume wa vijana na kwamba, waamini wanahimizwa kuwa ni vyombo na mashuhuda wa Habari Njema ya Wokovu. Makardinali wamegusia pia kashfa ya nyanyaso za kijinsia ndani ya Kanisa; kashfa ya masuala ya vitega uchumi kuwa ni madonda yanayohitaji uponyaji wa haraka na kwamba, Liturujia ya Kanisa; Ujenzi wa Kanisa la Kisinodi la Kimisionari ni muhimu!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baraza la Makardinali katika mikutano yake elekezi kama sehemu ya maandalizi ya uchaguzi wa Khalifa wa Mtakatifu Petro “Conclave” linawaalika watu wa Mungu, kukiishi kipindi hiki cha neema na utambuzi wa maisha ya kiroho sanjari na kusikiliza mapenzi ya Mungu. Makardinali wakitambua ukubwa na unyeti wa kazi na dhamana iliyoko mbele yao, wanatambua kwamba, kuna haja ya kuungwa mkono na kusindikizwa na sala za waamini. Hii ndiyo nguvu ya kweli ambayo inakuza ndani ya Kanisa umoja wa viungo vyote vya Fumbo la Mwili wa Kristo yaani Kanisa. Rej. 1Kor 12: 12. Baraza la Makardinali linatambua uzito wa kazi kubwa iliyoko mbele yao kwa wakati huu, kwanza kabisa Makardinali wenyewe wanapenda kujinyenyekesha, ili waweze kuwa ni vyombo vya hekima isiyokuwa na kikomo na kwa maongozi ya Baba yao wa milele na kwa unyenyekevu wa utendaji wa Roho Mtakatifu. Makardinali wanakaza kusema, kwa hakika Roho Mtakatifu ndiye Mhusika mkuu wa maisha ya watu wa Mungu, changamoto na mwaliko wa kumsikiliza na kuitikia kile ambacho anasema Roho Mtakatifu kwa Mama Kanisa. Rej. Ufu 3:6. Bikira Maria Mama wa Kanisa awasindikize kwa sala na kwa ulinzi na tunza yake ya Kimama.

Baraza la Makardinali Katika kikao chake cha nane na tisa
Baraza la Makardinali Katika kikao chake cha nane na tisa   (@VATICAN MEDIA)

Baraza la Makardinali linatambua kwamba, mchakato wa Uinjilishaji wa kina unaogusa mahitaji msingi ya binadamu: kiroho na kimwili kilikuwa ni kitovu cha “Magisterium” yaani Mamlaka fundishi ya Kanisa mintarafu Hayati Baba Mtakatifu Francisko kwa kuendelea kujikita katika ujenzi wa umoja na ushirika wa Kanisa; kwa Kanisa kuwekeza zaidi na zaidi katika utume wa vijana na kwamba, waamini wanahimizwa kuwa ni vyombo na mashuhuda wa Habari Njema ya Wokovu. Makardinali wamegusia pia kashfa ya nyanyaso za kijinsia ndani ya Kanisa; kashfa ya masuala ya vitega uchumi vya Vatican kuwa ni madonda yanayohitaji uponyaji wa haraka na kwamba, Liturujia ya Kanisa; Ujenzi wa Kanisa la Kisinodi la Kimisionari pamoja na utekelezaji wa Sheria za Kanisa ni mambo yanayopaswa kupewa msukumo wa pekee katika maisha na vipaumbele vya Kanisa katika mapambazuko ya Millenia ya Tatu ya Ukristo. Waamini watambue kwamba, Ekaristi Takatifu ni chanzo na kilele cha maisha na utume wa Kanisa na kwamba, huu ni ufunguo wa ujenzi wa Kanisa la Kimisionari. Huu ni mwendelezo wa Mamlaka fundishi ya Mababa wa Mtaguso wa Pili wa Vatican, Yohane Paulo II, Baba Mtakatifu Benedikto XVI na Hayati Baba Mtakatifu Francisko.

Baraza la Makardinali katika mkutano wake wa 8 na 9
Baraza la Makardinali katika mkutano wake wa 8 na 9   (@VATICAN MEDIA)

Kardinali Njue, Askofu mkuu mstaafu wa Jimbo kuu la Nairobi pamoja na Kardinali Antonio Cañizares Askofu mkuu mstaafu wa Jimbo kuu la Valencia, Hispania ni kati ya Makardinali wenye haki ya kupiga na kupigiwa kura, lakini kutokana na sababu zilizo nje ya uwezo wao hawataweza kushiriki katika uchaguzi wa Khalifa wa Mtakatifu Petro. Maadhimisho yote wakati wa uchaguzi wa Khalifa wa Mtakatifu Petro yatafanyika kwa lugha ya Kilatini. Makardinali wanaendelea kukazia umuhimu wa kutangaza na kushuhudia tunu msingi za Injili, Ujenzi wa Umoja wa Kanisa, Udugu wa kibinadamu na mshikamano wa dhati mambo msingi yaliyopewa upendeleo wa pekee na Hayati Baba Mtakatifu Francisko. Umoja na ushirikiano kati ya Sekretarieti kuu ya Vatican na Makanisa mahalia; dhamana na utume wa Sekretarieti kuu ya Vatican na Khalifa wa Mtakatifu Petro, Kanisa kama mragibishaji mkuu wa haki, amani na maridhiano; Elimu kama chemchemi ya matumaini na kwamba, Hayati Papa Francisko anasema, huruma ya Mungu ni chemchemi ya furaha ya kweli; msamaha unaowawezesha wafuasi wa Kristo kuwa ni vyombo na mashuhuda wa huruma ya Mungu na hatimaye, huruma ya Mungu ni faraja kubwa kwa wasioamini, wanaotaka kugusa Madonda Matakatifu, ili waweze kuamini kama ilivyokuwa kwa Mtume Toma! Lakini wawe tayari kugusa na kuganga madonda ya jirani zao kwa mafuta ya faraja na divai ya matumaini, tunda la Pasaka!

Uinjilishaji na utamadunisho ni chanda na pete
Uinjilishaji na utamadunisho ni chanda na pete   (VATICAN MEDIA Divisione Foto)

Ujenzi wa Kanisa la Kisinodi na Kimisionari, Urika wa Maaskofu; Majadiliano ya kidini na kiekumene sanjari na utume wa Kanisa katika mapambazuko ya Millenia ya tatu ya Ukristo ni kati ya tema zinazoendelea kujadiliwa na Baraza la Makardinali kwa wakati huu. Ukarabati wa dharura unakamilika tarehe 5 Mei 2025, kumbe, Makardinali na wahusika wakuu katika mchakato wa uchaguzi wa Khalifa wa Mtakatifu Petro wanaweza kuanzia kuingia, tarehe 5 na 6 Mei 2025 tayari kwa maadhimisho ya Ibada ya Misa Takatifu, Jumatano tarehe 7 Mei 2025 kwa ajili ya uchaguzi wa Khalifa wa Mtakatifu Petro: “Pro Eligendo Romano Pontifice.” Baraza la Makardinali katika kikao chake cha Jumatano tarehe 30 Aprili 2025, pamoja na mambo mengine, kimejadili kuhusu: hali ya uchumi ilivyo mjini Vatican pamoja na changamoto zake, ili kuendelea kuimarisha mfumo wa uchumi utakaoenzi utume wa Khalifa wa Mtakatifu Petro sehemu mbalimbali za dunia. Sera na mikakati ya vitega uchumi vya Vatican; hali ya kifedha ya Benki Kuu ya Vatican, IOR, iliyoanzishwa kunako mwaka 1942 na Papa Pio XII, inajihusisha na huduma kwa mashirika ya kitawa, kazi za kitume na shughuli za uinjilishaji unaofanywa na Kanisa la Kiulimwengu. Makardinali wamesikiliza pia taarifa ya ukarabati mkubwa unaoendelea kufanyika kwenye Sekretarieti kuu ya Vatican. Baraza la Huduma ya Upendo limeonesha kwa kina na mapana shughuli zake mbele ya Makardinali.

Utume wa Kanisa kwa vijana bado ni kipaumbele cha kwanza
Utume wa Kanisa kwa vijana bado ni kipaumbele cha kwanza   (Vatican Media)

Mambo mengine yaliyojadiliwa ni pamoja na: taalimungu ya watu wa Mungu; mateso na mahangaiko ya watu wa Mungu; tunu msingi za ujenzi wa Kanisa la Kisinodi na Kimisionari; Urika wa Maaskofu pamoja na marejeo ya umuhimu wa Nyaraka za Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican, lakini zaidi: Mwanga wa Mataifa, Lumen gentium; pamoja na Furaha na Matumaini, Gaudium et spes. Makardinali wamekazia umuhimu wa kutangaza na kushuhudia tunu msingi za Kiinjili kama sehemu muhimu sana ya mchakato wa uinjilishaji mpya. Baada ya maadhimisho ya Ibada ya Misa Takatifu kwa ajili ya uchaguzi wa Khalifa wa Mtakatifu Petro, tarehe 7 Mei 2025, Makardinali watatakiwa kuhamia kwenye Hosteli ya Santa Martha. Chumba kilichokuwa kinatumiwa na Hayati Baba Mtakatifu Francisko kitafunguliwa tu, mara baada ya uchaguzi wa Khalifa wa Mtakatifu Petro. Mchakato wa upigaji kura utakuwa ni mara mbili kwa siku; asubuhi na jioni. Wakati huo huo, Kardinali Giovanni Battista Re, Dekano wa Baraza la Makardinali kwa niaba ya Baraza la Makardinali amemtumia barua ya shukrani Mstahiki Meya wa Jiji la Roma, Mheshimiwa Roberto Gualtieri, kwa jinsi ambavyo watu wa Mungu Jijini Roma walivyoshiriki kwa wingi kutoa heshima zao za mwisho na hatimaye, maziko ya Hayati Baba Mtakatifu Francisko. Jiji la Roma liliwawezesha mahujaji wa matumaini kutoka sehemu mbalimbali za dunia kuweza kushiriki katika mazishi ya Baba Mtakatifu Francisko. Amewashukuru watu wote wa Mungu Jijini Roma kwa utayari na ushiriki wao uliowezesha kufanikisha mazishi ya Baba Mtakatifu Francisko.

Vipaumbele vya Kanisa
05 Mei 2025, 14:08