杏MAP导航

Tafuta

Kanuni maadili na utu wema ni kiini cha Mafundisho Jamii ya Kanisa, chombo cha ujenzi wa amani na majadiliano ili kujenga madaraja ya kuwakutanisha watu Kanuni maadili na utu wema ni kiini cha Mafundisho Jamii ya Kanisa, chombo cha ujenzi wa amani na majadiliano ili kujenga madaraja ya kuwakutanisha watu  (ANSA)

Baba Mtakatifu Leo XIV: Umuhimu wa Mafundisho Jamii ya Kanisa

Kanuni maadili na utu wema ni kiini cha Mafundisho Jamii ya Kanisa, chombo cha ujenzi wa amani na majadiliano ili kujenga madaraja ya kuwakutanisha watu sanjari na ujenzi wa udugu wa kibinadamu ulimwenguni. Hii ni sehemu ya hotuba iliyotolewa na Baba Mtakatifu Leo XIV kwa wanachama wa Mfuko wa “Centesimus Annus Pro Pontefice” kwa ajili ya Khalifa wa Mtakatifu Petro, CAPP., Jumamosi tarehe 17 Mei 2025. Maskini ni amana na utajiri wa Mama Kanisa.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Mfuko wa “Centesimus Annus Pro Pontefice” kwa ajili ya Khalifa wa Mtakatifu Petro, CAPP, ulianzishwa na Mtakatifu Yohane Paulo II, tarehe 5 Juni 1993. Hii ni kumbu kumbu endelevu tangu Papa Leo XIII alipochapisha Waraka wake wa Kitume “Rerum Novarum” yaani “Mambo Mapya” msingi wa Mafundisho Jamii ya Kanisa. Lengo la mfuko huu ni: Kufanya upembuzi yakinifu, kufafanua na kumwilisha Mafundisho Jamii ya Kanisa katika uhalisia wa maisha ya watu, kwa kuwasaidia: wafanyabiashara na wataalam katika medani mbalimbali za maisha; kufahamu shughuli zinazotekelezwa na Vatican katika kulinda, kutetea na kudumisha utu na heshima ya binadamu kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Mfuko huu umeendelea kuwa nyenzo muhimu sana ya ushuhuda wa uwepo fungamani wa Kanisa katika medani mbalimbali za maisha ya mwanadamu. Mfuko huu unawajumuisha viongozi wa Kanisa Katoliki, wasomi na wataalamu kutoka katika nyanja mbalimbali. Wanachama wa Mfuko wa “Centesimus Annus Pro Pontefice” kwa ajili ya Khalifa wa Mtakatifu Petro, CAPP, kuanzia tarehe 15 hadi 17 Mei 2025 wamekuwa wakiadhimisha Mkutano wao mkuu ulionogeshwa na kauli mbiu: “Jinsi mawazo ya Mafundisho Jamii ya Kikatoliki Yanavyochangia Mazungumzo ya Uongozi Wenye Uwajibikaji na Ushirikiano Katika Ulimwengu Wenye Migawanyiko.” Kanuni maadili na utu wema ni kiini cha Mafundisho Jamii ya Kanisa, chombo cha ujenzi wa amani na majadiliano ili kujenga madaraja ya kuwakutanisha watu sanjari na ujenzi wa udugu wa kibinadamu ulimwenguni.

Papa Leo XIV akizungumzia umuhimu wa Mafundisho Jamii ya Kanisa
Papa Leo XIV akizungumzia umuhimu wa Mafundisho Jamii ya Kanisa   (ANSA)

Hii ni sehemu ya hotuba iliyotolewa na Baba Mtakatifu Leo XIV kwa wanachama wa Mfuko wa “Centesimus Annus Pro Pontefice” kwa ajili ya Khalifa wa Mtakatifu Petro, CAPP., Jumamosi tarehe 17 Mei 2025.Katika Kipindi hiki cha Pasaka, Kristo Yesu Mfufuka anawatangulia waja wake kwenda hata pale ambapo inaonekana kwamba, dhuluma na utamaduni wa kifo vinaonekana kushinda. Hii ni changamoto na mwaliko kutoka kwa Baba Mtakatifu Leo XIV anayewaalika waamini na watu wote wenye mapenzi mema kusaidiana kujenga madaraja ya kuwakutanisha watu, kwa njia ya majadiliano katika ukweli na uwazi; kwa watu kukutana, watu wote waweze kuunganika na kuwa wamoja ili kujenga na kudumisha amani ulimwenguni. Kwa njia ya mwingiliano na mafungamano ya watu wenye nguvu, unawezesha neema na uhuru kuweza kuwaimarisha. Papa Leo XIII aliyeishi katika kipindi cha mapinduzi, yaliyosababisha usumbufu mkubwa, tayari alilenga kuhakikisha kwamba, anachangia katika ujenzi wa amani, kama ilivyo kwa wakati huu, ambapo Papa Francisko alipenda kutumia neno “Polycris” akimaanisha “Mgogoro wa kisiasa” ambao umeibua vita, athari za mabadiliko ya tabianchi; ongezeko la ukosefu wa usawa, uhamiaji wa nguvu; unyanyapaa kwa maskini; uvumbuzi wa teknolojia mpya zinazoleta mkanganyiko; na hivyo kuhatarisha fursa za ajira na haki kushindwa kukutana.

Mafundisho Jamii ya Kanisa: Mazingira Nyumba ya Wote
Mafundisho Jamii ya Kanisa: Mazingira Nyumba ya Wote   (ANSA)

Kuhusu masuala haya muhimu katika maisha ya binadamu, Mafundisho Jamii ya Kanisa yanaalikwa kutoa funguo za ufasiri zinazoweka sayansi na dhamiri katika majadiliano na hivyo kutoa mchango wa kimsingi wa ujuzi na maarifa, matumaini na amani. Kimsingi Mafundisho Jamii ya Kanisa yanawasaidia watu kutambua matatizo au majibu yanayopaswa kutolewa na jinsi ya kukabiliana nayo kwa kutumia vigezo vya tathmini, kanuni maadili na utu wema, daima wakiwa wazi kupokea neema ya Mungu.Baba Mtakatifu Leo XIV amewaambia wanachama hawa kwamba, wanayo fursa ya kuonesha kwamba, Mafundisho Jamii ya Kanisa, pamoja na mwelekeo wake kwa utu na heshima ya binadamu yanalenga kukuza ufikiaji wa kweli wa masuala jamii, kwa kuchambua kwa kina na mapana. Katika mambo kama haya ni vyema kufahamu zaidi jinsi ya kukabiliana nayo kwani kila kizazi ni kipya na kwamba, changamoto nazo ni mpya, ndoto mpya na pia maswali ni mapya.Baba Mtakatifu Leo XIV anakazia umuhimu wa ujenzi wa utamaduni wa watu kukutana kwa njia ya majadiliano ili kuweza kujadiliana: Sayansi, nidhamu au maraarifa. Hivyo inafahamika kwamba, kila fundisho ni tunda la utafiti, lengo ni kufikia ukweli. Mafundisho kinyume cha maadili yanazuia hukumu ya uhakiki, yanashambulia uhuru mtakatifu wa kuheshimu dhamiri ya mtu mwenyewe na hivyo kujifunga lenyewe kwa kukataa mabadiliko, mawazo au mageuzi ya mawazo mbele ya matatizo mapya. Mafundisho Jamii ya Kanisa ni kama tafakari nzito yenye utulivu na kali inayokusudia kuwafundisha watu: Mosi, kufahamu jinsi ya kukabiliana na hali na watu husika na hivyo kuwawezesha watu kutunga hukumu ya busara. Jamii inapaswa kujifunza: Umakini, ukali na utulivu kutoka kwa kila fundisho na katika muktadha huu Mafundisho Jamii ya Kanisa. Baba Mtakatifu Leo XIV anasema, katika muktadha wa mapinduzi ya kidijitali yanayoyoendelea kupamba moto sehemu mbalimbali za dunia, jukumu la kuelimisha lazima lipewe kipaumbele cha kwanza kwa kugunduliwa tena upya, kwa kuliweka wazi na kukuzwa, kwa kuangalia pia vishawishi vya wazi vilivyopo. Mara nyingi habari za uwongo na kughushi zinawanyanyasa wengi.

Mfuko kwa Ajili ya Khalifa wa Mtakatifu Petro: Ushuhuda
Mfuko kwa Ajili ya Khalifa wa Mtakatifu Petro: Ushuhuda   (ANSA)

Kumbe kukuza na kusoma akama za nyakati ni jambo la msingi, kama vile kukutana na kuwasikiliza maskini ambao kimsingi ni: amana, utajiri na hazina ya binadamu na Kanisa na kwamba, kuna haja ya kuuangalia ulimwengu kwa macho ya Kimungu, kwa kutoa kipaumbele cah pekee kwa maskini.Mababa wa Mataguso Mkuu wa Pili wa Vatican katika matumaini na fadhaa ya binadamu katika ulimwengu mamboleo wanasema, “ni wajibu wa kudumu wa Kanisa kuchunguza ishara za nyakati na kuzifahamu katika mwanga wa Injili hivi kwamba, kwa namna inayolingana na kila kizazi, liweze kuyajibu masuala yarudiayo siku zote mintarafu umaana wa maisha ya kisasa nay ale ya wakati ujayo, tena namna yanavyohusiana kati yao.” Gaudium et spes 4.Baba Mtakatifu Leo XIV mwishoni mwa hotuba yake amewaalika wanachama hawa kuhakikisha kwamba, wanashiriki kikamilifu katika mchakato wa mang’amuzi, yatakayosaidia kukuza na kuendeleza Mafundisho Jamii ya Kanisa, kwa kuendelea kushirikishana na kushikamana na watu wa Mungu, katika nyakati hizi muhimu katika historia ya maisha ya mwanadamu; mambo makubwa yanayogusa masuala jamii; kwa kusikiliza na kujadiliana na wote. Kuna haja ya kuendeleza na kudumisha haki miongoni mwa vijana wa kizazi kipya na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa vipaumbele vya jamii. Kwa sasa kuna kiu kubwa ya Mafundisho Jamii ya Kanisa, changamoto na mwaliko kwa watu wa Mungu kuitikia. Amewashukuru kwa sadaka na majitoleo yao amewasihi kuendelea kumsindikiza kwa sala katika maisha na utume wake.

Mfuko wa Centesimus Annus Pro Pontifice

 

17 Mei 2025, 16:43