Slovakia Mahujaji wa Matumaini, Umoja na Mshikamano na Khalifa wa Mt. Petro
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Jubilei ya Mwaka 2025 ya Ukristo inanogeshwa na kauli mbiu “Peregrinantes in spem” yaani: “Mahujaji wa Matumaini” baada ya dhoruba ya maambukizi makubwa ya Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19 pamoja na patashika nguo kuchanika kutokana na vita inayoendelea kupiganwa vipande vipande sehemu mbalimbali za dunia. Jubilei hii ni muda muafaka wa kupyaisha imani, matumaini na mapendo thabiti, kwa kuishi kama ndugu wamoja, sanjari na kusikiliza pamoja na kujibu kilio cha Dunia Mama na Kilio cha Maskini. Ni muda wa toba na wongofu wa ndani na wa kiikolojia, tayari kusimama kidete kulinda na kutunza mazingira nyumba ya wote. Ni muda muafaka kwa waamini kujikita katika kutangaza na kushuhudia imani na matumaini yanayomwilishwa katika huduma ya upendo kwa Mungu na jirani; kwa kukazia umoja na utofauti wa wateule watakatifu wa Mungu. Jubilei ni muda uliokubalika na Mwenyezi Mungu wa kuhakikisha kwamba, waamini wanajitahidi kumwilisha karama na mapaji yao kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Lengo ni kutangaza na kushuhudia imani na furaha ya Injili kwa watu wa Mataifa.
Ni katika muktadha wa maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 2025 ya Ukristo inayoadhimishwa na watu wa Mungu kutoka nchini Slovakia, Baba Mtakatifu Francisko, Ijumaa tarehe 4 Aprili 2025 amewaandikia ujumbe kwa kuwatia shime, ari na moyo mkuu wakati huu wanapoadhimisha Jubilei hii Kitaifa kama kielelezo cha imani na ushirika, huku akijunga nao kwa sala na upendo wake kwao. Baba Mtakatifu amewasalimia watu wote wa Mungu wanaofanya hija ya maisha yao kiroho mjini Vatican, kama sehemu ya mchakato unaopania kupyaisha imani, kujenga na kuimarisha mahusiano na mafungamano na Khalifa wa Mtakatifu Petro, tayari kutangaza na kushuhudia kwa furaha, tumaini lisilo katisha tamaa.Baba Mtakatifu Francisko anakaza kusema, ili ni tumaini linalobubujika kutoka katika Moyo Mtakatifu wa Kristo Yesu, uliotobolewa kwa mkuki, na kumiminwa ndani wao na Roho Mtakatifu ukawa ni chemchemi ya Sakramenti za Kanisa. Huu ni mwaliko kwa watu wa Mungu nchini Slovakia kuwa ni vyombo na mahujaji wa tumaini hili katika maisha yao yote. Hija ya maisha ya kiroho kwa kutembelea Roma na hivyo kupita katika Malango ya Huruma ya Mungu ni mwaliko wa kuendelea na hija hii inayofikia hatima yake katika umilele.
Baba Mtakatifu ameukumbuka mchango mkubwa wa ushuhuda kutoka kwa Watakatifu Cyril na Methodius na wengine walioimwagilia Injili ya Kristo Yesu kwa ushuhuda wa maisha yao ambayo yamesimikwa katika furaha ya Injili. Kama ilivyokuwa kwa Bikira Maria katika unyenyekevu na ujasiri aliweza kukubali na hatimaye, kuitikia wito wa Mungu na hivyo kufungua Mlango wa Ukombozi na kwa hakika akawa ni Tabernakulo ya kwanza ya Neno aliyefanyika Mtu. Bikira Maria akaukaribisha na kuumwilisha mpango wa Mungu katika maisha na kwamba, Mwenyezi Mungu anawaongoza waja wake na kuwatangulia kwa njia ya uwepo wake angavu.Ndiyo ya waamini isaidie kufungua upeo mpya wa imani, matumaini na amani, kwa ajili yao wenyewe na kwa wale ambao Mwenyezi Mungu huwafanya kuwa wamoja. Baba Mtakatifu Francisko anawahamasisha waamini nchini Slovakia kushiriki kikamilifu katika ujenzi wa Kanisa la Kisinodi na Kimisionari kwa kuendelea kusikiliza ujumbe wa Roho Mtakatifu kwa ajili ya Makanisa na hivyo kuendelea kutambua mpango wa Mungu unaowashangaza sana katika maisha yao; waendelee kushikamana na kutembea kwa pamoja na viongozi wao, huku wakiendelea kumkazia macho Kristo Yesu, wokovu wao. Bikira Maria Mama wa matumaini Mlinzi na msimamizi wa Slovakia awasaidie, awaongoze na kuwalinda.