Papa kwa Wasalesiani:Wasalesiani wana shauku ya Yesu Kristo na kujitolea kwa vijana.Ni mpango mzuri sana!
Na Angella Rwezaula – Vatican.
Katika fursa ya Mkutano Mkuu wa XXIX wa Shirika la Wasalesini wa Don Bosco, ulioanza tangu tarehe 16 Februari na utahitimishwa tarehe 12 Aprili 2025, Baba Mtakatifu amewatumia ujumbe wake. Katika Ujumbe huo anaanza kuwaelezea juu ya kutokuweza kukutana nao kwa bahati mbaya, lakini anawatumia “ujumbe katika fursa hiyo na pia katika maadhimisho ya miaka 150 tangu kutumwa wamisionari wa Kwanza wa Don Bosco nchini Argentina.
Kufuatia na kuchaguliwa kwa Mkuu Mpya wa Shirika, Baba Mtakatifu “anatuma salamu kwa Mkuu mpya wa Shirika hilo, Padre Fabio Attard, akimtakia heri na kazi njema na katika fursa hiyo amemshukuru Kardinali Ángel Fernández Artime aliyeongoza shirika hilo kuanzia(2014-2024), kwa ajili ya huduma ambayo aliwezesha kwa miaka hiyo na ambapo kwa sasa anaendelea kuitoa katika Kanisa la Ulimwengu," baada ya kuchaguliwa kuwa Kardinali.
Kwa njia hiyo hata akiwa mbali, kwa maana ya kuwa katika nyumba ya Mtakatifu Marta mjini Vatican, Papa Francisko amebainisha kuwa “ningependa kuwahimiza kuishi kwa uaminifu na kujitolea wakati huu wa kusikiliza Roho na utambuzi wa sinodi." Kwa njia hiyo katika mkutano huo wamechagua, kama mada ya kazi yao, yenye kauli mbiu: "Wasalesiani wana shauku kwa Yesu Kristo na kujitolea kwa vijana." Ni mpango mzuri sana: kuwa na "shauku" na "kujitolea", kujiruhusu kushiriki kikamilifu katika upendo wa Bwana na kutumikia wengine bila kujiwekea chochote, kama vile Mwanzilishi wao alivyofanya wakati wake.”
Papa ameongeza kuwa: "Hata kama leo hii, ikilinganishwa na wakati huo, changamoto zinazopaswa kukabili zimebadilika kwa kiasi fulani, imani na shauku inabaki vile vile, iliyojaa karama mpya, kama ile ya tamaduni tofauti." Kwa hiyo Papa anawashukuru "kwa mema wanayofanya duniani kote na anawatia moyo waendelee na uvumilivu." Amewabariki kwa moyo wote na kazi yao ya Mkutano mkuu pamoja na wanashiriki waliotawanyika katika mabara matano na anawaomba tafadhali wamuombee. Mama Maria Msaada wa Wakristo daima awasindikize."