Papa Francisko:utume wa kiafya siyo rahisi lazima usaidiwe na kuheshimiwa
Na Angella Rwezaula – Vatican.
Baba Mtakatifu Francisko, Dominika tarehe 6 Aprili 2025, kama kawaida ya kila Dominika ameandaa Mahubiri yake kabla ya sala ya Malaika wa Bwana. Papa anabainisha kuwa Injili ya Dominika ya 5 ya Kwaresima inawakilisha tukio la mwanake aliyefumaniwa katika uzinzi. (Yh 8,1-11). Wakati waandishi na mafarisayo wanataka kumpiga mawe, Yesu anamrudishia mwanamke huyo, uzuri uliopotea. Yeye alianguka katika mavumbi; Yesu katika mavumbi hayo alipitisha kidole chake na aliandika kwa ajili yake historia mpya: ni kidole cha Mungu ambaye anaokoa watoto wake (Es 8,15) na kumukoa katika dhambi( Lk 11,20).
Baba Mtakatifu amebainisha kuwa “kama wakati wa kulazwa, hata sasa katika kuendelea na tiba, ninahisi “kidole cha Mungu” na nafanya uzoefu wake wa bembelezo lake. Katika siku ya Jiblei ya wagonjwa na ya Ulimwengu wa kiafya, ninaomba Bwana ambaye kwa mguso wa upendo wake uwafikie wale ambao wanateseka na kuwatia moyo wale ambao wanawasaidia. Na ninasali kwa ajili ya madaktari, wauguzi na wahudumu wa kifya, ambao si mara zote wanasaidiwa katika kazi katika hali inayofaa na wakati mwingine hadi kuwa wahanga wa kushambuliwa. Utume wao siyo rahisi na wanapaswa kusaidiwa na kuheshimiwa. Ni matumaini yangu kuwa wanaweza kuwa rasilimali ya lazima kwa ajili ya tiba na kwa ajili ya utafiti. Kwa sababu, mifumo ya kifya iweze kuwa jumuishi na makini kwa walio wadhaifu zaidi na walio maskini.”
Asante wafungwa wa kike Rebibbia
Papa ametoa shukurani kwa matashi mema kutoka kwa wafungwa: “Ninashukuru wafungwa wa magereza ya kike ya Rebibbia kwa kadi ambayo mmenitumia. Ninasali kwa ajili yao na kwa ajili ya familia zao.”
Siku ya michezo duniani
Katika kumbukizi ya kimataifa Papa amesema “Katika Siku ya Dunia ya Michezo kwa ajili ya Amani na Maendeleo, ninatumaini kwamba michezo itakuwa ishara ya matumaini kwa watu wengi wanaohitaji amani na ushirikishwaji wa kijamii, na ninashukuru vyama vya michezo vinavyoelimisha kikamilifu kuhusu udugu.”
Tuendelee kuombea Ukraine na Gaza
Kama kawaida ya Papa Francisko hakukosa kutazama vita vilivyosambaa ambapo amesema: “Tuendelee kuombea amani: katika Ukraine inayoteswa, iliyokumbwa na mashambulizi yanayosababisha wahanga wengi wa raia, wakiwemo watoto wengi. Na hali hiyo hiyo inatokea huko Gaza, ambapo watu wanalazimika kuishi katika mazingira yasiyoweza kufikiria, bila makazi, bila chakula, bila maji safi.”
Silaha zinyamaze
Hatimaye ametoa wito wake kuwa “Silaha zinyamaze na mazungumzo yaanze tena; mateka wote lazima waachiliwe na watu lazima wasaidiwe. Tuombe amani katika eneo lote la Mashariki ya Kati; katika Sudan na Sudan Kusini; katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo; huko Myanmar, pia ilikumbwa sana na tetemeko la ardhi; na huko Haiti, ambako vurugu zinaendelea, ambazo ziliua watawa wawili siku chache zilizopita. Bikira Maria atulinde na kutuombea.”