Papa Francisko: Taasisi ya Kipapa ya Sayansi ya Diplomasia 2025
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Taasisi ya Kipapa ya Diplomasia ya Kanisa “Pontificia Accademia Ecclesiastica, PAE” ilianzishwa kunako mwaka 1701 na kuidhinishwa na Papa Clementi wa XI. Papa Pio XI akaipatia taasisi hii jina la “Taasisi ya Kipapa ya Diplomasia ya Kanisa. Baba Mtakatifu Francisko tarehe 15 Aprili 2025 amefanya mageuzi makubwa kwa Taasisi ya Kipapa ya Diplomasia ya Kanisa na kuigeuza kuwa ni Taasisi ya Kipapa ya Sayansi ya Diplomasia, lengo ni kuwaandaa Mapadre watakaokuwa wanatumwa sehemu mbalimbali za dunia kama wawakilishi wa Khalifa wa Mtakatifu Petro, kama kielelezo cha utekelezaji wa dhamana na utume wa umisionari wa Kanisa. Mabalozi wa Vatican ni wawakilishi wa Khalifa wa Mtakatifu Petro anayewakilisha Kanisa lote katika kifungo cha amani, upendo na umoja. Mabalozi wa Vatican ni Mapadre wanaotekeleza dhamana na wajibu wao katika ari na mwamko wa Kikasisi, huku wakitumia karama na mapaji waliyokirimiwa na Roho Mtakatifu kwa ajili ya mchakato wa uinjilishaji. Hawa ni viongozi wanaoteuliwa kwa ajili ya huduma kwa Makanisa mahalia na hivyo kuwa ni kiungo kati ya Baba Mtakatifu, Kanisa mahalia na viongozi wa Serikali, kumbe ni watumishi wanaopaswa kufahamu fika Sheria za Kimataifa, maisha ya watu wanaowahudumia na sehemu mbalimbali ambako kuna mahitaji msingi ya watu wa Mungu. Leo hii anasema Baba Mtakatifu Francisko kuna changamoto mamboleo zinazomwandama mwanadamu mintarafu kanuni maadili na utu wema mintarafu ustawi, maendeleo na mafao ya wengi, mambo yanayohitaji majiundo makini na endelevu na kwa kuzingatia mchakato wa ujenzi wa Kanisa la Kisinodi na Kimisionari. Ili kutekeleza dhamana na wajibu huu msingi kuna haja ya kujenga na kukuza tabia ya ujirani mwema, utamaduni wa kusikiliza kwa makini, ushuhuda wenye mvuto na mashiko; ni watu ambao wako tayari kujibidiisha katika ujenzi wa udugu wa kibinadamu unaosimikwa katika fadhila ya unyenyekevu na upendo, ili hatimaye, waweze kufanana na Kristo Yesu, Mchungaji mwema. Rej. Mt 11:28-30; Yn 10: 11-18.
Mapadre wanaoteuliwa kwa uangalifu mkubwa kutoka katika Majimbo mbalimbali wanapaswa kuandaliwa kwa umakini mkubwa ili waweze kukabiliana na kwa ufanisi na changamoto mamboleo zinazomwandama mwanadamu hasa kutokana na maendeleo makubwa ya sayansi na teknolojia. Taasisi ya Kipapa ya Diplomasia ya Kanisa “Pontificia Accademia Ecclesiastica, PAE” kwa muda wa takribani miaka mia tatu, imekuwa ikitekeleza dhamana na wajibu huu kama Chuo cha Diplomasia ya Kanisa. Ni katika muktadha huu wa maendeleo na Mapokeo kutoka kwa watangulizi wake, Baba Mtakatifu Francisko anasema, kuanzia tarehe 15 Aprili 2025 ameanzisha Taasisi ya Kipapa ya Diplomasia ya Kanisa kama Kitivo cha Sayansi ya Diplomasia na hivyo kuzingatia miongozo ya Sheria za Kanisa, Sheria na Taratibu za Sekretarieti kuu ya Vatican na Kitivo hiki kitatoa Shahada katika medani mbalimbali za maisha ya Jumuiya ya Kimataifa yaani: Sayansi ya Diplomasia, Historia, Sheria, Uchumi na Lugha kwa kuzingatia mahitaji ya Sekretarieti kuu ya Vatican, Makanisa mahalia na Jumuiya ya Kimataifa mintarafu mchakato wa uinjilishaji wa kina unaogusa mahataji msingi ya binadamu: kiroho na kimwili. Hiki ni kitivo kinachopania pamoja na mambo mengine, kujenga na kudumisha utamaduni wa majadiliano ili kulinda: amani, utu, heshima na haki msingi za binadamu sanjari na uhuru wa kidini kwa waamini wote; pamoja na Usalama kwa Jumuiya ya Kimataifa. Hii ni Taasisi itakayojikita katika majiundo makini ya Mabalozi wa Vatican pamoja na Tafiti za kina.
Wakati huo huo, Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican anasema diplomasia ya Vatican na Kanisa Katoliki katika ujumla wake, inatoa kipaumbele cha pekee kwa: Amani, uhuru wa kidini, utu, heshima na haki msingi za binadamu aliyeumbwa kwa sura na mfano wa Mungu, bila kusahau utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote. Hii ndiyo dhamana inayotekelezwa na Vatican katika medani mbalimbali za Kimataifa. Kutambua na kuheshimu haki msingi za binadamu ni hatua muhimu sana ya maendeleo fungamani ya binadamu, kwani mizizi ya haki za binadamu inafumbatwa katika hadhi, heshima na utu wa binadamu aliyeumbwa kwa sura na mfano wa Mungu. Hizi ni haki za wote zisizoweza kukiukwa wala kutenguliwa. Ni za binadamu wote bila kujali: wakati, mahali au mhusika. Haki msingi za binadamu zinapaswa kulindwa na kudumishwa na wote. Haki ya kwanza kabisa ni uhai tangu pale mtoto anapotungwa mimba tumboni mwa mama yake hadi pale anapofariki dunia kadiri ya mpango wa Mungu. Mkazo umewekwa katika haki ya uhuru wa kidini inayofafanuliwa katika uhuru wa kuabudu. Hiki ni kiini cha haki msingi kinachofumbata haki nyingine zote. Kuheshimu na kuthamini haki hii ni alama ya maendeleo halisi ya binadamu katika medani mbalimbali za maisha. Haki inakwenda sanjari na wajibu! Mama Kanisa anakazia kwa namna ya pekee kabisa, umuhimu wa kuheshimu haki msingi za binadamu, kichocheo muhimu sana cha amani na utulivu miongoni mwa binadamu. Kanisa linapenda kusimama kidete: kulinda na kudumisha haki na amani sehemu mbalimbali za dunia kwa njia ya mwanga na chachu ya tunu msingi za Kiinjili!
Hii ni amani inayofumbatwa katika: ukweli, haki, mshikamano na uhuru wa kweli. Uhuru wa kidini ni sehemu muhimu sana ya Tamko la Haki Msingi za Binadamu lililopitishwa na Umoja wa Mataifa kunako mwaka 1948. Mwamini anapaswa kukiri na kushuhudia imani yake inayomwilishwa katika matendo. Uhuru wa kidini ni kati ya mambo ambayo hayapewi tena kipaumbele cha pekee katika vyombo vya utekelezaji wa sheria na hata wakati mwingine kwenye vyombo vya mawasiliano ya jamii. Kuna haja ya kuwajulisha walimwengu kwamba, kuna nyanyaso na dhuluma za kidini zinazoendelea kutendeka sehemu mbalimbali za dunia, kinyume kabisa cha haki msingi za binadamu.Mahusiano ya kidiplomasia kati ya Vatican na Mataifa mbalimbali duniani yanafanyika kwa uvumilivu na ustahimilivu mkubwa, hata sehemu ambazo kuna ugumu mkubwa, kwa kuwa kuna matumaini ya familia bora ya wanadamu kwa baadae. Shughuli za kidiplomasia zinakuwa nyenzo katika kufuatilia, kushiriki, na kushawishi katika Jumuiya na maisha ya Kimataifa. Utume wa Kanisa ni kuhangaikia kwa matumaini na kushuhudia ile hamu ya amani, haki na mafao ya wengi. Kardinali Parolin amegusia umuhimu wa mahusiano ya kidiplomasia kati ya Vatican na Mataifa mbali mbali duniani na kwamba, yanatekelezwa kwa uvumilivu mkubwa, hata sehemu ambazo kuna ugumu, kwa kuwa kuna matumaini ya ujenzi wa familia bora ya wanadamu kwa siku za mbeleni. Shughuli za kidiplomasia ni nyenzo katika kufuatilia, kushiriki, na kutoa ushawishi katika Jumuiya ya Kimataifa. Utume wa Kanisa ni kuhangaikia kwa matumaini na kushuhudia ile hamu ya haki, amani, ustawi na mafao ya wengi. Kimsingi, matatizo na changamoto mbalimbali zinapaswa kujadiliwa kwa kuzingatia msingi ya ukweli na uwazi; kuibua mbinu mkakati na hatimaye, sera za utekelezaji wake. Changamoto kubwa kwa wakati huu ni amani. Kuna baadhi ya Mataifa yanatishia kufumbia macho mafao ya wengi, hali ambayo inayatumbukiza Mataifa yenye mwelekeo kama huo katika uchoyo na ubinafsi. Mafanikio ya taifa lolote liwe yanapata chimbuko lake katika elimu na tafiti makini.
Kwa upande wake, Askofu mkuu Salvatore Pennacchio, Rais wa Taasisi ya Kipapa ya Diplomasia ya Kanisa “Pontificia Accademia Ecclesiastica, PAE”, anasema, kumekuwepo na mabadiliko makubwa ikiwa ni pamoja na kuanzishwa kwa “Mwaka wa Kimisionari” unaofanywa na Mapadre kabla ya kuingizwa kwenye diplomasia ya Kanisa; Sheria za Diplomasia ya Kimataifa; Mahusiano ya Kimataifa pamoja na kujifunza Lugha. Kumekuwepo na mahitaji ya majiundo ya majadiliano ya kidini na kiekumene; majadiliano ya kisiasa katika ukweli na uwazi; na kuendelea kusimamia ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Mabalozi wa Vatican wanapaswa kuwa ni viongozi wenye uwezo wa kujenga Kanisa la Kisinodi na Kimisionari, tayari kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu. Majiundo yote haya yanasimikwa katika: Uelewa wa Neno la Mungu, Maisha ya Sala na Unyenyekevu katika huduma.