杏MAP导航

Tafuta

Baba Mtakatifu Francisko, Jumatano tarehe 16 Aprili 2025 amekutana na kuzungumza na wafanyakazi  wa Mfuko wa Hospitali ya Chuo Kikuu cha Agostino Gemelli Baba Mtakatifu Francisko, Jumatano tarehe 16 Aprili 2025 amekutana na kuzungumza na wafanyakazi wa Mfuko wa Hospitali ya Chuo Kikuu cha Agostino Gemelli  (ANSA)

Papa Francisko Awashukuru Wahudumu wa Afya Hospitali ya Gemelli

Baba Mtakatifu Francisko, Jumatano tarehe 16 Aprili 2025 amekutana na kuzungumza na wafanyakazi wa Mfuko wa Hospitali ya Chuo Kikuu cha Agostino Gemelli, Chuo Kikuu cha Kikatoliki cha Agostino Gemelli pamoja na Kurugenzi ya Afya na Usafi ya Vatican kuwashukuru kwa ukarimu na udugu wao wa kibinadamu, ambao ameuonja wakati wote alipokuwa amelazwa hospitalini hapo, kiasi cha kumfanya ajisikie kuwa yuko nyumbani. Jumla yao walikuwa ni 70.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko alikuwa anasumbuliwa na ugonjwa wa mkamba (Bronchitis) uliopelekea kulazwa tangu Ijumaa tarehe 14 Februari 2025 kwenye Hospitali ya Chuo Kikuu cha Agostino Gemelli, iliyoko mjini Roma. Ugonjwa wa mkamba ni wa kawaida kwa watu wengi hasa katika kipindi hiki, kiasi kwamba, vituo vya dharura nchini Italia vilikuwa vimefurika. Kumbe, huduma hii kwa Baba Mtakatifu lilikuwa ni jambo la kawaida kwa mtu mwenye umri wa miaka 88 kupatiwa mahali pa faragha kwa matibabu zaidi; matibabu yaliyotolewa kwa ushirikiano mkubwa na jopo la madaktari likiongozwa na Daktari Sergio Alfieri na hatimaye tarehe 23 Machi 2025 akaruhusiwa kurejea mjini Vatican, huku akiendelea na matibabu. Falsafa ya neno asante ni kuomba tena! Waswahili husema, “Moyo usio na shukrani hukausha mema yote.” Baba Mtakatifu Francisko, Jumatano tarehe 16 Aprili 2025 amekutana na kuzungumza na wafanyakazi wa Mfuko wa Hospitali ya Chuo Kikuu cha Agostino Gemelli IRCCS “Fondazione Policlinico Universitario Agostino Gemelli IRCCS”, Chuo Kikuu cha Kikatoliki cha Agostino Gemelli pamoja na Kurugenzi ya Afya na Usafi ya Vatican kuwashukuru kwa ukarimu na udugu wao wa kibinadamu, ambao ameuonja wakati wote alipokuwa amelazwa hospitalini hapo, kiasi cha kumfanya ajisikie kuwa yuko nyumbani, jumla yao ikiwa ni watu 70.

Papa anawashukuru wafanyakazi wa Hospitali ya Gemelli, Roma
Papa anawashukuru wafanyakazi wa Hospitali ya Gemelli, Roma   (ANSA)

Baba Mtakatifu Francisko anasema, hospitali ni mahali pa mateso na mahangaiko ya binadamu, lakini pia ni mahali pa matumaini. Akiwa hospitalini hapo ameonja mazingira ya kifamilia, udugu na ukarimu; mambo ambayo yamechangia kwa kiasi kikubwa kuimarisha afya yake na hatimaye, kuruhusiwa kurejea tena kwenye Hosteli ya Mtakatifu Martha kuendelea na maisha pamoja na shughuli zake za kila siku. Anawashukuru na kuwapongeza kwa kutoa kipaumbele cha kwanza kwa huduma ya afya, daima utu, heshima na haki msingi za binadamu zikipewa kipaumbele cha kwanza. Huduma hii imenogeshwa kwa weledi wa kisayansi. Baba Mtakatifu anakiri kwamba, ndani ya moyo wake, anabeba nyuso, historia na mahangaiko ya watu mbalimbali.

Papa alilazwa kuanzia tarehe 14 Februari hadi 23 Machi 2025
Papa alilazwa kuanzia tarehe 14 Februari hadi 23 Machi 2025   (ANSA)

Hospitali ya Gemelli ni sawa na mji mdogo ndani ya Jiji kuu la Roma. Hapa ni mahali ambapo kila siku kuna maelfu ya watu wanaofika wakiwa na matumaini pamoja na wasiwasi mbalimbali kutokana na mahangaiko yao. Hospitalini hapo, licha ya kutoa huduma ya tiba, wagonjwa wanapata pia huduma ya kiroho na hivyo Hospitali inamhudumia mtu mzima: kiroho na kimwili; daima utu na heshima yake vikipewa msukumo wa pekee. Huduma hii anasema Baba Mtakatifu inakuwa ni chemchemi ya faraja na matumaini wakati wa mateso na majaribu katika maisha. Baba Mtakatifu anawapongeza kwa kazi nyeti na ngumu wanayoitekeleza Hospitalini hapo! Hii ni huduma ya huruma ambayo kwa njia ya wagonjwa, wahudumu hao wanaweza kukutana na Madonda Matakatifu ya Kristo Yesu. Baba Mtakatifu anakiri na kutambua kwamba, ameona kwa macho yake mwenyewe na akatunza hicho alichokiona na atakiwakilisha mbele ya Mwenyezi Mungu kama ushuhuda wa matendo ya huruma.

Papa Shukrani
17 Aprili 2025, 15:56