Papa Francisko Atembelea Gereza la "Regina Coeli" Na Kuzungumza Na Wafungwa
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Baraza la Kipapa la Huduma ya Maendeleo Fungamani ya Binadamu ndilo ambalo limekabidhiwa dhamana ya shughuli za kichungaji kwa ajili ya wafungwa magerezani, ili kuonesha wasiwasi na ukaribu wa Mama Kanisa kwa wafungwa wanaoteseka magerezani. Hii ni dhamana na wajibu wa Kanisa zima kama sehemu ya utekelezaji wa utume wake unaomwilisha matendo ya huruma katika uhalisia wa maisha ya watu. Wakati wa hukumu ya mwisho, watu watahukumiwa kadiri walivyowatendea ndugu zake walio wadogo, na kwa kufanya vile, walimtendea Kristo Yesu mwenyewe. (Rej. Mt. 25:40) Kristo Yesu anajitambulisha kuwa kati ya watu wenye njaa, kiu, wageni, watu walio uchi, wagonjwa na wale walioko kifungoni. Baba Mtakatifu Francisko anasema taswira inayotolewa na magereza sehemu mbalimbali za dunia inaonesha ukweli wa jamii ambamo uchoyo, ubinafsi na utandawazi wa kutoguswa na mahangaiko ya jirani vinatawala. Kuna maamuzi ambayo yamefanywa kisheria lakini yanakiuka utu, heshima na haki msingi za binadamu; kwa kujidai kukuza na kutaka kudumisha ulinzi na usalama wa raia na mali zao. Matokeo yake ni watu kutengwa na kutupwa magerezani kama suluhu ya matatizo mbalimbali yanayoisonga jamii. Lakini ikumbukwe kwamba, kuna kiasi kikubwa cha rasilimali na utajiri wa nchi unaotumika kwa ajili ya kuwahudumia wafungwa magerezani, ikilinganishwa na kiasi cha fedha zinazotengwa kwa ajili ya kuchochea kasi ya maendeleo fungamani ya binadamu, ambayo yangewezesha idadi kubwa ya wafungwa kupata kazi na kipato halali badala ya kujiingiza kwenye vitendo vya jinai na uvunjaji wa sheria. Baba Mtakatifu anakaza kusema, ni rahisi sana kufumbia macho umuhimu wa elimu na malezi makini kwa jamii, sanjari na kushindwa kuona ukweli halisi wa matatizo na ukosefu wa haki na hivyo suluhu ya haraka inayoweza kupatikana ni ujenzi wa magereza, ili “kuwashikisha adabu wale wote wanaovunja sheria za nchi.”
Umefika wakati wa kutoa msukumo wa pekee kwa ajili ya maendeleo fungamani ya binadamu kwa raia wote. Kwa bahati mbaya, magereza mengi yameshindwa kutekeleza dhamana na wajibu wake wa kuweza kutoa mafunzo bora zaidi, ili wafungwa wanapomaliza adhabu zao na kutoka magerezani waweze kuwa ni watu wema zaidi kuliko walivyoingia magerezani. Ni ukweli usioweza kufumbiwa macho kwamba, kuna uhaba mkubwa wa rasilimali fedha na watu ili kukabiliana na changamoto za kijamii, kisaikolojia na kifamilia wanazokabiliana nazo wafungwa magerezani.Baba Mtakatifu Francisko anasema, magereza yamegeuka kuwa ni mahali hatari sana, ambapo utu na heshima ya binadamu vinasiginwa. Mafunzo makini kwa wafungwa yanaanza pale ambapo wafungwa wanapewa fursa ya kushiriki katika mchakato wa maendeleo, wanapopewa elimu makini na kufanyishwa kazi zenye staha. Yote haya lazima pia yazingatie huduma bora za afya kwa wafungwa pamoja na kuunda mazingira ambayo, wafungwa wataweza pia kushirikiana kwa karibu na raia wengine. Jamii inapaswa kuwa na mwelekeo tofauti sana kwa wafungwa magerezani, kwa kuwapatia msaada wa hali na mali, ili kuboresha maisha yao, kama sehemu ya faraja kutoka kwa Mwenyezi Mungu. Kwa bahati mbaya sana, wafungwa wamekuwa wakiangaliwa kwa “jicho la kengeza” kiasi kwamba, si rahisi sana kuthamini utu na heshima yao. Wafungwa waonjeshwe matumaini na kupewa tena fursa ya kufanya kazi, ili kujipatia mahitaji yao msingi. Pale ambapo wafungwa baada ya kumaliza adhabu yao wanashindwa kutambuliwa utu na heshima yao, wanajikuta wakiwa kwenye majaribu makubwa kati ya kutafuta fursa za kazi, kutenda uhalifu pamoja na kujenga mazingira yasiokuwa salama. Baba Mtakatifu anaitaka Jumuiya ya waamini kuwaonjesha wafungwa huruma na mapendo, dhamana na utume unaopaswa kutekelezwa na Makanisa mahalia. Kila mwamini awe ni shuhuda na chombo cha huruma ya Mungu kwa wafungwa, ili kuiwezesha jamii kukita mizizi yake katika misingi ya haki na amani.
Baba Mtakatifu Francisko anakaza kusema, matendo ya huruma: kiroho na kimwili ni nyenzo thabiti katika mchakato wa huduma kwa wafungwa magerezani. Huu ni mchakato unaowawezesha watu wa Mungu kutoa huduma kwa wafungwa na hivyo kujenga ndani mwao: Imani, matumaini na mapendo. Waamini waendelee kumtambua Kristo Yesu anayejitambulisha kati ya wafungwa magerezani. Baba Mtakatifu anawapongeza wale wote wanaoendelea kujisadaka kwa ajili ya huduma kwa wafungwa pamoja na familia zao, hasa katika kipindi hiki kigumu cha majaribio. Baba Mtakatifu mwishoni anawaombea heri na baraka wale wote wanaojisadaka kwa ajili ya huduma za kichungaji kwa wafungwa magerezani sehemu mbalimbali za dunia, kwani kwa kufanya hivi, wanaendeleza utume ambao Kristo Yesu ameliachia Kanisa lake kwani mwishoni mwa maisha yao hapa dunia, wataweza kusikia “Njooni mliobarikiwa na Baba yangu, urithini ufalme mliowekewa tayari tangu kuumbwa ulimwengu.” Mt. 25:35. Ni katika muktadha wa kukazia umuhimu wa huduma bora na maboresho ya maisha ya wafungwa magerezani, Baba Mtakatifu Francisko, Alhamisi kuu tarehe 17 Aprili 2025 ametembelea Gereza Kuu la “Regina Coeli” lililopo mjini Roma! Baba Mtakatifu amebahatika kupata nafasi ya kukutana na kuzungumza na wafungwa wapatao 70 na kuwaambia kwamba, daima anatamani kuadhimisha Karamu ya Bwana pamoja na kuwaosha miguu wafungwa, lakini kwa mwaka 2025 haiwezekani, ndiyo maana amewatembelea ili kuonesha ukaribu wake kwao. Gereza ni mahali pa watu kutumikia adhabu zao na wakati mwingine ni mahali pa mateso yanayohitaji kuangaliwa kwa jicho la huruma na mapendo, kwa kukazia utu, heshima na haki msingi za binadamu. Magereza ni mahali ambapo wadau mbali mbali wanaitwa na kutumwa kuganga madonda ya watu waliofanya makosa na sasa wako kifungoni na hawana tena uhuru binafsi.
Baba Mtakatifu anasikitika kusema, kutokana na uhaba wa askari magereza pamoja na magereza kufurika kwa kuwa na idadi kubwa ya watu kuliko uwezo wake, kuna hatari kwa magereza kugeuka kuwa ni mahali ambapo watu wana changanyikiwa na hivyo kupoteza dira na mwelekeo sahihi wa maisha! Hii inatokana na ukweli kwamba, wafanyakazi magerezani wanakabiliwa na msongo mkubwa wa mawazo ambao unathari kubwa katika maisha yao, kiasi hata cha kuwafanya kushindwa kutekeleza vyema dhamana na wajibu huu tete katika maisha ya wafungwa na mahabusu. Hawa ni watu wanaopaswa kuhakikisha usalama wa wafungwa na gereza lenyewe, lakini wakati mwingine, wanajikuta wakiwaachia madonda ya kudumu wafungwa magerezani. Baba Mtakatifu anasema, magereza yanapaswa kuboreshwa zaidi, ili kulinda na kudumisha utu na heshima ya binadamu! Inasikitisha kusikia na kuona kwamba, magereza yanageuka kuwa ni mahali pa vurugu, uvunjifu wa sheria, kanuni na taratibu; mahali ambapo utu na heshima ya binadamu vinasiginwa kwa kiasi kikubwa! Ikumbukwe kwamba, wafungwa na mahabusu wengi ni watu wa kawaida kabisa; wengi wao hawana hata uhakika wa usalama wa maisha yao, hawana rejea wala familia; hawana uwezo wala nguvu ya kiuchumi kuweza kusimamia na kupigania haki zao msingi. Hawa ni watu ambao wametelekezwa na kwa jamii wanaonekana si mali kitu na hata wakati mwingine ni mzigo mzito usiobebeka hata kidogo “hata kama atabebeshwa Mnyamwezi” kama wanavyosema Waswahili!
Baba Mtakatifu anafurahi kusema kwamba, uzoefu na mang’amuzi yanaonesha kwamba, gereza linaweza kuwa ni mahali pa msaada mkubwa kwa wadau mbali mbali; mahali ambapo panaweza kugeuka kuwa ni chemchemi ya mwanzo mpya wa maisha; mahali ambapo wale waliodhani kwamba wamekufa na kusahaulika mbele ya uso wa dunia, wanaweza kufufuka tena na kutoka kifua mbele kutangaza matendo makuu ya Mungu. Gereza ni mahali ambapo wafungwa wanaweza kufanya mageuzi makubwa katika maisha yao. Baba Mtakatifu anaendelea kufafanua kwamba, yote haya yanawezekana kwa njia ya elimu na stadi za maisha; kwa uwepo wa karibu wa walezi wa maisha ya kiroho wanaotekeleza dhamana na wajibu wao kama alivyofanya Msamaria mwema.Upendo na ukaribu kwa wafungwa unapaswa kupata chimbuko lake kutoka kwa Kristo Yesu. Hali hii itawapatia wafungwa imani na matumaini kwamba, wanapendwa na kuthaminiwa! Kazi hii inapaswa kutekelezwa kwa umoja, upendo na utulivu wa ndani unaooneshwa na kushuhudiwa na wadau mbali mbali, ili kuwasaidia wawe walioteleza na kuanguka katika hatia kwa makosa mbali mbali, waweze kusimama tena na kusonga mbele kwa imani na matumaini makubwa. Baba Mtakatifu amehitimisha hotuba yake, kwa kuwahakikishia wadau wote kwamba, anawasindikiza kwa sala na sadaka yake, ili kweli magereza yawe ni mahali pa kutumikia adhabu na mateso ya mwanadamu; lakini pia magereza yawe ni maabara ya utu, heshima na matumaini mapya!