Papa Francisko anaendelea kupata nafuu huko Mtakatifu Marta
Vatican News
Siku ya Dominika wakati wa sala ya Malaika wa Bwana inaweza kufanyika kwa namna tofauti ikilinganishwa na Dominika zilizopita, na sasisho litatolewa kwa mujibu wa Ofisi ya Vyombo vya habari Vatican iliyotoa taarifa kwa waandishi wa habari Ijumaa asubuhi tarehe 4 Aprili 2025. Wakati wa taarifa hiyo fupi kuhusu afya ya Papa, Ofisi ya Wanahabari ilieleza kwamba Papa Francisko anaendelea kuonesha maboresho ya kimatibabu anapopata nafuu katika makazi yake huko nyumba ya Mtakatifu Marta, kufuatia na kulazwa hospitalini kwa maambukizi ya Mapafu ambayo yalisababisha nimonia ya pande mbili.
Vipimo vya damu pia ni vizuri
Baba Mtakatifu aliruhusiwa kutoka katika Hospitali ya Gemelli jijini Roma na kutoka katika uthibiti mkali, siku ya Dominika tarehe 23 Machi 2025. Hali ya Papa Francisko kwa sasa imeonesha uboreshaji zaidi wa kupumua, mazozi ya viungo na sauti, ilibainisha taarifa ya Ofisi ya Vyombo vya Habari. Uchunguzi wa hivi karibuni wa damu pia unaonesha uboreshaji mdogo katika maambukizi yake ya mapafu. Baba Mtakatifu amekuwa akiendelea na matibabu na mazoezi ya viungo, tiba ya viungo inayohusiana na kupumua na anahitaji pia oksijeni kidogo ya ziada.
Maboresho yapo hata kwa matumizi ya Oksijeni
Wakati wa mchana, anaendelea kawaida kutumia oksijeni, na wakati, usiku akitumia oksijeni ya mtiririko wa juu kwa kutumia mirija ya pua kama inahitajika. Aidha, Papa Francisko anaendelea na shughuli zake za kazi na yuko katika ari nzuri, ilisema Ofisi ya Vyombo vya Habari. Wakati huo huo, hata Siku ya Ijumaa asubuhi tarehe 4 Aprili 2025 Baba Mtakatifu alifuatilia tafakari ya Kwaresima kwa njia ya video iliyofanyika katika Ukumbi wa Paulo VI, mjini Vatican, iliyotolewa na Mhubiri Nyumba ya Kipapa, Padre Roberto Pasolini, (OFM Cap).
Kufuatilia misa ya kumbukizi ya miaka 20 ya kifo cha Papa Yohane Paulo II
Siku ya Jumatano tarehe 2 Aprili Papa alifuatilia hatakwa njia ya video Ibada ya Misa Takatifu katika Kanisa Kuu la Mtakatifu Petro iliyoongozwa na Katibu wa Vatican, Kardinali Pietro Parolin, katika maadhimisho ya miaka 20 ya kifo cha Mtakatifu Yohane Paulo wa Pili. Ofisi ya Vyombo vya Habari ilibainisha kuwa hakupokea wageni, na kuongeza kuwa bado ni mapema sana kujadili ushiriki wa Papa katika ibada za Juma Takatifu. Sasisho zaidi la Afya ya Baba Mtakatifu utakuwa Jumanne, tarehe 8 Aprili 2025.