Mkutano Mkuu wa 29 Wa Shirika la Wasalesiani wa Don Bosco 2025
Na Padre Philemon Anthony Chacha, SDB, - Vatican.
Shirika la Wasalesiani wa Don Bosco, “Societas Sancti Francisci Salesii, SDB” lilianzishwa na Mtakatifu Yohane Bosco kunako mwaka 1859 na kukita utume wake miongoni mwa vijana maskini, huko Torino, Kaskazini mwa Italia. Wasalesiani wa Don Bosco wanaendelea kujisadaka hasa kwa ajili ya malezi, makuzi na elimu kwa vijana kwa kuwekeza hasa katika sekta ya elimu, vituo vya mafunzo, kilimo na utume katika vyombo vya mawasiliano ya jamii. Shirika kuanzia tarehe 16 Februari hadi 12 Aprili 2025 linaadhimisha Mkutano wake mkuu wa 29. Katika maadhimisho ya Mkutano mkuu wa Shirika, Wasalesiani wanamshukuru Mungu kwa matunda ya kwanza ya Wamisionari waliotumwa na Mtakatifu Yohane Bosco, miaka 150 iliyopita kwenda Argentina kueneza karama ya Shirika. Wana kila sababu ya kumshukuru Mungu kwani matunda yake ndani ya mti mkubwa ambao ni Familia ya Kisalesiani, Familia ya Don Bosco, ambapo leo hii wapo katika Mataifa 134 duniani ikiwemo Tanzania, Kenya, Sudani na Sudani Kusini, ishara ya imani, matumaini na mapendo. Ni katika muktadha wa maadhimisho ya Mkutano mkuu wa 29 wa Shirika la Wasalesiani wa Don Bosco na Jubilei ya Miaka 150 tangu Wamisionari wa kwanza walipotumwa kwenda nchini Argentina, Baba Mtakatifu Francisko ametumia fursa hii kuwatumia salam viongozi wa Shirika waliomaliza muda wao na kuwapongeza hawa waliochaguliwa. Baba Mtakatifu anapenda kuwaalika Wasalesiani kuwa na shauku na Kristo Yesu kwa kujitoa na kujisadaka kwa ajili ya huduma kwa vijana wa kizazi kipya kama sehemu ya kauli mbiu ya Maadhimisho ya Mkutano wa 29 wa Shirika. Maadhimisho haya kiwe ni kipindi cha kufanya mang’amuzi ya kina kisinodi na kwa kumsikiliza Roho Mtakatifu.
Baba Mtakatifu Francisko anawataka Wasalesiani, huku wakisukumwa na upendo wa Kristo Yesu kujisadaka bila ya kujibakiza katika huduma, kama alivyofanya Mtakatifu Yohane Bosco wakati wa uhai wake. Leo hii changamoto zimebadilika, lakini ari ya imani inaendelea kubaki ile ile huku ikirutubishwa na mwingiliano wa tamaduni. Baba Mtakatifu anawashukuru Wasalesiani kwa huduma wanayoendelea kuitoa kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya watu wa Mungu sehemu mbalimbali za dunia na anawataka waendelee kudumisha huduma hii na hatimaye, amewabariki wajumbe wa Mkutano mkuu wa 29 pamoja na Wasalesiani wote walioenea sehemu mbalimbali za dunia. Mkutano mkuu wa 29 wa Shirika la Wasalesiani wa Don Bosco umemchagua Padre Fabio Attard tarehe 25 Machi 2025, kama mrithi wa kumi na moja wa Don Bosco na atakayeongoza Familia nzima ya Kisalesiani katika kipindi cha miaka sita (2025-2031). Ikumbukwe kwamba mkutano huu ulianza tangu tarehe 16 Februari 2025 huko Valdocco, Torino nchini Italia ukihusisha wajumbe zaidi ya 220 wanaowakilisha jumuiya za kisalesiani katika Kanda zote ulimwenguni. Hiki ni kipindi muhimu sana cha mang’amuzi kama bado shirika linaendelea kuishi karama yake katika ulimwegu wa leo, yaani ya kuwahudumia vijana hasa wale masikini na waliosahaulika katika jamii. Mkuu Mpya wa Shirika Padre. Attard alizaliwa Machi 23, 1959, huko Gozo, Malta. Wito wake ulianza kukua alipokuwa katika Seminari Kuu ya Gozo (1975-1978), kisha akaingia katika kipindi cha majaribio ya kisalesiani katika Chuo cha Savio, Dingli, Malta, na baadaye akaendelea na malezi yake ya kitawa katika Novisiati ya Dublin. Tarehe 8 Septemba 1980, aliweka nadhiri zake za kitawa huko Maynooth, Ireland. Baadae alihitimu katika Chuo Kikuu cha Kipapa cha Wasalesian (UPS) kwa shahada ya Taalimungu na baadae Shahada ya Uzamili na Taalimungu kutoka Chuo Kikuu cha Kipapa cha Alfonsianum, Roma.
Alipadrishwa tarehe 4 Julai 1987 na baadaye alihitimu katika Shahada ya Uzamivu kuhusu dhamiri katika mahubiri ya John Henry Newman kutoka Taasisi ya Milltown ya Falsafa na Taalimungu. Miongoni mwa majukumu aliyotekeleza, miaka ya 1980 alihusika katika kuanzisha uwepo wa Wasalesiani nchini Tunisia; alihimiza programu za kujitolea za kimisionari na kuimarisha elimu ya ufundi kupitia miradi kama “Don Bosco Tech Africa na Don Bosco Tech Asia” akiwa mwakilishi wa Wasalesiani katika majukwaa muhimu ya kimataifa; mwaka 2005 alianzisha na kuongoza Taasisi ya mafunzo katika maswala ya Kichungaji huko Malta; na mwaka 2018 aliteuliwa kuwa Mshauri katika Baraza la Kipapa la Walei, Familia na Maisha. Kama Mkuu wa Shirika, Padre Fabio Attard anawaongoza Wasalesiani 13,750 waliowekwa wakfu na waliopo katika Kanda 92 ndani ya nchi 136. Mtu wa wa kwanza kumpongeza Padre Attard alikuwa ni Mwadhama Kardinali Ángel Fernández Artime, ambaye kwa sasa ni Mwenyekiti mwenza wa Baraza la Kipapa la Mashirika ya Kitawa na Kazi za Kitume, na ambaye aliongoza Shirika la Wasalesiani kwa zaidi ya miaka 10 hadi mwaka 2024. Katika kutekeleza majukumu yake kama Mkuu wa Shirika la Wasalesiani wa Don Bosco ulimwenguni, Padre Attard anahitaji wasaidizi katika sekta mbalimbali. Hivyo Mkutano mkuu tarehe 26 Machi 2025 ulimchagua Padre Stefano Martoglio kama Makamu wa Mkuu wa Shirika. Kwa mujibu wa Katiba ya Wasalesiani, Makamu wa Mkuu wa Shirika ni msaidizi wa kwanza wa Mkuu wa Shirika katika uongozi wa Jumuiya na ana mamlaka ya kawaida ya uwakili. Anamwakilisha Mkuu wa Shirika wakati hayupo au anapozuiwa kutekeleza majukumu yake. Pia anahusika hasa na usimamizi wa maisha ya kitawa na nidhamu ya kiroho ndani ya Shirika.
Padre Stefano Martoglio alizaliwa tarehe 30 Novemba 1965 huko Torino, nchini Italia. Mwaka 2008, aliteuliwa kuwa Mkuu wa Kanda yaa Piemonte na Valle d'Aosta (ICP). Ilikuwa katika Mkutano Mkuu wa 27 wa mwaka 2014 ambapo alichaguliwa kwa mara ya kwanza kuwa Mshauri wa Kanda mpya ya Mediteranea, iliyoanzishwa na mkutano huo kupitia muungano wa Kanda mbili za awali, Italia-Mashariki ya Kati na Ulaya Magharibi. Katika Mkutano Mkuu wa 28 wa mwaka 2020, alichaguliwa kwa mara ya kwanza kuwa Makamu wa Mkuu wa Shirika, na kutokana na wadhifa huu, aliongoza Shirika la Salesiani kuanzia tarehe 17 Agosti 2024 hadi Mkutano Mkuu huu, kwa mujibu wa muda uliokubaliwa na Vatican baada ya uteuzi wa Mkuu wa Shirika, Ángel Fernández Artime, kuwa Kardinali. Wengine waliochaguliwa katika kumsaidia mkuu wa Shirika katika vitengo tofauti ni pamoja na Padre Silvio Roggia kama Msaidizi na Mshauri wa Mkuu wa Shirika katika upande wa Malezi. Padre Gabriel Stawowy amechaguliwa kama Mkuu wa kitengo cha usimamizi wa Fedha; Padre Jorge Mario Crisafulli kama Msaidizi na Mshauri wa Mkuu wa Shirika katika sekta ya utume, Padre Fidel Maria Orendain kama Msaidizi na Mshauri wa Mkuu wa shirika katika kitengo cha Mawasiliano Jamii huku Padre Rafael Bejarano amechaguliwa kuwa Msaidizi na Mshauri wa Mkuu wa Shirika katika Utume kwa vijana.
Kutokana na ukubwa wa Bara la Afrika na ukuaji wake katika idadi ya Wasalesiani, Mkutano mkuu umeona ni wakati sahihi sasa kuligawanya na kuwa kanda mbili yaani Afrika Mashariki na Kusini pamoja na Afrika Magharibi na Kati. Hivyo kuwa na viongozi wawili badala ya mmoja kama ilivyokuwa hapo awali. Padre Innocent Bizimana amechaguliwa kuwa Msaidizi na Mshauri wa Mkuu wa Shirika wa kwanza katika ukanda wa Afrika Mashariki na Kusini, huku Padre Alphonce Owoudou amechakuliwa kuwa Msaidizi na Mshauri wa mkuu wa Shirika katika upande wa Afrika Magharibi na Kati. Wengine ni Padre Juan Carlos Perez Godoy katika Ukanda wa Mediterranea, Padre Roman Jachimowicz Ukanda wa Ulaya ya kati na Mashariki, Padre Hugo Orozco Sanchez katika Ukanda wa Amerika, Padre William Matthews Ukanda wa Asia Mashariki na Oceania, Padre Michael Biju Ukanda wa Asia ya Kusini na Padre Hector Gabriel Romero Ukanda wa Amerika Kusini. Katika Ibada ya Misa Takatifu yake ya kwanza kama Mkuu wa Shirika la Wasalesiani ulimwenguni, Padre Fabio Attard, alimshukuru Mungu kwa zawadi na jukumu alilolipata kwa sababu ni wito wa kuandamana na vijana pamoja na familia nzima ya Wasalesiani kwenye safari ya kuelekea nchi ya ahadi ikiongozwa daima na upendo wa Kristo. Vilevile aliwahimiza Wasalesiani waishi kwa imani, tumaini na upendo, huku akisema “Pamoja na Yesu, ndani ya Yesu na kupitia Yesu tunaweza kuendelea kutembea pamoja kwenye safari hii nzuri na ya matumaini.” Tunawaombea majukumu mema viongozi wote waliochaguliwa katika kuongoza Shirika la Wasalesiani wa Don Bosco katika kipindi hiki cha miaka sita (2025-2031). Bikira Maria Mama Msaada wa Wakristo akawe daima Mwombezi wao.