杏MAP导航

Tafuta

Padre Roberto Pasolini Katika mahubiri ya tatu ya Kipindi cha Kwaresima tarehe 4 Aprili 2025 yamenogeshwa na kauli mbiu: “Jifunze Kusimama Tena! Furaha ya Ufufuko.” Padre Roberto Pasolini Katika mahubiri ya tatu ya Kipindi cha Kwaresima tarehe 4 Aprili 2025 yamenogeshwa na kauli mbiu: “Jifunze Kusimama Tena! Furaha ya Ufufuko.” 

Mahubiri ya Kipindi Cha Kwaresima Mwaka 2025: Jifunze Kusimama Tena! Furaha ya Ufufuko!

Mahubiri ya tatu ya Kipindi cha Kwaresima tarehe 4 Aprili 2025 yamenogeshwa na kauli mbiu: “Jifunze Kusimama Tena! Furaha ya Ufufuko.” Kristo Yesu ambaye kwa njia ya ufufuko wake, amewaachia waja wake ushuhuda wa upendo, ukuu, unyenyekevu na furaha isiyokuwa na kifani, kielelezo cha maisha mapya. Amani ni zawadi ya kwanza kutoka kwa Kristo Mfufuka na Fumbo hili kushuhudiwa kwa machozi na Mtakatifu Thoma akisema: “Bwana na Mungu na Mungu wangu."

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Ufufuko wa Kristo Yesu kutoka kwa wafu ni kilele cha ukweli wa imani katika Kristo Yesu aliyeteswa, akafa na hatimaye kufufuka kwa wafu kadiri ya Maandiko Matakatifu. Ni ufunuo wa Uungu wa Kristo Yesu unaowapatia waamini maisha ya uzima mpya na hivyo kuhesabiwa haki pamoja na kufanywa wana wateule wa Mungu. Ufufuko wa Kristo ni msingi wa ufufuko wa miili na uzima wa milele ijayo! Ndiyo maana Pasaka ni Sherehe kubwa katika Kanisa. Hii ni Sherehe ya upendo, huruma na msamaha wa Baba wa milele unaofumbatwa katika Fumbo la Msalaba. Dominika ya Pasaka, Kanisa linamshangilia Kristo Mfufuka kwa “Sekwensia ya Pasaka” yaani “Kristo Pasaka yetu aliyechinjwa sadaka, tumaini la watu wake amefufuka na amewatangulia mjini Galilaya. Kwa njia ya Fumbo la Pasaka, wote wamehesabiwa haki, kwa vile wamefufuka katika Kristo Yesu, wanapaswa kuyatafuta na kuyaambata yale ya mbinguni, ushuhuda wa imani tendaji. Kwa wale waliozaliwa upya kwa kuuvua utu wao wa kale, wataweza kuhesabiwa haki mbele ya Kristo Yesu. Baba Mtakatifu Francisko anawataka waamini kuondokana na unafiki katika maisha yao kwa kuishi na kutenda mema na pale wanapotumbukia dhambini, wawe na ujasiri wa kusimama tena na kukimbilia huruma na upendo wa Mungu katika maisha yao, ili hatimaye, wao pia waweze kuwa ni vyombo na mashuhuda wa huruma ya Mungu kwa wale wanaoteseka na kudhalilishwa kwa utupu; vita, njaa, magonjwa; watu wanaokosa mahitaji yao msingi, watu wanaoishi katika upweke na uvuli wa mauti.

Jifunze Kusimama Tena! Furaha ya Uufufuko
Jifunze Kusimama Tena! Furaha ya Uufufuko

Baba Mtakatifu anaendelea kufafanua kwamba, kwa upya wa maisha ndani ya Kristo Yesu, Wakristo wanaweza kuwa ni mashuhuda wa Injili ya matumaini, alama ya maisha mapya na ufufuo. Wakristo wawe na ujasiri wa kumwachia Kristo Yesu, aweze kuosha na kutakasa macho ya imani, ili kuona na kutenda vyema, kama ushuhuda wenye mvuto na mashiko kwa Kristo Mfufuka. Kwa kuishi vyema Fumbo la Mateso, Kifo na Ufufuko wa Kristo Yesu kutoka kwa wafu, Baba Mtakatifu anawaalika waamini kuiga mfano wa maisha ya Bikira Maria aliyefuatana na Mwanaye Mpendwa katika Njia yake ya Msalaba, akateseka sana pamoja naye hadi kudiriki kusimama chini ya Msalaba bila kumwonea aibu! Ni Mama ambaye, moyo wake ulisheheni furaha isiyokuwa na kipimo, kwa Fumbo la Ufufuko wa Kristo kutoka wafu. Maadhimisho ya Fumbo la Pasaka, yawawezeshe waamini kushiriki kikamilifu Fumbo hili la Wokovu ili waweze kupyaisha maisha yao! Ni katika muktadha huu, Mahubiri ya Kipindi cha Kwaresima kwa Mwaka 2025 yanaongozwa na Padre Roberto Pasolini, OFM Cap., Mhubiri wa Nyumba ya Kipapa na kuongozwa na kauli mbiu “Kutia nanga katika Kristo” Kukita mizizi na kusimikwa katika tumaini la maisha mapya.” Mahubiri haya ni kwa ajili ya waamini wote wanaojisikia kutaka kuboresha maisha yao ya kiroho na yanaanza saa 3:00 kwa Saa za Ulaya.

Padre Roberto Pasolini, Mhubiri wa Nyumba ya Kipapa
Padre Roberto Pasolini, Mhubiri wa Nyumba ya Kipapa   (VATICAN MEDIA Divisione Foto)

Katika mahubiri ya tatu ya Kipindi cha Kwaresima tarehe 4 Aprili 2025 yamenogeshwa na kauli mbiu: “Jifunze Kusimama Tena! Furaha ya Ufufuko.” Huu ni mwaliko wa kuendelea kujifunza kutoka kwa Kristo Yesu ambaye kwa njia ya ufufuko wake, amewaachia waja wake ushuhuda wa upendo, ukuu, unyenyekevu na furaha isiyokuwa na kifani, kielelezo cha maisha mapya na uzima wa milele. Amani ni zawadi ya kwanza kutoka kwa Kristo Mfufuka na Fumbo hili kushuhudiwa kwa machozi na Mtakatifu Thoma akisema: “Bwana wangu na Mungu wangu” (Yn. 20:28.) Hii ni kiri kuu ya Imani ya Mtume Thoma aitwaye pacha kuwa Kristo mfufuka ni mtu kweli na ni Mungu kweli. Fumbo la Pasaka, yaani mateso, kifo na ufufuko wa Kristo Yesu kwa wafu linaamsha tena imani kwa Mitume na wafuasi wa Kristo Yesu.Siku ya kwanza ya Juma, asubuhi na mapema, Kristo Yesu akamtokea Maria Magdalena na kumshuhudia kuwa ni chemchemi ya huruma ya Mungu kwa mwanadamu, kiasi cha kudondosha chozi la furaha ya Pasaka. Mtakatifu Maria Madgalena alipata heshima ya kuwa ni mfuasi wa kwanza kushuhudia kufufuka kwa Kristo Yesu kutoka kwa wafu, "testis divinae misericordiae", kama Papa Gregory Mkuu anavyofafanua. Yesu Mfufuka akamwonjesha huruma na upendo wake; chemchemi ya maisha mapya, dhidi ya Eva aliyesababisha kifo. Yesu akamwambia Maria Magdalena “Non me tangere”, yaani “Yesu akamwambia: Usinishike; kwa maana sijapaa kwenda kwa Baba. Lakini enenda kwa ndugu zangu ukawaambie, Ninapaa kwenda kwa Baba yangu naye ni Baba yenu, kwa Mungu wangu naye ni Mungu wenu.” Yn 20:17. Huu ni wito pia kwa Kanisa kuambata imani na kuendelea kuamini ubinadamu unaojionesha katika Fumbo la Mungu. Fumbo la Pasaka ni ushuhuda wa binadamu aliyeumbwa kwa sura na mfano wa Mungu, changamoto na mwaliko wa kusimama tena, pale anapoteleza na kuanguka, ili kuonja tena ile furaha ya Pasaka, yaani ufufuko wa Kristo Yesu kwa wafu. Kristo Yesu aliliandaa Fumbo la Pasaka kwa ufundi na ustadi mkubwa, ili kupandikiza na kukuza mbegu ya maisha na uzima wa milele: Toba na wongofu wa ndani, ili kuwa kweli ni mashuhuda upendo wa Mungu.

Ufufuko wa wa Kristo ni kiini cha imani, matumaini na mapendo
Ufufuko wa wa Kristo ni kiini cha imani, matumaini na mapendo   (VATICAN MEDIA Divisione Foto)

Padre Roberto Pasolini, OFM Cap., anasema katika muktadha wa maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 2025 ya Ukristo kupita katika Lango la Jubilei ni mwaliko wa kuacha dhambi nyuma, ili kupata maisha na uzima wa milele unaobubujika kutoka kwa Kristo Yesu, Lango la imani, matumaini na mapendo, kwa kuendelea kubaki imara na thabiti katika Kristo Yesu, kwa njia ya Neno na Sakramenti zake na hasa Sakramenti ya Ubatizo, tayari kuwaongoza wengine kutambua na kuambata upendo wa Mungu. Fumbo la Pasaka ni kiini cha imani ya Kanisa, mwaliko wa kutafuta na kuambata yale mambo msingi yanayowaunganisha na Kristo Yesu, tayari kutangaza na kushudia huruma na upendo wa Mungu. Kwa mateso, kifo na ufufuko wake kwa wafu, Kristo Yesu amewaachia waja wake ushuhuda wa upendo, ukuu, unyenyekevu na furaha isiyokuwa na kifani, kielelezo cha maisha mapya na uzima wa milele. Huu ni mwaliko kwa waamini kutangaza na kushuhudia Ufufuko wa Kristo Yesu kwa watu wa Mataifa kama walivyofanya wale wanawake na wale Mitume wa Yesu. Rej. Mk 16:8; 9-20. Itakumbukwa kwamba, Fumbo la Ufufuko ni kielelezo cha huruma na upendo wa Mungu kwa binadamu na wala si ushuhuda wa nguvu ya Mungu. Huu ni upendo kama unavyoshuhudiwa na Mtakatifu Paulo katika utenzi wa upendo kati ya ndugu 1Kor 13: 1-13. Furaha ya kweli inasimikwa katika upendo, amani na utulivu wa ndani, kielelezo cha Kristo Mfufuka.

Waamini wanaitwa na kutumwa kutangaza Fumbo la Pasaka
Waamini wanaitwa na kutumwa kutangaza Fumbo la Pasaka   (VATICAN MEDIA Divisione Foto)

Padre Roberto Pasolini, OFM Cap., anasema Ufufuko wa Kristo Yesu ni chemchemi ya maisha mapya na uzima wa milele; furaha ya kweli kama ilivyokuwa kwa Mitume wake waliokuwa wamejifungia ndani kwa woga na kuamua kuwapatia amani kama zawadi ya Fumbo la Pasaka. Rej Yn 20: 19-20. Hawa ni wale Mitume waliomkana na kumkimbia siku ile alipokamatwa, akateswa na kufa Msalabani. Anawakirimia tena zawadi ya amani na upatanisho; umoja, ushirika na mshikamano, chemchemi ya furaha ya Pasaka ya Bwana na chanzo cha furaha ya kweli, inayopaswa kutangazwa na kushuhudiwa kwa watu wa Mataifa. Akawapatia zawadi ya Roho Mtakatifu na uwezo wa kuwaondolea watu dhambi zao. Rej. Yn 20: 21-23.Mitume wanatumwa kuwa ni vyombo na mashuhuda wa toba, wongofu wa ndani na msamaha wa dhambi, utume ambao unaendelea kutekelezwa na Mama Kanisa. Mtakatifu Thoma hakuwepo wakati Kristo Yesu alipowatokea Mitume kwa mara ya kwanza, akataka kuona na kugusa Madonda Matakatifu ya Kristo Yesu na alipowatokea tena, alikiri akisema: “Bwana wangu na Mungu wangu” (Yn. 20:28.) Hii ni kiri kuu ya Imani ya Mtume Thoma aitwaye pacha kuwa Kristo mfufuka ni mtu kweli na ni Mungu kweli, kielelezo cha hali ya juu kabisa cha imani. Fumbo la Pasaka, yaani mateso, kifo na ufufuko wa Kristo Yesu kwa wafu linaamsha tena: Matumaini, ujasiri, upendo na imani kwa Mitume na wafuasi wa Kristo Yesu katika ujumla wao. Hata leo hii, Kristo Yesu anatembelea kujifunua katika familia na jumuiya za waamini katika Neno, Sakramenti na historia ya kila mmoja wao, jambo la msingi ni kutambua uwepo wake angavu kati yao!

Fumba la Pasaka ni chemchemi ya maisha mapya na uzima wa milele
Fumba la Pasaka ni chemchemi ya maisha mapya na uzima wa milele   (Vatican Media)

Padre Roberto Pasolini, OFM Cap., anasema Ufufuko wa Kristo Yesu unaamsha tena matumaini kwa Maria Madgalena na Wanafunzi wa Emau waliobahatika kuandamana na Kristo Yesu katika safari yao ya matumaini ya Kikristo bila kumtambua kwani macho yao yalikuwa yamefumbwa! Lakini, wakamtambua Yesu wakati wa kuumega mkate na hapo hapo akatoweka tena machoni pao! Nao wakaambiana, Je, mioyo yetu haikuwaka ndani yetu pale alipokuwa akizungumza na kufafanua Maandiko Matakatifu? Wanafunzi wa Emau walikuwa na majonzi makubwa mioyoni mwao kwani Fumbo la Msalaba, yaani mateso na kifo cha Kristo Yesu liliwaachia machungu makubwa kwani liliyeyusha matumaini na maisha yao; wakaonekana kushindwa vita hata kabla ya kuianza. Rej. Lk 24: 36-43. Wanafunzi wa Emau wakamtambua Kristo Yesu Mfufuka wakati wa kuumega mkate, maisha yakawa tena ni sherehe iliyopyaishwa kwa neema ya uwepo angavu wa Kristo Yesu kati yao na hivyo kufukuzia mbali: hofu, mashaka na uvuli wa mauti kwa mwanga wa Habari Njema ya Wokovu. Rej. Lk 24: 25-27. Mateso, kifo na ufufuko wa Kristo Yesu kwa wafu ni kielelezo cha huruma na upendo wa Mungu kwa binadamu. Mkate ukawa ni ishara ya matumaini na uwepo wa Kristo Yesu kati yao, ukpyaisha mtazamo wao na hivyo kuwa tayari kulipokea, kuliishi na kulishuhudia Fumbo la Pasaka, kielelezo cha upendo wa Mungu kwa mwanadamu. Waamini wanahimizwa kugundua tena ndani mwao ule moto wa imani, matumaini na mapendo ambao haukuzimwa na maumivu ya mateso na kifo cha Kristo Yesu, tayari kukumbatia na kuambata Fumbo la Ufufuko katika maisha yao, hazina na amana ya thamani; kwa kuumbwa upya na Roho Mtakatifu, ili kuendelea kuwa ni sura na mfano wa Mungu. Kristo Yesu aliwaandaa wafuasi wake ili kupokea Fumbo la Pasaka kama chemchemi ya imani, matumaini na mapendo, kwa kuanzisha mahusiano na mafungamano ya dhati kabisa na wafuasi wake, changamoto na mwaliko kwa wafuasi wa Kristo Yesu kuwa ni vyombo na mashuhuda wa upendo mkuu wa Kristo Yesu unaobubujika kutoka katika Fumbo la Pasaka.

Mahubiri ya Kwaresima ni kwa ajili ya watu wote
Mahubiri ya Kwaresima ni kwa ajili ya watu wote   (Vatican Media)

Padre Roberto Pasolini, OFM Cap., Mhubiri wa Nyumba ya Kipapa ameihitimisha mahubiri yake ya tatu katika Kipindi cha Pasaka kwa sala ifuatayo: “Ee Baba, ambaye kwa njia ya Mwana wako wa pekee ulishinda mauti na kutufungulia njia ya uzima wa milele, utujalie sisi tunaoadhimisha ufufuko wa Bwana, tupate kuzaliwa upya katika nuru ya uzima, tufanywe upya na Roho wako Mtakatifu. Kwa Bwana wetu Yesu Kristo.”

Mahubiri 3 ya Kwaresima
04 Aprili 2025, 15:20