杏MAP导航

Tafuta

Baba Mtakatifu, Jumatano tarehe 16 Aprili 2025 ameanzisha mzungumko mpya wa Katekesi kuhusu mifano ya Injili na ameanza kwa mfano wa Baba Mwenye huruma. Kristo Yesu ni ufunuo wa huruma ya Mungu. Baba Mtakatifu, Jumatano tarehe 16 Aprili 2025 ameanzisha mzungumko mpya wa Katekesi kuhusu mifano ya Injili na ameanza kwa mfano wa Baba Mwenye huruma. Kristo Yesu ni ufunuo wa huruma ya Mungu. 

Katekesi Kuhusu Yesu Tumaini Letu: Baba Mwenye Huruma

Ni katika muktadha wa maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 2025 ya Ukristo, Kristo Tumaini letu, Papa tarehe 16 Aprili 2025 ameanzisha mzungumko mpya wa Katekesi kuhusu mifano ya Injili na ameanza kwa mfano wa Baba Mwenye huruma, kama unavyosimuliwa na Mwinjili Luka.Hii ni mifano inayokita ujumbe wake katika uhalisia wa maisha ya kila siku na kwamba kiini cha Injili ya Luka ni Baba Mwenye Huruma, yaani Mwenyezi Mungu mwingi wa huruma na mapendo!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Katekesi kuhusu: “Roho Mtakatifu na Bibi Arusi. Roho Mtakatifu anawaongoza watu wa Mungu kuelekea kwa Yesu, tumaini letu” ni sehemu ya Maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 2025 ya Ukristo yanayonogeshwa na kauli mbiu “Peregrinantes in spem” yaani “Mahujaji wa matumaini.” “Basi palikuwa na mtu mmoja wa Mafarisayo, jina lake Nikodemo, mkuu wa Wayahudi. Huyo alimjia usiku, akamwambia, Rabi, twajua ya kuwa u mwalimu, umetoka kwa Mungu; kwa maana hakuna mtu awezaye kuzifanya ishara hizi uzifanyazo wewe, isipokuwa Mungu yu pamoja naye. Yesu akajibu, akamwambia, Amin, amin, nakuambia, Mtu asipozaliwa mara ya pili, hawezi kuuona ufalme wa Mungu. Nikodemo akamwambia, Awezaje mtu kuzaliwa, akiwa mzee?” Yn 3:1-3. Hii ni sehemu ya Maandiko Matakatifu iliyoongoza Katekesi ya Baba Mtakatifu Francisko, Jumatano tarehe 19 Machi 2025 na kunogeshwa na kauli mbiu “Hamna budi kuzaliwa mara ya pili.” Baba Mtakatifu amekwisha kugusia kuhusu yule Mwanamke Msamaria aliyekutana na Kristo Yesu akamwomba maji ya uzima wa milele. Baba Mtakatifu Francisko katika mwanga wa Injili kuhusu: Kodi, Sheria, Kutopendelea, Ukweli na Uwazi, anasema haya ni mambo ambayo yanaongoza kila siku maisha ya watu wa Mungu. Watawala wote wa dunia, walianzisha kodi na kama ilivyokuwa hata nyakati za Kristo Yesu. Warumi katika utawala wa Kaisari waliwatoza watu kodi, kazi iliyotekelezwa na watoza ushuru na kati yao alikuwepo Zakayo, mkubwa mmoja kati ya watoza ushuru naye alikuwa tajiri. Rej. Lk 19:1-9.

Kristo Yesu ni Ufunuo wa huruma na upendo wa Mungu
Kristo Yesu ni Ufunuo wa huruma na upendo wa Mungu   (Vatican Media)

Baba Mtakatifu Francisko anasema, ni furaha, utulivu na amani ya ndani, baada ya mwamini kujipatanisha na nafsi yake, Mwenyezi Mungu, jirani pamoja na mazingira nyumba ya wote. Rej. Lk 15:1-3; 11-32. Sehemu hii ya Injili kwa wengi inajulikana kama “Injili ya Mwana Mpotevu.” Lakini inapaswa kuitwa “Injili ya Baba Mwenye Huruma” kwani ndiye mhusika mkuu anayewangojea watoto wake wawili, waweze kutubu na kurejea tena nyumbani, ili aweze kuwafanyia sherehe.Baba Mwenye huruma ni kielelezo cha Mungu Baba Mwenyezi anayesamehe daima, ambaye yuko tayari kuwapokea na kuwafanyia watoto wake sherehe, hata kama wametenda dhambi kubwa kiasi gani. Jambo la msingi ni: toba na wongofu wa ndani, tayari kuambata njia ya maisha mapya. Kristo Yesu ni ufunuo wa huruma na upendo wa Mungu, unaowatafuta wale wote waliopotea. Mifano yote mitatu katika Injili ya Luka15:1-32, inaonesha mapungufu katika maisha ya mwanadamu: Mchungaji amempoteza kondoo, mwanamke amepoteza shilingi na Baba mwenye huruma amempoteza Mwana, ingawa alikuwa na mwanae mkubwa, lakini akapiga moyo konde na kuendelea kumsubiri. Hiki ni kielelezo cha mtu anayependa kwa dhati, kwani hataki hata mara moja chochote kile kipotee. Baba Mtakatifu anasema huruma ya Mungu ndiyo mahangaiko ya upendo wake kwa binadamu dhaifu na mdhambi. Huruma hii inamsumbua na “kumnyima usingizi” kiasi cha kuacha yote na kuanza kumtafuta binadamu dhaifu na mdhambi, ili akimpata aweze kumbeba na kumweka mabegani mwake, kielelezo cha Baba mwenye huruma na mapendo thabiti, au Mama anayeteseka kwa kukosekana kwa mtoto wake mpendwa.

Waamini wajenge utamaduni wa kukimbilia huruma ya Mungu
Waamini wajenge utamaduni wa kukimbilia huruma ya Mungu   (Vatican Media)

Ni katika muktadha wa maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 2025 ya Ukristo, Kristo Tumaini letu, Baba Mtakatifu, Jumatano tarehe 16 Aprili 2025 ameanzisha mzungumko mpya wa Katekesi kuhusu mifano ya Injili na ameanza kwa mfano wa Baba Mwenye huruma, kama unavyosimuliwa na Mwinjili Luka 15: 32. Hii ni mifano inayokita ujumbe wake katika uhalisia wa maisha ya kila siku na kwamba kiini cha Injili ya Luka ni Baba Mwenye Huruma, yaani Mwenyezi Mungu mwingi wa huruma na mapendo na kwamba, Injili inataka kuwapatia watu wa Mungu matumaini katika maisha kwani Mwenyezi Mungu daima yuko katika harakati za kuwatafuta waja wake, kama Kondoo au shilingi iliyopotea, kama Baba mwenye huruma na watoto wake wawili. Upendo unawajibisha anasema Baba Mtakatifu, kama ilivyokuwa kwa yule kijana mdogo au hata kwa Kaka mkubwa alivyopotea katika uchoyo na ubinafsi wake na hivyo kuishia kuishi vibaya. Kijana mdogo kama ilivyo kwa watu wengi alikuwa na kiu ya upendo wa dhati, kwani kwa hakika upendo ni zawadi inayopaswa kuheshimiwa na kuthaminiwa. Kijana mdogo alitambua thamani ya upendo pale njaa kuu ilipoingia katika nchi ile yule kijana naye akaanza kuhitaji, akatubu kutoka katika undani wa maisha yake na kuamua kurejea tena nyumbani kwao, ili kuonja tena upendo wa Baba yake, akiwa ametubu, tayari kuzaliwa tena upya, na hivyo kuonja nguvu za huruma na upendo kutoka kwenye mikono ya msamaha.

Huruma ya Mungu ni chemchemi ya furaha, amani na utulivu wa ndani
Huruma ya Mungu ni chemchemi ya furaha, amani na utulivu wa ndani   (Vatican Media)

Kaka mkubwa anawawakilisha wale Wakristo waaminifu waliodhani kwamba wamebaki nyumbani, huku wakiendelea kumtumikia Baba yao, kumbe, alikuwa ni mtu ambaye alikuwa mbali sana na moyo wa Baba yake! Hata kijana mkubwa pengine alitamani hata yeye kutoroka nyumbani kwao, lakini akabakia nyumbani akiwa katika mahusiano tenge na Baba yake. Matokeo yake ana onesha chuki na hasira iliyokuwa ndani mwake, kiasi cha kuitapika alipo rejea yule kijana mdogo na hivyo hakutaka kushiriki ile furaha ya Baba mwenye huruma baada ya kumpata Mtoto wake mdogo akiwa salama salimini. Baba mwenye huruma anataka kutoka ndani ya moyo wake, anataka kuwaonjesha huruma yake. Ana mwalika kijana mkubwa kuingi ndani, kwani mlango daima uko wazi, kielelezo cha matumaini, hata kwa waamimini wa nyakati hizi, kwani Mwenyezi Mungu daima anawasubiri. Baba Mtakatifu Francisko mwishoe anawauliza maswali waamini huku akiwataka kuchagua picha kati ya wahusika watatu kwenye sehemu ya simulizi hilì. Baba Mtakatifu anawaomba waamini wamwombe Mungu nehema ya uatakaso ili hatimaye waweze kurudi nyumbani kwa Baba!

Baba Mwenye Huruma
16 Aprili 2025, 14:13