Kardinali Parolin aliongoza Rozari mbele ya Kanisa Kuu la Mtakatifu Maria Mkuu!
Na Angella Rwezaula - Vatican.
Kardinali Pietro Parolin, Katibu wa Vatican, usiku saa 3.00 kamili masaa ya Ulaya, Jumanne tarehe 22 Aprili 2025 aliongoza Rozari kwa ajili ya kumwombea Papa Francisko ikiwa ni mfululizo wa sala hiyo mbele ya Kanisa Kuu la Kipapa la Bikira Maria Mkuu, Roma. Katika maneno yake mwanzoni mwa liturujia hiyo, Kardinali Parolin alikumbusha kuwa: “Kama mtume Paulo anavyotukumbusha, tunaalikwa kuinua macho yetu kuelekea mbinguni na kumtafakari Kristo aliyeketi mkono wa kuume wa Mungu na kutazama mbinguni ili kufurahia uzima wa milele hasa katika sala ya jioni hii, tunapomkabidhi Baba Mtakatifu wetu mpendwa kwa Maria Mtakatifu Afya ya Waroma.
Akitambulisha tendo la kwanza kati ya matano ya Utukufu kwa waamini waliokusanyika mbele ya uwanja wa Basilika hiyo Kardinali Parolin alisema: "Maria mtetezi mbele ya Baba, atuombee.” Na kwa kuhitimisha Kardinali Parolin alikumbusha jinsi ambavyo Papa Francisko alivyotoa mateso yake mwishoni mwa maisha yake kwa ajili ya amani duniani na udugu kati ya watu."