杏MAP导航

Tafuta

Alhamisi Kuu 2025: Mapadre ni Mashuhuda wa Injili ya Matumaini kwa watu wa Mungu Alhamisi Kuu 2025: Mapadre ni Mashuhuda wa Injili ya Matumaini kwa watu wa Mungu  (VATICAN MEDIA Divisione Foto)

Alhamisi Kuu 2025: Mapadre Ni Vyombo Na Mashuhuda wa Injili ya Matumaini

Baba Mtakatifu Franciskoamekazia kuhusu: Mapadre kuwa ni vyombo na mashuhuda wa matumaini yanayosimikwa katika huduma, changamoto na mwaliko wa toba na wongofu wa ndani, ili kuwa kweli ni watangazaji wa matumaini na hivyo kuendelea kuliishi Fumbo la Pasaka, yaani: Mateso, kifo na ufufuko wa Kristo. Mapadre wasimike maisha na utume wao katika Neno la Mungu na kwamba, Roho Mtakatifu ni mhimili mkuu wa mchakato wa uinjilishaji wa watu wa kina.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Ibada ya Misa Takatifu kwa ajili ya kuweka wakfu Krisma ya Wokovu, ni ufunuo wa Kanisa, Fumbo la Mwili wa Kristo unaofumbatwa katika huduma, karama na neema mbalimbali za Roho Mtakatifu katika hija ya maisha yake kumwendea Kristo Yesu. Mafuta ni alama ya ushirika, furaha, upendo na mshikamano. Ni alama ya imani inayoimarisha vifungo vya upendo kwa njia ya Roho Mtakatifu ili kutangaza na kushuhudia: Ukuu, uzuri na utakatifu wa familia ya Mungu. Hii ni changamoto kwa waamini kuhakikisha kwamba, kamwe hawatindikiwi na mafuta ya neema ya imani, matumaini na mapendo. Huu ni mwaliko wa kuboresha maisha ya kiroho kwa kujikita katika: Sala, Neno la Mungu, Sakramenti za Kanisa, Matendo adili na matakatifu na kwamba, Msalaba uwe ni kimbilio na ngao ya maisha ya mwamini. Kardinali Domenico Calcagno, Rais mstaafu wa Utawala wa Amana ya Kiti cha Kitume kwa niaba ya Baba Mtakatifu Francisko, Alhamisi kuu tarehe 17 Aprili 2025 ameongoza Ibada ya Misa Takatifu kwa ajili ya kuweka wakfu Mafuta ya Krisma ya Wokovu, “Sacrum Chrisma.” Ni mafuta yanayowaweka wakfu Wakristo, ili hatimaye, kushiriki: Ukuhani, Unabii na Ufalme wa Kristo Yesu. Ibada hii ya Misa Takatifu inalionesha Kanisa kuwa ni Sakramenti ya Wokovu, inayotakasa. Kardinali Domenico Calcagno, amebariki: Mafuta ya Wakatekumeni na Mafuta ya Wagonjwa pamoja kuweka wakfu Mafuta ya Krisma ya Wokovu; mafuta yanayotumika kwa ajili ya kuwapaka waamini wakati wanapopokea Sakramenti ya Ubatizo, Sakramenti ya Kipaimara na wanapowekwa wakfu kuwa Mapadre na Maaskofu.

Mafuta Matakatifu: Krisma ya Wokovu, Mafuta ya Wagonjwa na Wakatekumeni
Mafuta Matakatifu: Krisma ya Wokovu, Mafuta ya Wagonjwa na Wakatekumeni   (VATICAN MEDIA Divisione Foto)

Kwa vile Mapadre ni waadhimishaji na wagawaji wa Mafumbo ya Kanisa, wanapaswa kujitakatifuza katika maisha yao, kwa kuambatana na Mungu kwa njia ya Sala, Tafakari ya Neno la Mungu na Maisha ya Kisakramenti. Haya ni mafuta yanayotumika pia kutabaruku Kanisa kwa kupaka Altare na kuta za Kanisa kuonesha kwamba, Jengo hili, yaani Kanisa limetengwa kwa ajili ya maadhimisho ya mambo matakatifu ya Mungu, yaani Mafumbo ya Kanisa. Mafuta haya ni ishara ya uwepo wa Roho Mtakatifu. Haya ni mafuta yaliyotiwa manukato na kuwekwa wakfu na Askofu mahalia, huashiria paji la Roho Mtakatifu kwa mbatizwa mpya. Amekuwa Mkristo, yaani “Mpakwa” na Roho Mtakatifu na hatimaye, ameingizwa katika Kristo Yesu, ambaye amepakwa mafuta kama: Kuhani, Nabii na Mfalme. Hii ni siku ambayo Mama Kanisa amebariki pia Mafuta ya Wagonjwa: “Oleum infirmorum.” Mafuta haya hutumika katika Sakramenti ya Mpako wa wagonjwa na hutolewa kwa wagonjwa walio katika hatari kubwa, kwa kuwapaka mafuta usoni na mikononi; mafuta yaliyobarikiwa itakiwavyo, yaliyokamuliwa kutoka katika matunda ya Mizeituni kwa kusema mara moja tu: “Kwa Mpako huu Mtakatifu na kwa pendo lake kuu, Bwana akujaze kwa nguvu ya Roho Mtakatifu. Akuondoe katika enzi ya dhambi, akuweke huru. Kwa wema wake akupe nafuu katika mateso yako na kukujalia neema.” Ni mafuta yanayoweza kuleta: faraja, msamaha wa dhambi na uponyaji kadiri ya mapenzi ya Mungu pamoja na kumwondolea dhambi mgonjwa ambaye hawezi kuungama.

Mafuta ya Kristo ya Wokovu: Ubatizo, Kipaimara  na Daraja Takatifu
Mafuta ya Kristo ya Wokovu: Ubatizo, Kipaimara na Daraja Takatifu   (VATICAN MEDIA Divisione Foto)

Mafuta ya Wakatekumeni: “Oleum Catechumenorum” ni ishara ya nguvu ya Kristo Yesu kwa waamini wanaojiandaa kupokea Sakramenti ya Ubatizo, ili waweze kupata uwezo wa kupambana na vishawishi pamoja na dhambi. Ni mafuta yanayowaandaa Wakatekumeni kupambana dhhidi ya uovu na hivyo kuwakirimia waamini neema ya awali kabla ya kupokea Sakramenti ya Ubatizo. Mama Kanisa anafundisha kwamba, Kristo Yesu aliwapenda watu wake upeo na alipokuwa anakaribia “Saa yake” ili kutoka hapa ulimwenguni na kurudi kwa Baba yake wa mbinguni, Siku ile ya Alhamisi kuu, walipokuwa wakila, aliwaosha Mitume wake miguu yao na kuwapatia Amri ya upendo inayomwilishwa katika huduma ya upendo, hasa kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Akataka pia kuwapatia amana ya upendo huu na kuendelea kubaki kati yao na kuendelea kuwashirikisha Fumbo la Pasaka, aliweka Sakramenti ya Ekaristi Takatifu, kielelezo cha sadaka, shukrani, kumbukumbu endelevu na uwepo wake kati yao katika alama ya Mkate na Divai!

Alhamisi Kuu: Ekaristi Takatifu, Daraja na Huduma
Alhamisi Kuu: Ekaristi Takatifu, Daraja na Huduma   (Vatican Media)

Alhamisi kuu ni Siku ambayo Mama Kanisa anakumbuka siku ile Kristo Yesu alipoweka Sakramenti ya Daraja Takatifu ya Upadre inayopata utimilifu wake katika Daraja ya Uaskofu. Hii ni siku ambayo Kristo Yesu aliwaweka Mitume wake, wawe wafuasi wake wa karibu, tayari kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu. Kumbe, hii ni siku ya kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa zawadi ya Daraja Takatifu ya Upadre na kuwashukuru Mapadre kwa sadaka na majitoleo yao licha ya dhambi na mapungufu yao ya kibinadamu. Huu ni mwaliko kwa Mapadre kuishi mintarafu Daraja Takatifu ya Upadre, kwa njia ya ushuhuda wa maisha na utume wa Kipadre, wakitambua kwamba, kwa njia ya Daraja Takatifu ya Upadre wanashirikishwa maisha na utume wa Kristo Yesu, ili kufundisha, kuongoza na kuwatakatifuza watu wa Mungu. Mapadre wanapaswa kusimama kidete ili kuweza kuishi fadhila za maisha na utume wa Kipadre, kwa kujitahidi kuishi kama Kristo mwingine “Alter Christus” ili kwamba, waamini waweze kumtambua Kristo Yesu ndani mwao. Hii pia ni Siku ambayo Mapadre wanarudia tena ahadi pamoja na viapo vyao, jambo wanalopaswa kulifanya kutoka katika sakafu ya nyoyo zao, ili kuendelea kuimarisha urika wao pamoja na Maaskofu wao. Kardinali Domenico Calcagno, Rais mstaafu wa Utawala wa Amana ya Kiti cha Kitume katika mahubiri yaliyoandaliwa na Baba Mtakatifu Francisko kama sehemu ya maadhimisho ya Alhamisi kuu kwa Mwaka 2025 amekazia kuhusu: Mapadre kuwa ni vyombo na mashuhuda wa matumaini yanayosimikwa katika huduma kwa watu wa Mungu, changamoto na mwaliko wa toba na wongofu wa ndani, ili kuwa kweli ni watangazaji wa matumaini na hivyo kuendelea kuliishi Fumbo la Pasaka, yaani: Mateso, kifo na ufufuko wa Kristo. Mapadre wasimike maisha na utume wao katika Neno la Mungu na kwamba, Roho Mtakatifu ni mhimili mkuu wa mchakato wa uinjilishaji wa kina unaogusa mahitaji ya mtu mzima: kiroho na kimwili. Mapadre katika ulimwengu mamboleo wanaendelea kukabiliana na changamoto pevu, kumbe, ni dhamana na wajibu wa waamini kumwomba Bwana wa mavuno ili apeleke watenda kazi wema, watakatifu, wenye ari, moyo na bidii ya kazi, ili kweli waweze kuwa ni mashuhuda na vyombo vya faraja na furaha kwa watu wa Mungu.

Alhamisi Kuu: Ahadi za Kipadre
Alhamisi Kuu: Ahadi za Kipadre   (VATICAN MEDIA Divisione Foto)

Kardinali Domenico Calcagno anasema, Kristo Yesu ni Alfa na Omega, Mwanzo na Mwisho na kwamba, nyakati zote ni zake; ni ufunuo wa matumaini na upendo unaosimikwa katika Fumbo la Msalaba. Ni Kristo Yesu pekee anayeweza kukifungua Kitabu cha Historia na kukisoma. Alhamisi kuu, Mapadre wanarudia tena viapo na ahadi zao za Kipadre, tayari kumsikiliza Kristo Yesu anayewaita na kuwatuma kuwa ni vyombo na mashuhuda wa matumaini kwa watu wa Mungu, mwaliko kwa Mapadre ni kuendelea kusoma kitabu cha maisha yao bila woga. Kristo Yesu anafanya yote kuwa ni mapya, hivyo Mapadre wanapaswa kuwa tayari kusoma maisha na utume wao wa Kipadre kama huduma kwa watu wa Mungu. Maadhimisho ya Jubilei ya Mwaka 2025 ya Ukristo ni mwaliko kwa Mapadre kutubu na kumwongokea Mungu, tayari kuwa ni vyombo na mashuhuda wa Injili ya matumaini, daima wakiendelea kuwa ni waaminifu wa upendo wa Kristo Yesu unaokoa; kwa kujisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya huduma kwa maskini na watu wa Mungu katika ujumla wao! Imani ya Kanisa inasimikwa katika Fumbo la Pasaka, yaani: mateso, kifo na ufufuko wa wafu, mwaliko kwa Mapadre kuendelea kujichimbia katika maisha na utume wa Kristo Yesu ili waweze kuzaa matunda mema: kielelezo cha mazoea mazuri yanayopata chimbuko lake kwa kupenda kusoma, kutafakari na kulimwilisha Nebo la Mungu katika uhalisia wa vipaumbele vya maisha, daima Kristo Yesu akiwa ni rejea ya maisha na utume wao wa Kikuhani. Huduma ya Kipadre ipate chanzo na kilele chake katika Maandiko Matakatifu ambamo kila Padre anao ukurasa wake wa maisha. Wawasaidie jirani zao, kutafuta na hatimaye kuambata kurasa za maisha yao, ili kujiaminisha na kujizamisha katika huruma na upendo wa Mungu.

Alhamisi kuu ni Ufunuo wa Kanisa la Kristo Yesu
Alhamisi kuu ni Ufunuo wa Kanisa la Kristo Yesu   (VATICAN MEDIA Divisione Foto)

Mapadre watambue kwamba, wameitwa na Kristo Yesu ili kushiriki katika utume wake wa kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu kwa watu wa Mataifa kama ilivyoandikwa katika Injili ya Luka: “Akapewa chuo cha nabii Isaya, akakifungua chuo, akatafuta mahali palipoandikwa, Roho wa Bwana yu juu yangu, kwa maana amenitia mafuta kuwahubiri maskini habari njema. Amenituma kuwatangazia wafungwa kufunguliwa kwao, na vipofu kupata kuona tena, kuwaacha huru waliosetwa, na kutangaza mwaka wa Bwana uliokubaliwa. Akakifunga chuo, akamrudishia mtumishi, akaketi; na watu wote waliokuwamo katika sinagogi wakamkazia macho. Akaanza kuwaambia, Leo maandiko haya yametimia masikioni mwenu.” Lk 4: 17-21.Neno la Mungu linamwilishwa na kuwa ni sehemu ya ukweli wa maisha ya watu wa Mungu, changamoto na mwaliko kwa Mapadre kuwa ni mashuhuda na watangazaji wa Neno la Mungu; wawe ni mashuhuda kwa wale waliojeruhiwa na hivyo kumkataa Roho Mtakatifu; Kuna wale waliovutwa na hatimaye kumezwa na malimwengu; waweze kutambua ndani ya Mapadre nguvu ya Neno la Mungu linalotangazwa na kushuhudiwa kwa kuwa wamepakwa Mafuta, ili ile kazi aliyoianzisha Mungu ndani mwao iweze kupata ukamilifu. Huu ni mwaliko wa kutangaza na kushuhudia Habari Njema kwa wafungwa, vipofu ili wapate kuona tena, kuwaachia huru waliosetwa na kutangaza mwaka wa Bwana.

Alhamisi kuu ni Ufunuo wa kanisa la Kristo Yesu
Alhamisi kuu ni Ufunuo wa kanisa la Kristo Yesu   (VATICAN MEDIA Divisione Foto)

Maneno haya ya Kristo Yesu yawe ni chemchemi ya maisha na utume wao wa Kipadre na kama sehemu ya mchakato wa Uinjilishwaji wao kutoka kwa Kristo Yesu, kwa kuwafungua kutoka katika magereza na upofu wa macho yao, ili kushiriki katika maisha na utume wake kwa njia ya Sakramenti za Kanisa, ili kweli utume wao wa Kipadre uwe ni huduma katika maadhimisho ya Jubilei sanjari na ujenzi wa Ufalme wa Mungu. Mapadre waendelee kutekeleza utume wao, ili watu wa Mungu waweze kufutiwa deni, kuwepo na uwajibikaji pamoja na mgawanyo mzuri wa rasilimali za dunia, kwani haya ndiyo matarajio ya watu wa Mungu, kila mtu akiwajibika barabara na kwamba, furaha ya Injili ni faraja kwa Mapadre na waendelee kusoma alama za nyakati na kwamba, ni Mwenyezi Mungu anayetenda kazi ndani mwao anayewapaka wafuasi wake kwa mafuta ya furaha. Kardinali Domenico Calcagno anasema waamini ni vyombo na mashuhuda wa Injili ya matumaini, waendelee kusali kwa ajili ya kuwakumbuka na kuwaombea Mapadre wao ili kweli wawe ni vyombo na mashuhuda wa furaha ya Injili, wawe pia ni vyombo vya ukombozi unaorutubishwa kwa Sakramenti za Kanisa. Mapadre wanazungukwa na vitendo vya ukosefu wa haki msingi, lakini wakumbuke kwamba, “Kwa maana jinsi hii Mungu aliupenda ulimwengu, hata akamtoa Mwanawe pekee, ili kila mtu amwaminiye asipotee, bali awe na uzima wa milele. “Mwenyezi Mungu amemtoa Mwanae wa pekee ili aweze kuganga na kuponya madonda ya waja wake; awafute machozi na “tazama yu aja na mawingi.” Ufu 1:7. Ufalme na utukufu ni vyake milele yote.

Alhamisi Kuu 2025
17 Aprili 2025, 16:15