杏MAP导航

Tafuta

Kardinali Robert Francis Prevost, O.S.A., Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa kwa ajili ya Wakleri, Jumatatu tarehe 4 Machi 2025 amewaongoza watu wa Mungu kusali Rozari Takatifu kwa ajili ya kumwombea Baba Mtakatifu Francisko. Kardinali Robert Francis Prevost, O.S.A., Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa kwa ajili ya Wakleri, Jumatatu tarehe 4 Machi 2025 amewaongoza watu wa Mungu kusali Rozari Takatifu kwa ajili ya kumwombea Baba Mtakatifu Francisko.  (VATICAN MEDIA Divisione Foto)

Watu Wa Mungu Wanasali Kumwombea Baba Mtakatifu Francisko: Hali Ni Tete

Na habari kutoka kwa Dr Matteo Bruno, Msemaji mkuu wa Vatican zinabainisha kwamba Jumatatu, tarehe 3 Machi 2025, Papa alikabiliana na changamoto ya kupumua papo kwa hapo, changamoto iliyoshughulikiwa na kupatiwa ufumbuzi. Wakati wa mchana madaktari walimwekea mashine ya kupumlia na wakati wote, ameendelea kuwa macho, akitambua kile kilichokuwa kinaendelea sanjari na kuonesha ushirikiano mkubwa na kwamba, Usiku alipata usingizi mnono!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Bwana awabariki na kuwalinda, Bwana awaangazie uso wake na kuwahurumia, Bwana awainulie uso wake na kuwapa amani. Ni maneno ya baraka kwa mwanzo wa Mwaka Mpya kutoka katika Maandiko Matakatifu. Hes 6:22-27. Ni maneno yaliyosheheni nguvu, ujasiri na matumaini yasiyo danganya kwani matumaini haya yanapata chimbuko lake kutoka katika baraka ya Mwenyezi Mungu na matashi mema ambayo Mama Kanisa anapenda kumpatia kila binadamu, kwa kukimbilia tunza na upendo wa Mungu. Matashi haya yanapata utimilifu wake kwa Bikira Maria, Mama wa Mungu. Hali inayoonesha ubora, dhamana katika imani ya Kikristo. Hii ni sehemu ya mahubiri yaliyotolewa na Baba Mtakatifu Francisko kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican wakati wa Maadhimisho ya Sherehe ya Bikira Maria Mama wa Mungu, sanjari na Siku ya 47 ya Kuombea Amani Duniani kwa Mwaka 2014. Baba Mtakatifu Francisko anasema, Bikira Maria daima amekuwa mioyoni mwa waamini, katika Ibada lakini kwa namna ya pekee katika hija ya imani ambayo ilifanywa na Bikira Maria katika maisha yake na waamini wanajitahidi kuifuatilia. Bikira Maria ni kielelezo makini cha fadhila ya imani, kwani katika maisha yake hapa duniani ametembea katika njia ya maisha na matatizo kama binadamu wengine, lakini daima amekuwa ni hujaji wa imani ambaye Kristo Yesu alimkabidhi kuwa ni Mama wa Kanisa pale chini ya Msalaba.

Bikira Maria Mama wa Mungu na Kanisa, chombo cha matumaini.
Bikira Maria Mama wa Mungu na Kanisa, chombo cha matumaini.

Baba Mtakatifu anasema pale ambapo Kristo Yesu aliona imani ya wafuasi wake inatindika kutokana na matatizo, kinzani na changamoto akawakabidhi kwa Mama yake Bikira Maria, mwamini wa kwanza kuamini, Mama ambaye imani yake haikupungua hata kidogo! Bikira Maria akawa Mama wa wote pale alipomwona Mwanaye wa pekee akiyamimina maisha yake kwa ajili ya ukombozi wa ulimwengu. Moyo Mtakatifu wa Bikira Maria ukafunuliwa wazi, ili utoe hifadhi kwa wema na wabaya, kwa kupenda kama vile Kristo Yesu mwenyewe alivyopenda. Kielelezo makini cha ushuhuda wa imani pale kwenye Arusi ya Kana ya Galilaya, alipofanikiwa kuwaonesha watu wa Mataifa utukufu wa Mungu. Pale Mlimani Kalvari, moto wa imani uliendelea kuwaka katika Ufufuko wa Mwanaye Mpendwa kwa kuwashirikisha wengine, kwa njia hii, Bikira Maria akawa ni chemchemi ya matumaini na furaha ya kweli! Baba Mtakatifu Francisko alihitimisha mahubiri yake kwa kusema kwamba, Bikira Maria Mama wa Mkombozi anawatangulia waamini, ili kuwaimarisha katika imani, wito na utume wa Kanisa. Kwa njia ya mfano wake wa unyenyekevu, utayari katika kutekeleza mapenzi ya Mungu anawawezesha waamini kumwilisha imani yao katika hija ya Injili ya Furaha bila mipaka. Kwa njia hii, utume wa Kanisa utaweza kuzaa matunda yanayokusudiwa, kwani unaratibiwa na Umama wa Bikira Maria. Baba Mtakatifu akawaweka chini ya ulinzi na tunza ya Bikira Maria waamini wote katika hija ya imani, matamanio yaliyomo mioyoni mwao bila kusahau mahitaji yao msingi na yale ya ulimwengu katika ujumla wake; hasa kwa wale wenye njaa na kiu ya haki na amani.

Watu wa Mungu wanasali kumwombea Papa Francisko ili apone haraka
Watu wa Mungu wanasali kumwombea Papa Francisko ili apone haraka   (VATICAN MEDIA Divisione Foto)

Kardinali Robert Francis Prevost, O.S.A., Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa kwa ajili ya Wakleri, Jumatatu tarehe 4 Machi 2025 amewaongoza watu wa Mungu kusali Rozari Takatifu kwa ajili ya kumwombea Baba Mtakatifu Francisko ambaye kwa sasa anasumbuliwa na ugonjwa wa mkamba (Bronchitis) pamoja na Nimonia “Pneumonia" hali ya kuvimba kwa mapafu inayoathiri hasa vifuko vya hewa viitwavyo alveoli. Husababishwa na maambukizi ya virusi au bakteria na kwa nadra kwa vimelea. Huu ni ugonjwa unaoambatana na: kikohozi, maumivu ya kifua, joto jingi mwilini na upumuaji mgumu. Tangu Ijumaa tarehe 14 Februari 2025 Baba Mtakatifu Francisko amelazwa kwenye Hospitali ya Chuo Kikuu cha Agostino Gemelli iliyoko mjini Roma. Watu wa Mungu wametafakari mafumbo ya maisha na utume wa Kristo Yesu, kwa kujikita katika Matendo ya furaha, kwa kusimama pamoja na Bikira Maria Mama wa Mungu na Kanisa kusali kwa ajili ya afya ya Baba Mtakatifu Francisko. Bikira Maria, Mama tumaini takatifu, awasaidie na kuwafariji wale wote wanaokimbilia tunza na msaada wake, awape pia ishara ya faraja na matumaini, li kwa maombezi ya Bikira Maria, waamini wajionee uwepo angavu wa upendo wa Kristo Yesu. Ibada hii imeongozwa na “Sura ya Bikira Maria Mama wa faraja na matumaini.” Lengo la Sala hii ya Rozari Takatifu ni kumwombea Baba Mtakatifu ili aweze kupona haraka na hatimaye, kurejea tena kwenye maisha na utume wake.

Waamini wameitikia kwa wingi mwaliko wa kusali kwa ajili ya Papa Francisko
Waamini wameitikia kwa wingi mwaliko wa kusali kwa ajili ya Papa Francisko   (VATICAN MEDIA Divisione Foto)

Huu ni mwendelezo wa maadhimisho ya Ibada ya Misa Takatifu, pamoja na Ibada ya Kuabudu Ekaristi Takatifu kwa ajili ya kumwombea Baba Mtakatifu Francisko, Ibada zinazofanywa sehemu mbalimbali za dunia. Wakati huo huo wanadiplomasia pamoja na wawakilishi wa Mashirika ya Kimataifa mjini Vatican, wanaungana na watu wa Mungu kumwombea Baba Mtakatifu Francisko, kiongozi ambaye ameonesha upendeleo wa pekee kwa wagonjwa, maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa vipaumbele vya kijamii.Na habari kutoka kwa Dr Matteo Bruno, Msemaji mkuu wa Vatican zinabainisha kwamba Jumatatu, tarehe 3 Machi 2025 Baba Mtakatifu Francisko alikabiliana na changamoto ya kupumua papo kwa hapo, changamoto iliyoshughulikiwa na kupatiwa ufumbuzi. Wakati wa mchana madaktari walimwekea mashine ya kupumlia na wakati wote, Baba Mtakatifu ameendelea kuwa macho, akitambua kile kilichokuwa kinaendelea mwilini mwake sanjari na kuonesha ushirikiano mkubwa kwa madaktari na wauguzi wake. Usiku alipata usingizi mwanana na kwamba, Jumanne tarehe 4 Machi 2025 ameendelea na matibabu pamoja na mapumziko. Lakini kimsingi hali ya afya ya Baba Mtakatifu Francisko inabaki kuwa ni tete sana!

Rozari Takatifu
04 Machi 2025, 15:55