杏MAP导航

Tafuta

Papa Francisko: Utu, heshima na haki msingi za binadamu ni mambo yanayopaswa kupewa kipaumbele cha kwanza Papa Francisko: Utu, heshima na haki msingi za binadamu ni mambo yanayopaswa kupewa kipaumbele cha kwanza   (VATICAN MEDIA Divisione Foto)

Waamini Jengeni Utamaduni wa Kulinda Na kutetea Injili ya Uhai

Baba Mtakatifu Francisko anawapongeza na kuwatia shime wanawake, ili waweze kuwa na ujasiri wa kupokea zawadi ya uhai na kuilea kwa moyo wa ukarimu na upendo, ili kuandika kitabu cha maisha ya mwanadamu kinachosimikwa katika utamaduni wa upendo na Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo. Utu, heshima na haki msingi za binadamu ni mambo yanayopaswa kupewa kipaumbele cha kwanza na hivyo kuendelea kuonesha upendo na mshikamano wa dhati.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Mtakatifu Yohane Paulo II katika Wosia wake wa Kitume, “Evangelium vitae” yaani “Injili ya uhai”. Kwa ufupi anakazia kuhusu: Thamani ya maisha, ukuu, utu, heshima na haki msingi za binadamu kama zawadi kubwa kutoka kwa Mwenyezi Mungu. Hii ni Injili ya upendo wa Mungu kwa binadamu; Utu na heshima yake, mambo msingi yanayofumbatwa katika Injili. Katika ulimwengu mamboleo kuna mambo ambayo yanaendelea kutishia Injili ya uhai kwa kukumbatia utamaduni wa kifo. Haya ni matokeo ya watu kukengeuka pamoja na kuporomoka kwa kanuni maadili na utu wema. Kuna sera na mikakati mbali mbali ya kisiasa, kiuchumi na kijamii inayotishia Injili ya uhai, ustawi na maendeleo ya wengi. Mtakatifu Yohane Paulo II anawataka waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kusimama kidete: kuheshimu, kulinda na kuhudumia Injili ya uhai, ili kukuza na kudumisha haki, maendeleo fungamani ya binadamu, uhuru wa kweli, amani na furaha ya kweli inayobubujika kutoka katika sakafu ya maisha ya mwanadamu. Waamini wanapaswa kujipambanua kuwa ni watu wanaotetea Injili ya uhai kwa ajili ya maisha. Hata leo hii bado kuna damu ya watu wasiokuwa na hatia inaendelea kumlilia Mwenyezi Mungu. Haya ndiyo mauaji ya kimbari na vita. Kuna sera za utoaji na uzuiaji mimba; kifo laini pamoja na uzalishaji kwa njia ya chupa. Maendeleo ya sayansi na teknolojia yamepelekea hata mauaji ya watoto wenye ulemavu kuanzia tumboni mwa mama zao. Yote haya ni matokeo ya uhuru unaoshindwa kutambua: utu, heshima na haki msingi za binadamu.

Jubilei ya Miaka 50 ya Chama cha Harakati za Kutetea Uhai
Jubilei ya Miaka 50 ya Chama cha Harakati za Kutetea Uhai   (Vatican Media)

Kumbe, kuna haja kwa waamini na watu wote wenye mapenzi mema kujenga na kudumisha Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo kwa kutambua uwepo angavu wa Mungu na kuzingatia kanuni maadili na utu wema, kwa kuimarisha matumaini pamoja na maboresho katika huduma ya tiba ya mwanadamu. Jitihada hizi hazina budi kwenda sanjari na mchakato wa kupinga adhabu ya kifo na kwamba, umefika wakati wa kuachana na dhana ya “vita halali na ya haki”, ili kujenga na kudumisha kanuni maadili zinazolenga kukuza na kudumisha misingi ya haki na amani, pamoja na kupambana dhidi ya mauaji ya kimbari.Mtakatifu Yohane Paulo II anasema, Kristo Yesu ni chemchemi ya utimilifu wa maisha, mwaliko kwa waamini kuwa ni vyombo na mashuhuda wa Injili ya uhai, kwa sababu maisha ni tunu adhimu inayofumbatwa katika maadili na maisha ya kiroho. Ikumbukwe kwamba, utukufu wa Mungu unang’aa katika sura ya mwanadamu kama kielelezo cha hali ya juu kabisa cha ufunuo wa utimilifu wa upendo wake ambao ni zawadi ya maisha ya uzima wa milele. Hii ni changamoto kwa waamini kudumisha upendo kwa Injili ya uhai, kwa kuwajibika barabara kulinda na kudumisha maisha. Utu, heshima na haki msingi za watoto ambao hawajazaliwa zinapaswa kulindwa na wote. Maisha yana thamani hata katika mateso, magonjwa na uzee kama yanavyofafanuliwa katika Amri za Mungu. Huu ni mwaliko wa kuendelea kuwa waaminifu katika Sheria na Injili ya uhai. Kristo Yesu, kwa mateso, kifo na ufufuko wake ameonesha kilele cha ufunuo wa Injili ya uhai. Msalabani, Kristo Yesu alionesha ukuu na utukufu wake, chemchemi ya maisha mapya na mwaliko kwa Wakristo kusimama kidete kulinda Injili ya uhai.

Waamini wanahamasishwa kujenga utamaduni wa kutetea Injili ya Uhai
Waamini wanahamasishwa kujenga utamaduni wa kutetea Injili ya Uhai   (Vatican Media)

Mtakatifu Yohane Paulo II anasema, Usiue kwa sababu maisha ya mwanadamu ni matakatifu na yasioharibika na kwamba, Mwenyezi Mungu ni chanzo na utimilifu wa maisha ya binadamu. Kanisa linalaani vitendo vyote vya utoaji mimba, kifo laini au watu kujinyonga kwa sababu hii ni dhambi dhidi ya utu, heshima na haki msingi za binadamu. Huruma na upendo ni urithi na amana ya ubinadamu. Mwanadamu anapaswa kuheshimu Sheria na Amri za Mungu, kanuni maadili na utu wema. Upendo kwa Mungu na jirani, usaidie kulinda na kudumisha Injili ya uhai. Mtakatifu Yohane Paulo II analihamasisha Kanisa kujenga na kudumisha utamaduni mpya wa maisha kwa kulinda na kutetea Injili ya uhai; kwa kutangaza na kuadhimisha Injili ya upendo unaomwilishwa katika huduma, ili kuenzi: ukuu na utakatifu wa maisha. Injili ya uhai iwe ni sehemu ya maisha ya sala ya kila siku, maadhimisho ya Sakramenti za Kanisa pamoja na Liturujia ya Mwaka wa Kanisa. Huu ni mchakato wa ushuhuda wa imani tendaji unaozingatia mpango wa uzazi kwa njia ya asili. Kwa kutambua kwamba, familia ni tabernakulo ya Injili ya uhai; kwa kuwalinda na kuwahudumia watu wanaoteseka kwa uzee na magonjwa ya muda mrefu. Ni katika muktadha huu wa kuenzi na kudumisha Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo, Chama cha Harakati za Kutetea Uhai “The Movement for Life (MpV)” kinaadhimisha Jubilei ya Miaka 50 tangu kuanzishwa kwake. Chama hiki kilianzishwa tarehe 22 Mei 1975 ili kulinda na kutetea Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo unaofumbatwa katika sera za utoaji mimba na kifo laini. Chama kinapania kutoa hifadhi kwa watu dhaifu ndani ya jamii, hasa watoto ambao wametungwa mimba na bado hawajazaliwa. Lengo ni kuenzi mamlaka fundishi ya Kanisa “Magisterium”, Mafundisho Jamii ya Kanisa pamoja na Mapokeo hai ya Kanisa.

Simameni kidete kulinda na kutetea Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo
Simameni kidete kulinda na kutetea Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo   (VATICAN MEDIA Divisione Foto)

Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe wake, aliouandika akiwa Hospitalini Gemelli, tarehe 5 Machi 2025, anawapongeza na kuwatia shime wanawake, ili waweze kuwa na ujasiri wa kupokea zawadi ya uhai na kuilea kwa moyo wa ukarimu na upendo, ili kuandika kitabu cha maisha ya mwanadamu kinachosimikwa katika utamaduni wa upendo na Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo. Utu, heshima na haki msingi za binadamu ni mambo yanayopaswa kupewa kipaumbele cha kwanza na hivyo kuendelea kuonesha upendo na mshikamano na watoto ambao bado hawajazaliwa; watoto wanaotolewa mimba. Ujumbe wa Baba Mtakatifu Francisko umesomwa kwa niaba yake na Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican wakati wa maadhimisho ya Ibada ya Misa Takatifu kama sehemu ya kumbukizi ya Miaka 50 tangu kuanzishwa kwa Chama cha Harakati za Kutetea Uhai “The Movement for Life (MpV)”. Baba Mtakatifu Francisko anawatia shime wajumbe wa Chama hiki kuendelea kusimama kidete kutangaza na kushuhudia Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo; kwa kujisadaka bila ya kujibakiza kulinda, kutetea na kudumisha Injili ya uhai katika hatua zake mbalimbali. Ikumbukwe kwamba, maisha ni matakatifu na kwamba, hii ni zawadi kubwa kutoka kwa Mwenyezi Mungu. Huu ni mwaliko kwa watu wa Mungu nchini Italia kupyaisha tena utamaduni wa upendo; kwa kutoa kipaumbele cha kwanza kwa utu, heshima na haki msingi za binadamu sanjari na kuwekeza katika ustawi, maendeleo na maisha bora kwa wanawake. Chama hiki kinawatunza zaidi ya watoto 270, 000, ushuhuda wa Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo. Kardinali Parolin, ametambua mchango mkubwa uliotolewa na Muasisi wa Chama hiki Carlo Casini (1935-2020.)

Papa Injili ya Uhai
11 Machi 2025, 15:56